Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Abdulrazak Gurnah: Mfahamu raia wa Tanzania aliyeshinda tuzo ya Nobel ya fasihi 2021
Mwandishi wa riwaya Mtanzania Abdulrazak Gurnah ametwaa tuzo ya fasihi ya Nobel mwaka huu. Kwa ushindi alioupata amejinyakulia kitita cha dola za kimarekani milioni $1.14 .
Tuzo hiyo hutolewa na kituo cha Sweden ikionyesha heshima kwa watu mahiri kwenye upande wa fasihi.
Lakini Abdulrazak Gurnar ni nani hasa?
Abdulrazak Gurnah ni mwandishi wa riwaya Mtanzania, anayeishi nchini Uingereza. Alizaliwa Disemba 20, mwaka 1948 visiwani Zanzibar.
Alikwenda Uingereza kama mwanafunzi mwaka 1968, miaka saba baada ya Tanzania kupata uhuru na amekuwa akiishi huko kwa muda mrefu na mpaka sasa ni mwalimu wa fasihi katika chuo kikuu cha Kent.
Mbali na kufundisha Gurnah amekuwa akifanya kazi za kuhariri nyaraka mbalimbali, vitabu na majarida na sasa ni mhariri wa jarida la 'Wasafiri.
Gurnah na tuzo ni damu damu
Gurnah si mgeni wa tuzo, amewahi kupata tuzo kadhaa huko nyuma kwa sababu ya umahiri wake wa kuandika riwaya zilizosaidia kuleta mageuzi.
Tuzo aliyopata mwaka huu ya fasihi ya Nobel, ni moja kati ya tuzo nyingi ndogo na kubwa alizowahi kuzipata katika maisha yake ya uandishi.
Mwaka 1994, akiwa ameanza kufahamika kwa uwezo wake wa kuandika riwaya, alifanikiwa kutwaa tuzo ya Booker Prize for Fiction, iliyoanza kumtambulisha kwenye ulimwengu wa waandishi.
Mwaka 2001 haukupita kavu, alifanikiwa pia kutwaa tuzo yake ya pili kubwa ya Los Angeles Times Book Prize (Fiction).
Kati ya tuzo zinazofahamika zaidi alizowahi kupata ni pamoja na ile aliyopata mwaka 2006, ya jumuiya ya madola iliyoitwa 'Commonwealth Writers Prize (Eurasia Region, Best Book)
Ukweli mchungu ndio silaha yake
Abdulrazak Gurnah anatambulika zaidi kwa namna anavyoamini suala la ukweli. Anasema falsafa ya uandishi wake ni ukweli, hata baada ya kushinda na kuulizwa na BBC falsafa ya uandishi wake ni kuzungumza ukweli. Gurnar anasema 'nadhani ni kuzungumza ukweli'.
Waandishi wengi wa riwaya, hasa wenye asili ya Afrika, huandika riwaya na vitabu mbali mbali kwa hadithi za kufikirika, lakini uthabiti wa Abdulrazak Gurnah ni kuandika ukweli na mambo mengi halisi.
Anaamini kwamba pamoja na kazi za aina nyingine za kuburidisha, kufundisha na kuelemisha kwa kutumia hadithi mbalimbali, lakini ukweli unapaswa kupewa kipaumbele.
Haishangazi kuona riwaya zake nyingi alizoandika kuhusu uhamiaji, alitumia uhusika uliofichua na kuanika uzoefu wa uhamiaji pamoja na maisha ya ujumla ya wahamiaji hasa wanaotoka Afrika na kuingia Ulaya.
Uhamiaji na watu kuyakimbia makazi yao, ama kutoka Afrika Mashariki kwenda Ulaya ama ndani ya Afrika ni masuala ambayo karibu riwaya zake zote zimejiegemeza huko. Na huko utabaini kile anachokisema, na kuonekana kama anakosoa lakini anazungumza kilichopo na anachoamini ndio ukweli wenyewe.
Utitiri wa vitabu vyake
Abdulrazak Gurnah, alikuwa tayari amepata sifa kama msomi na mkosoaji wa fasihi wa Kiafrika na alishawahi kuchapisha riwaya tatu kuhusu jamii ya wahamiaji nchini Uingereza mnamo 1994.
Riwaya hizo Memory of Departure (1987), Pilgrims Way (1988) na Dottie (1990), kuhusu masuala ya uhamiaji ikigusia zaidi huko Uingereza, zimemtambulisha zaidi kama mwandishi mzuri.
Riwaya yake ya nne Paradise (1994), iliyoangazia hadithi ya mvulana aliyekulia nchini Tanzania katika karne ya 20 na kushinda tuzo ya Booker na hivyo basi kuzidi kumtambulisha kama nguli wa riwaya.
Riwaya ya Admiring Silence (1996) inamzungukia kijana ambaye anaondoka Zanzibar na kwenda Uingereza kama mhamiaji ambapo anafika huko anapata mchumba anaoa na baadae anakuwa mwalimu. Ni riwaya ambayo kama inayomzungumzia yeye, ambaye alitoka Zanzibar miaka ya 1960's kwenda Zanzibar akaoa na sasa ni mkufunzi wa fasihi.
Abdulrazak Gurnah anaishi Brighton, mashariki mwa Sussex. Riwaya yake ya hivi karibuni ya Desertion (2005), iliorodheshwa kwenye riwaya zilizowania tuzo ya jumuia ya madola ya mwaka 2006 'Commonwealth Writers Prize' na riwaya nyingine aliitoa mwaka 2011 kwa jina The Last Gift (2011).
Vitabu alivyowahi kuandika na kupata umaarufu
2011 - The Last Gift
2007 - The Cambridge Companion to Salman Rushdie
2005 - Desertion
2001 - By the Sea
1996 - Admiring Silence
1994 - Paradise
1993 - Essays in African Literature: A Re-evaluation
1990 - Dottie
1988 - Pilgrim's Way
1987- Memory of Departure
Abdulrazak Gurnah, hafahamiki sana nyumbani kwao Tanzania kama nguli wa riwaya kama walivyo manguli wengine akiwemo Shaaban Robert , lakini kwa ushindi huu sasa, atajitambulisha vyema miongoni mwa Watanzania.