Maisha gerezani: Kwa nini magereza ya Amerika ya Kusini yana msongamano mkubwa?

Ghasia za magereza za Septemba huko Ecuador zilizosababisha vifo vya watu 119, huku wengine wakiwa wamekatwa vichwa, zimeibua tena suala la msongamano magerezani.

Wataalamu wanalaumu miongoni mwa mambo mengine msongamano mkubwa wa watu magerezani unaofikia asilimia 133% - au, kwa maana nyingine kwenye kila sehema ya wafungwa 100 wapo wafungwa 133.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi nchini, magereza 52 ya Ecuador yanahifadhi zaidi ya wafungwa 39,000 - ikiwa ni wafungwa 10,000 zaidi ya idadi inayotakiwa.

Mauaji katika gereza la Guayaquil yalikuwa ya tatu kurekodiwa katika magereza ya Ecuador kwa mwaka wa 2021. Mwezi Februari, watu 79 walikufa kabla ya mauaji mengine ya watu 22 kutokea mwezi Julai.

Pamoja na haya, Ecuador si miongoni mwa nchi 10 za juu za Amerika Kusini na Caribbean zenye magereza yenye msongamano mkubwa zaidi.

Kwa sasa inashika nafasi ya 18 katika orodha iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Sera ya Uhalifu na Haki ya Uingereza (ICPR), kama sehemu ya mradi unaoitwa World Prison Brief.

Ili kujua ukubwa wa tatizo, ni vyema kutambua kwamba ni taifa moja tu la Amerika Kusini ambalo halina magereza yenye msongamano: Suriname, lililopo pwani ya kaskazini-mashariki mwa Amerika Kusini, likiwa na kiwango cha wafungwa takribani asilimia 75.2%.

Chile inashika nafasi ya pili kwa kuwa na magereza yenye msongamano mdogo zaidi, kwa kiwancgo cha 100.4% - na sawa na asilimia 0.4% zaidi ya uwezo wake.

Hili linafanana na hali ilivyo Amerika ya Kati: Belize ni nchi pekee ambayo haina magereza yenye watu wengi zaidi, ina wafungwa 49.8% tu sawa na kusema wafungwa waliopo hawafikii hata nusu ya uwezo wa magereza yake. Mexico iko juu kidogo ya uwezo wake, ikiwa na kiwango cha 101.8%.

Kwa hivyo, idadi kubwa ya nchi za Amerika ya Kusini huwa na wafungwa wengi zaidi ya uwezo wao, kukiwa na wastani wa 160%.

Katika baadhi ya nchi kiwango cha wafungwa ni mara mbili, tatu au hata mara nne ya uwezo wake.

Nchi sita zenye magereza yenye wafungwa wengi zaidi

Nchi yenye idadi kubwa zaidi ni Haiti. Hii ni nchi maskini zaidi katika bara la Amerika, ikiwa na idadi ya watu gerezani kwa kiwango cha 454.4% - ni zaidi ya mara 4 na nusu ya uwezo wake. Inafuatiwa na Guatemala, ambayo ina wafungwa mara tatu zaidi ya uwezo wake ikiwa na kiwancgo cha 367.2%. Kisha inakuja Bolivia, yenye 269.9%.

Mataifa haya matatu yana kati ya magereza kumi yenye watu wengi zaidi duniani.

Lakini kwa nini nchi hizi, na Amerika ya Kusini kwa ujumla, zina tatizo kubwa la msongamano wa wafungwa magereza?

Jela chache sana?

Unaweza kudhani tatizo hili la wafungwa wengi lipo kwa sababu kuna magereza machache. Unaweza kuwa sahihi kwa kiasi fulani. Idadi ya watu magerezani inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko idadi ya selo za za magereza.

Lakini wataalam wanasema kujenga magereza zaidi hakutatatua tatizo la msongamano.

"Tunajua kwamba kadiri magereza yanavyojengwa, ndivyo yatakavyokaliwa zaidi," anasema Sacha Darke, anayesomea uhalifu katika Chuo Kikuu cha Westminster cha Uingereza, ambaye ni mtaalamu wa mifumo ya magereza ya Amerika Kusini.

Darke anasema kuwa idadi ya wafungwa katika eneo hilo imeongezeka karibu mara tatu tangu 2000 na kuliita Amerika Kusini kama "eneo jipya la watu wengi kufungwa".

"Itaipita Amerika Kaskazini," anasema, akimaanisha eneo lenye wafungwa wengi zaidi duniani, lakini bila matatizo mengi ya msongamano, licha ya idadi kubwa ya wafungwa.

