Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Mfahamu mwanamke aliyeamua kuwa 'kahaba' licha ya kujua hali yake
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Regina Jane, 25, kutoka nchini Kenya, ni mwanamke ambaye amepitia milima na mabonde maishani mwake kama anavyosimulia mwenyewe.
Mama huyo wa watoto wawili, anasema kuwa alifahamu mambo yake yanapaswa kuwa siri kwa watoto wake yaani ya maisha yake ya mapenzi kuanzia alipokuwa na umri wa miaka, 14, na ikawa hivyo, hadi alipojitumbukiza katika kazi haramu ya ukahaba akiwa na miaka 16.
Bila shaka sio simulizi yenye kuleta tabasamu lakini anachosisitiza ni kwamba dunia imekuwa somo kwake, hasa kupitia aina ya maisha aliyochagua kuishi hapo awali.
Maisha ya utotoni
Regina alizaliwa miaka 25 iliyopita, na anakiri kuwa alizaliwa na virusi vinavyosababisha maambukizi ya ukimwi - HIV, ila alifahamaishwa hayo baada ya kifo cha mama yake akiwa na umri wa miaka minane.
"Nilizaliwa katika jamii iliyokuwa na mzazi mmoja pekee, ambaye ni mama yangu. Sijawahi kumuona baba yangu hadi wa leo. Nikiwa mdogo nakumbuka mara nyingi nililelewa na bibi na babu yangu kwani mama yangu mzazi alikuwa anafanya kazi mbali na nyumbani kwetu", Regina anasema.
Aidha, anakumbuka akimuona mama yake akiwa anaugua mara kwa mara ila kutokana na umri mdogo aliokuwa nao, hakuelewa mengi kuhusu ugonjwa uliokuwa umemsibu mama yake.
Kwa hiyo mama yake alipofariki alibaki mikononi mwa babu na bibi yake.
Punde baada ya mama yake kufariki, Regina naye pia akaanza kuwa mgonjwa kila wakati kiasi cha yeye kulazwa hospitalini kwa muda mrefu.
Lakini wakati wataalam walipokuwa wanamfanyia vipimo mbalimbali hospitalini, aligundulika kuwa na virusi vya HIV akiwa na umri mdogo na ikawa vigumu kwake kuelezwa kipindi kile kilichokuwa kina mtatiza au hata kuelewa kuwa na virusi hivyo ilimaanisha nini ama kuwa na athari zipi katika maisha yake.
Baada ya hali yake ya afya kugunduliwa, alianza kumeza dawa za kumsaidia kuimarisha kinga mwilini - ARVs. Wakati alipokuwa anaanza kumeza dawa hizo, hakuelewa ni kwasababu ipi anatakiwa kuzinywa kila siku, na alipomuuliza bibi au babu yake hakuna aliyempa jibu kamili.
Hadi kufikia wakati huo, anakiri kuwa tukio hilo lilimsumbua akili na kumuacha na maswali mengi. Ilikuwa ada kwa babu kuhakikisha anameza tembe zake mbili tena kwa wakati, ila hakuna aliyekuwa tayari kumuelezea dawa hizo ni za nini.
"Nikiwa na miaka 12, kuelekea 13 hapo, nilikuwa nimeanza kukomaa na kuelewa mambo mbalimbali. Na pia wakati huo nilikuwa ninajipeleka mwenyewe kliniki kuchukua dawa zangu za mwezi mzima. Siku moja nikapata ujasiri na kumuuliza daktari ni kwanini mimi humeza dawa kila siku? Alinijibu kwa kunielezea hali yangu ya HIV, na kuniambia kuwa sina budi kumeza dawa hizo katika kipindi chote cha maisha yangu", Regina anakumbuka.
Mama huyo anasema kuwa nyumbani alitafuta sana majibu aliyopewa siku ile na daktari lakini kwa kuwa mama yake alifariki kutokana na ugonjwa wa ukimwi, ilisalia kuwa siri kubwa iliyolindwa kama dhahabu katika boma lile na ukweli wa kwamba mama yake alikuwa amemwambukiza Regina virusi hivyo akiwa bado mtoto mchanga, hilo nalo likawa mwiko kuzungumziwa ama na babu au bibi yake.
Regina anasema ni hali aliyoikubali japo shingo upande, wakati huo alitamani sana kama maneno aliyoarifiwa hospitalini yangetoka kwa wapendwa wake, ila haikuwa hivyo.
