Yafahamu mataifa matano yaliyofuzu fainali za kombe la dunia kwa 'bahati ya mtende'

Chanzo cha picha, Getty Images
Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars inaongoza kundi J kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia zitakazochezwa huko Qatari mwaka 2022.
Tanzania inaongoza kundi hilo baada ya ushindi wa kihistoria ugenini dhidi ya Benin Jumapili hii na kuweka hai matumaini yake ya kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Saimon Msuva anayecheza soka lake Morroco, ndiye aliyeipatia bao pekee 'Taifa stars' katika mchezo huo ambao, Stars ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya kupata hata sare. Kwa ushindi huo, Stars inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 7 sawa na Benin anayepigiwa chapuo kuongoza kundi hilo, ambalo lina timu za Madagascar na DRC.
Ukiacha Ghana na Cameroon mataifa ya Algeria, Tunisia, Nigeria, Ivory Coast, Stars, Mali, Misri, Afrika Kusini, Senegal, Morroco yalikuwa yanaongoza makundi hayo kabla ya michezo ya Jumatatu hii. Tanzania kuongoza kundi lake baada ya michezo minne ikiungana na mataifa hayo makubwa kisoka Afika, kumeleta hamasa kubwa kiasi mpaka Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu kutoa neno la kuwapongeza.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Ni hatua ya kufikirika, kabla ya kuanza kwa michuano hiyo mwaka huu, lakini Tanzania imeigeuza kuwa ya kweli ikisalia na michezo miwili dhidi ya DRC nyumbani na Madagascar ugenini. Ushindi wowote katika mechi hizo, huenda ikaivusha kimaajabu taifa hilo katika hatua inayofuata ya mtoano itakayojumuisha mataifa 10 yaliyoongoza makundi, yatakayocheza ili kupata timu 5 zitakazoiwakilisha Afrika.
Wakati Tanzania, kukiwa na furaha na mijadala mikubwa kuhusu uwezekano usiotarajiwa wa taifa hilo hilo la Afrika mashariki kufuzu fainali zijazo za kombe la dunia. BBC inakuletea orodha ya mataifa ambayo yalifuzu michuano hiyo, yakiwa hayajapewa kipaumbele wala kufikiriwa na walio wengi.
5. Trinidad & Tobago - 2006

Chanzo cha picha, Google
Ilikuwa timu pekee kutoka Caribbean kufuzu hatua ya mwisho ya kufuzu michuano ya kombe la dunia kutoka ukanda wa CONCACAF. Trinidad & Tobago ilikuwa ikifanya vibaya mara nyingi ikiwa timu inayoshika mkia, lakini mwaka 2006 ilijikuta ikicheza mtoano na Bahrain.
Mataifa kama Honduras na Jamaica hayakuwepo , na kuiacha Trinidad ikielekea kupigana vikumbo na mataifa kama Marekani, Mexico na Costa Rica kabla ya kuiondosha Bahrain katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini.
Katika fainali zenyewe za kombe la dunia, ilianza kwa kupata sare ya 0-0 dhidi ya Sweden katika hatua ya makundi kabla ya kukomaa katika mchezo dhidi ya England, waliohitaji kufanya kazi ya ziada kupata ushindi. Waliondolewa baada ya mchezo wa tatu wa makundi baada ya kuchapwa na Paraguay. Hakuna aliyewatarajiwa wangefuzu, achilia mbali kupata alama moja kwenye fainali hizo.
4. Jamaica - 1998

Chanzo cha picha, Google
Jamaica ililazimika kucheza michezo 20 katika raundi nne za kufuzu fainali za kombe la dunia mwaka 1998 kutoka ukanda wa CONCACAF. Ilifuzu kwa mara ya kwanza na pekee fainali za kombe la dunia, ikiwa nchi ya 3 kutoka kisiwa cha Caribbean kufuzu kombe la dunia, baada ya Cuba (1934) na Haiti (1974).
Wachezaji wengi wa timu hii maarufu kama Reggae Boyz walikuwa wanacheza soka kwenye vilabu vya nchi hiyo, ukiacha wachache waliozaliwa England kama Robbie Earle, Marcus Gayle, Frank Sinclair Darryl Powell na Deon Burton.
Hata hivyo Jamaica ilitolewa mapema tu kwenye fainali hizo baada ya kutandikwa 3-1 na Croatia kabla ya kupiga 5-0 na Argentina (0-5), lakini walifanikiwa kupata ushindi katika mechi ya tatu dhidi ya Japan waliokuwa wageni pia wa michuano hiyo.
3. Angola - 2006