Leo, Marekani ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa duniani, kwa ujumla (zaidi ya watu milioni 2) na kwa kiwango cha wafungwa kwa kila magereza inayopaswa kukaliwa na wafungwa 100,000 kuna wafungwa 629).

Katika bara la Amerika ya Kusini, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wafungwa ikitoka 650 elfu hadi milioni 1.7.

Ripoti ya ICPR inaonyesha kuwa kati ya 2000 na 2018 idadi ya wafungwa duniani iliongezeka kwa 24%, kulingana na ukuaji wa idadi ya watu kwa ujumla. Lakini katika katika bara la Amerika Kusini ongezeko lilikuwa kubwa kwa asilimia 175%.

Sababu ni nini hasa?

Tatizo la mahakama

"Tatizo kuu ni mfumo wa haki ya jinai, si mfumo wa magereza, ambao hauamui nani atakamatwa," anasema César Muñoz, mtafiti mkuu katika Human Rights Watch (HRW) katika Amerika ya Kusini.

Muñoz anaashiria mapungufu mawili mahususi ya mfumo wa haki ya jinai: upole na "matumizi makubwa kupita kiasi ya kuwaweka watu mahabusu kabla ya kesi".

Kwa mujibu wa takwimu za Muhtasari wa Magereza Duniani, Asilimia 81.9% ya wafungwa nchini Haiti wanashikiliwa bila kufunguliwa mashitaka.

Nchini Paraguay idadi hii ni asilimia 71.7%. Nchini Bolivia, 65%. Na, nchini Brazil, karibu 40% ya wafungwa bado hawajahukumiwa.

Kwa wastani, zaidi ya 40% ya wafungwa katika bara la Amerika Kusini wako ndani bila kuhukumiwa.

Na kesi zikiwa mahakamani zinaweza kuchukua muda mrefu mpaka miaka - na hilo kuongeza shinikizo la idadi ya wafungwa.

Sera ya madawa ya kulevya

Hili nalo linatajwa kama sababu nyingine inayochangia.

"Leo moja ya sababu kuu inayochangia sana watu kuwa magerezani ni kuuza dawa za kulevya," anasema Sacha Darke.

"Watu wengi wanaokamatwa si wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya, bali ni vijana wanaokutanisha wauzaji na wanaonunua," anasema.

"Katika bara la Amerika ya Kusini, kila mtu anayeuza dawa za kulevya anaitwa muuza dawa za kulevya, lakini huko Ulaya ni wale tu wanaojishughulisha moja kwa moja wana jina hilo.

Magenge ya uhalifu

Katika kitabu cha 'Prisons and Crime' kilichochapishwa mwaka huu, Gustavo Fondevila na Marcelo Bergman wanasisitiza kwamba magereza yametoka kwenye "vyombo vya kutofanya kazi, kuzuia na kurekebisha tabia na kuwa waendelezaji wa vurugu na uhalifu".

Mbali na Ecuador, mapigano kati ya vikundi vya wahalifu vinavyodhibiti magereza yamesababisha mauaji katika nchi kadhaa za eneo hilo, kama vile Peru na Venezuela.

Katika gereza la Alcaçuz nchini Brazili, huko Rio Grande do Norte, wafungwa 26 waliuawa mwaka wa 2017 wakati wa mzozo kati ya vikundi viwili vya uhalifu. Huko Manaus, katika mwaka huo huo, wafungwa 56 waliuawa katika mapigano kati ya vikundi.

Machafuko

Mwaka 1992, Brazili ilishuhudia mauaji makubwa zaidi ya gereza, huko Carandiru, São Paulo, wakati wafungwa 111 walipouawa na polisi wakati wa askari walipolazimika kuingilia kati ghasia.

Wataalamu wanaonya kuwa jela zilizojaa sana zina mchango mkubwa wa nguvu za magenge.

"Msongamano wa magereza unachochea ukuaji wa mitandao ya uhalifu kwa sababu kuna udhibiti mdogo wa serikali," anasema Cezar Muñoz.

Anatoa mfano: "Ikiwa una selo ambayo ina uwezo wa kuhifadhi watu watano, lakini ina 30, walinzi hawawezi kuweka udhibiti wa mahali hapo. Kwa hivyo msongamano unachochea ukuaji wa vikundi vya uhalifu."

"Kwa kweli, katika eneo hili tuna kesi nyingi za vikundi vya uhalifu ambavyo viliundwa magerezani na kisha kufanya biashara zao haramu nje."

Sacha Darke, kwa upande wake, anasema kwamba katika nchi nyingi mamlaka za magereza "zinahitaji magenge ili kuandaa operesheni ya gereza hilo".

"Katika baadhi ya maeneo, magenge haya hata huteuliwa na mfumo wa magereza ili kudumisha utulivu," anasema.