Alipofikisha miaka 14 alikuwa ameanza kubaleghe, na hapo ndipo alipoanza urafiki japo kwake yeye ulikuwa urafiki wa kawaida tu na mwanamume mtu mzima. Urafiki huo uliendelea kwa muda na kubadilisha kabisa mkondo wa maisha yake.
"Nikiwa darasa la saba nilikuwa nimeanza kuhudhuria warsha zilizokuwa zinahusu wanarika na watoto waliokuwa wamezaliwa na virusi vya HIV. Nilikuwa ninasafiri umbali mrefu kiasi kuhudhuria shughuli hizo na hapo ndipi nilipokutana na mwanamume mmoja ndani ya gari la usafiri wa umma, aliyeanza kuonyesha hisia za mtu mkarimu. Sikuwa na wasiwasi naye kabisa licha ya kwamba ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana naye. Alisisitiza kwamba angenitembelea kwetu kesho yake," Regina anasema.
Ziara ya mwanaume huyo kumuona Regina, iliishia kwa kitendo cha kunajisiwa kichakani na hiyo ikawa mara yake ya mwisho kumtia machoni.
Kilichofuata, Regina alibainika kuwa mjamzito. Wakati huo, alikuwa bado ni mwanafunzi wa shule ya msingi. Kibaya zaidi, ukawa ndio mwisho wa safari yake ya kutafuta elimu na kulazimika kukumbatia majukumu yakuwa mlezi.
Na hadi anaanza utekelezaji wa jukumu la kuwa mama baada ya kupata mtoto wa kiume, Regina alikuwa anakabiliwa na unyanyapaa, chanzo cha hilo ikiwa ni kukosa kumnyonyesha mtoto wake. Baadhi ya kina mama wenzake walianza kumsema na kumsimanga.
Muda si muda, taarifa hizo zikawa gumzo mtaani, jambo lililomuathiri mno kisaikolojia kiasi cha hata kufanya uamuzi wa kukosa kumeza tembe zake kwa kipindi cha miezi minane.
Ndani ya miezi hiyo, akawa yuko mbioni kujaribu kutumia kila njia kubadilisha uhalisia wa hali yake ya kuwa mwathirika wa virusi vya HIV mbele ya watu.
'Nilidhani kuwa nikiombewa nitapona'
Kwasababu ya changamoto alizokuwa anakumbana nazo kipindi kile, Regina aliamua kuwa muumini wa dhehebu moja, na kuamini kwamba maombi maalum aliyopata katika eneo hilo la ibada, yangebadilisha hali yake ya afya.
"Nilikuwa ninaabudu katika eneo moja la ibada, hii ni baada ya kuelezewa kuwa nikiombewa nitapona. Mimi niliamini hilo kwa asilimia 100, na nilipojipeleka kliniki kupimwa tena, bado nikapatikana na HIV. Yule mhudumu wa afya alinipa nasaha ya kwamba licha ya kuwa naendelea kupokea maombi, nisiache kumeza dawa zangu", anasema Regina.
Hayo yote Regina anasema yalikuwa mahangaiko ya kujitafutia tiba akiwa na matumaini kwamba hatimaye atapona kabisa virusi vya HIV.
Regina anakiri kuwa kuna kipindi maishani mwake alihisi machungu mengi na pia kujiuliza maswali chungu nzima kuhusu wajibu wa mama yake marehemu katika maisha aliyokuwa anaishi.
Fikra zilizotokana na ukweli kwamba aliyemuambukiza alikuwa mama yake mzazi aliyeamua kumnyonyesha licha ya kufahamu kwamba ana virusi hivyo ilhali alikuwa na kiu sana ya kumsamehe kwa dhati ya moyo wake hata kama hakuwepo tena duniani.
Majuto ya kuingia kwenye ukahaba
Baada ya Regina kujifungua alifahamu fika kuwa hangeendelea kuishi na babu yake na kuamua kuanza kufanya biashara mbalimbali kama njia ya kijitafutia riziki aweze kujikimu kimaisha.
Akiwa bado anajitafuta, baadhi ya rafiki zake wa kike aliokuwa anatembea nao walimshawishi kuingia katika biashara ya ukahaba.