Chanzo cha picha, WP
Fainali za kombe la dunia za mwaka 2006 , zilishuhudia timu nne kati ya tano kutoka Afrika zikicheza kwa mara ya kwanza fainali za michuano hiyo. Mataifa kama Ivory Coast na Ghana yalikuwa yanaonekana kukaribia kufuzu na yenye wachezaji wengi wenye vipaji ambao kufuzu kwake, kusingeshangaza sana, lakini kufuzu kwa Angola kulishangaza wengi mwaka 2016. Hakuna aliyetarajia.
Ikiwa koloni la Ureno mpaka mwaka 1975 ilipopata uhuru, ilipitia hali mbaya ya miaka 27 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mpaka mwaka 2002, hali ilipotulia kisoka na kuonekana kufanya vyema kwenye michuano mbalimbali. Angola ilimaliza juu ya vigogo Nigeria kwa tofauti ya mabao na kufuzu michuano ya kombe la dunia la 2006 nchini Ujerumani.
Kabla ya mwaka 2006, taifa hilo lilikuwa limefuzu mara tatu tu fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON0 ikiwemo mwaka huo wa 2006 ambao iliyolewa katika hatua za makundi. Kwenye fainali za kombe la dunia, ilimaliza ya tatu nyuma ya Ureno na Mexico, ikiambulia alama mbili, sare ya 0-0 dhidi ya Mexico na sare ya 1-1 dhidi ya Iran.
Ilichapwa 1-0 na Ureno katika mechi yake ya kwanza.
2. Togo - 2006

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama ilivyo kwa Angola, Togo lilikuwa taifa moja wapo kutoka Afrika lililoshiriki kwa mara ya kwanza fainali za kombe la dunia. Ilifuzu kwa kushangaza, hakuna aliyetarajiwa, baada ya kuifunga Senegal, waliotoka kuishangaza dunia kwenye fainali za mwaka 2002 kwa kuifunga Ufaransa 1-0, Iliyokuwa na wakali kama Zinedine Zidane, Thierry Henry, Claude Makelele, Marcel Desailly, Patrick Viera, Robert Pires, David Trezeguet, Lilian Thuram na Emanuel Petit.
Togo ilikuwa na nyota wake Emmanuel Adebayor siku chache baada ya kuhamia Arsenal akitokea Monaco, lakini kwa kiwango kikubwa ilikuwa na wachezaji ambao hawakuwa na majina kabisa. Wengi wao walikuwa wanacheza kwenye ligi za madaraja ya chini nchini Ufaransa, huku kipa wake wa pili akiwa mchezaji pekee anayecheza Afrika.
Kwa bahati mbaya hawakuweza kuwa na bahati ya kufanya vyema kwenye fainali hizo, wakifunga goli moja tu kwenye mashindano hayo lililofungwa na Mohamed Kader aliyekuwa anachezea klabu ya Guingamp katika mchezo wa ufunguzi waliolala kwa 2-1 dhidi ya Korea Kusini, baadae wakapata vipigo vya 2-0 kutoka kwa Switzerland na Ufaransa.
1. Dutch East Indies (Indonesia) - 1938

Chanzo cha picha, AFP
Kabla ya mwaka 1945 na kabla ya kupata uhuru kutoka kwa Uholanzi, Indonesia ilishiriki mashindano hayo kwa jina la 'Dutch East Indies' na ilishiriki fainali za mwaka 1938 nchini Ufaransa, ikawa nchi ya kwanza kutoka Asia kushiriki michuano hiyo.
Ilipata nafasi kwa bahati, kama embe kudondoka mtini. Ilipangwa kwenye kundi la timu mbili kupata mwakilishi wa Asia, ikiwa na Japan. Lakini Japan ikajitoa hivyo ikapata nafasi ya moja kwa moja kushiriki fainali za michuano hiyo.
Ikapata kipigo cha aibu kwenye fainali hizo za mwaka 1938 baada ya kupigwa 6-0 na Hungari iliyokuwa na kikosi kikali kilichofika fainali ya michuano hiyo. Hiyo ikawa mwisho wa safari yao ya kuonekana kimataifa. Tangu miaka hiyo, hakuna anayeijadili Indonesia kwenye ulimwengu wa soka mpaka hivi karibuni iliposimamishwa na shirikisho la soka ulimwenguni FIFA baada ya serikali kuingilia masuala ya soka. Ilisimamisha isishiriki michezo ya kufuzu zainali za mwaka 2018.