''Nilisafiri kutoka kwetu Lamu hadi Mombasa. Nikiwa kule nilikutana na mwanadada mmoja aliyenikaribisha kwenye kazi ya ukahaba. Sababu kubwa iliyopelekea mimi kukubali kazi hii, ni kutokana na kuwa nilijiona kama mwanamke aliyefeli maishani. Nilikuwa na umri mdogo wa miaka 16 na kuamini kwamba ingekuwa vyema ikiwa nitachagua njia ya mkato kujikimu kwa kuuza mwili wangu", Regina anasema.
Na bila kufikiria mara mbili, Regina akajitosa kwenye biashara haramu ya ukahaba. Kila usiku hata wakati mwingine mchana, alijipeleka katika mitaa mbalimbali kusaka wateja.
"Sio kwamba biashara ya ukahaba ni kazi yenye tija. Niligundua kuwa wanawake wengi wakiwa makahaba huwa wanadharauliwa mno kwani kuna wakati mwingine ningekutana na wateja ambao wanalipa kunitumia tu, na baada ya hapo wanakuona kama chombo chao", Regina anakumbuka.
Kazi ya ukahaba na HIV
Je biashara ya ukahaba ilikuwaje ilihali alikuwa anajuwa kwamba ana virusi vya HIV?
Regina anasema kwamba alikuwa akiwaeleza ukweli baadhi ya wateja wake ila wengi ni wale ambao hawakumsikiliza ama walikuwa wakaidi wa kuwajibikia hali yao ya kiafya.
Mama huyo anasema katika biashara ya ukahaba, idadi kubwa ya wateja aliotoka nao, hawakuwa wanatumia mipira ya kondomu hata baada ya kuwatahadharisha mara kwa mara.
"Nilikuwa ninaamini ya kuwa ni wajibu wa kila mtu mzima kujijali, na wakati wanaamua kushiriki ngono na makahaba wajikinge".
Regina anasema safari yake hii ilikuwa na panda shuka za aina yake na hata kama ilimpa riziki kwa zaidi ya miaka minne, hasara ni nyingi sana kuliko hata mapato aliokuwa anapata.
Bado anakumbuka majina aliyopewa wakati anaendeleza kazi hiyo, hatua iliyozidisha unyanyapaa hata zaidi kwa watu wanaoishi na HIV.
Kwa mfano, Regina anasimulia kilichotokea siku moja akidai kuwa hawezi kuisahau maishani mwake.
"Nilikuwa nimempata mteja mmoja ambaye nilikwenda naye kwenye vyumba tulivyokuwa tunavikodisha. Baada ya muda wake kumalizika, alinilipa na nikaanza kujitayarisha kuondoka sehemu ile, ila aliniamrisha nirejee tena. Nikamueleza kwamba atatakiwa kunilipa tena. Lakini cha kushangaza ni kuwa papo hapo alianza kunizaba makofi huku akinichania nguo zangu. Hakuna hata mtu mmoja aliyeingilia kati kunisaidia. Ilibidi nichukue nguo mmoja iliyokuwa imeanikwa kwenye kamba ili nijisitiri", Regina anasema.
Kuanzia kipindi hicho, Regina alianza kufikiria na kujutia hatari iliyokuwa inamkodolea macho, vilevile hatari ambayo alikuwa anajiwekea kutokana na kuwa kahaba anayeishi na virusi vya HIV.
Ila kila alipowaza kuiwacha ile kazi ya ukahaba, alijikuta akijiuliza maswali mengi kuhusu namna atakavyoweza kusukuma gurudumu la maisha pamoja na familia yake.
Pia anasema kuwa ukahaba unahitaji ujasiri ambao sio wa kawaida kwa hiyo wakati mwingi aliishia kunywa pombe pamoja na kuvuta bangi nyingi kuliko kawaida.
Kumaanisha kuwa kila wakati alipokuwa kazini ni lazima angekuwa mlevi.
Hilo ni moja wapo ya yale yaliyomkosesha usingizi na baada ya kujitathmini tena, ikawa moja ya kilichochea kuachana na ukahaba.
Na ili kufanikiwa kuanza safari mpya ya maisha na kuupiga teke ukahaba, Regina aliamua kufanya maamuzi ambayo hayakuwa rahisi kwake, kuondoka mji wa Mombasa na kuhamia mji mkuu nchini Kenya, Nairobi.
Na hapo ndipo alipoamua kuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na pia kutoa mafunzo maalum kwa umma na hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV.