Vita vya Afghanistan: Mfahamu Haibatullah, Kiongozi katili wa Taliban mwenye jina la kike

Chanzo cha picha, EPA
Kikundi cha Taliban kiliwachukua miaka miwili kuthibitisha kifo cha kiongozi wao, Mullah Omar, mwaka 2013.
Hata hivyo, baada ya kifo cha mrithi aliyefuata wa kiongozi huyo kilichotokana na mashambulizi ya anga ya Marekani, Mullah Akhtar Mansoor, iliwachukua siku nne tu kutangaza kifo chake kwa umma, ilikuwa mwaka 2016.
Siku hiyo hiyo Taliban ikamtangaza, Mullah Haibatullah Akhunzada, kurithi mikoba ya Mansoor akitambulika kama mwanazuoni kutokana na kubobea sana kwenye elimu ya dini.

Chanzo cha picha, AFP
"Anafahamika kwa majukumu yake ya kikatili wakati wa utawala wa Taliban akiwa jaji wa mahakama pale Kandahar. Akaendelea kuwa mtu muhimu na mpiganaji wa kijadi na akiongoza kundi pale ambapo Mullah Mansoor hayupo," alisema Akbar Agha, mmoja wa viongozi wa juu wa zamani wa Taliban.
Akhunzada Katokea wapi?
Akhunzada, anayetokea jimbo la Kandahar alishiriki katika vita dhidi ya warusi nchini Afghanistan, Katika miaka ya 1980s kabla ya kujiunga na harakati za kundi la Taliban mwaka 1994 chini ya utawala wa aliyeasisi sheria ngumu zaidi za kiislamu nchini Afghanistan.
Akhunzada ana zaidi sifa ya kuwa kiongozi wa masuala ya dini kuliko kuwa kiongozi na Kamanda wa jeshi. Amekuwa kiongozi mwandamizi wa muda mrefu kwenye mahakama za Taliban, akiwa mstari wa mbele kwenye utoaji wa hukumu dhidi ya wauaji na wezi wa mali katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Baada ya kujiunga na Taliban, Akhunzada akateuliwa na aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, Omar kuongoza mahakama ya kijeshi ya Kandahar kabla ya kujisimika na miongoni mwa viongozi wanaokubalika, kuheshimika na kupendwa ndani ya kundi hilo.
Akhunzada anayetokea kwenye jamii inayojali na kupenda sana utamaduni anafahamika kwa uwezo wake wa kufanya maamuzi magumu hasa kuhusu mashambulizi ya mabomu, wakati huo akiwa msaidizi wa karibu wa Mansoor.
Kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo ya kuongoza kundi la Taliban, kulitokana na wosia aliouacha Mansoor, ambaye alimuamini sana Akhunzada kama mtu anayeweza kutekeleza majukumu yake vyema bila uoga.
Lakini uteuzi wake, ulilenga kulipa nguvu zaidi kundi hilo, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiendesha mashambulizi nchini Afghanistan.
Maisha yake ya utotoni
Akhundzada alizaliwa mwaka 1961 katika wilaya ya Pnjwayi, huko Kandahar, akitokoea kwenye kabila la Noorzai.
Jina lake la kwanza, Hibatullah, ni jina maarufu sana nchini humo likitumiwa na mtoto wa kike. Ni kama leo usikie mwanaume akiitwa Mariamu, Beatrice, Hadija,
Regina au Mwanaisha. Lakini jina hilo kwa kiarabu linamaanisha 'zawadi' kutoka kwa Muumba. Baba yake Mullah Mohammad Akhund, alikuwa mwanazuoni pia na Imamu wa msikiti wa kijiji.
Baba yake ni masikini hakua anamiliki chochote hata ardhi zaidi ya kutegemea kupanga kwa kulipa fedha taslim ama kubadilisha na mazao. Akhundzada alisomeshwa elimu ya dini ya kiislamu na baba yake, baadae familia ikahamia Qaetta baada ya vita ya Soviet. Aliandaliwa kuwa kiongozi wa dini, akasomeshwa zaidi dini, akaishi kwenye misingi ya dini, na ameendelea kuwa mtu wa dini mwenye maamuzi magumu.
Mwandishi wa Vitabu anayeamini Taliban ni kundi pekee linalostahili kila kitu duniani Inawezekana kila kiongozi wa kundi akawa na imani kwamba, kundi lake ni bora zaidi ya kundi li gine, lakini anavyoamini Mullah Akhunzada ni zaidi ya hivyo.
Anaamini Kundi la Taliban, linastahili kuongoza Afghanistan, Taliban linastahili kusikilizwa Afghanstan, Taliban linastahili kuheshimiwa Afghanistan na nje ya Afghanistan na Taliban linastahili kupendwa na vizazi vilivyopo na vijavyo.
Amekua akiandika vitabu mbalimbali kuonyesha hilo, akitumia mgongo wa Imani yake ya dini kupenyeza anayoyaamini.
Ameandika vitabu kadhaa kikiwemo maarufu cha mwaka 2017 alichokiita 'Mujahedino ta de Amir ul-Mumenin Larshowene' akimaanisha Maelekezo kwa mujahidina kutoka kwa kamanda wa Imani.
Je ni Kiongozi mtata kama watangulizi wake?

Akhunzada, haonekana kufuata nyayo za watangulizi wake hasa Mullar Mansoor na Mullah Omar, walioamini kushugulikia kila jambo kwa kupitia mtutu wa bunduki.
Kwa sababu ya misimamo yake, awali alionekana kama mtu mkatili kimisimamo,ambaye isingekuwa rahisi kukaa chini na kuzungumza nae jambo lolote lililo tofauti na mitazamo ya Taliban.
Hali imekuwa tofauti, pengine ubobezi wake kwenye masuala ya dini na Imani yake inampeleka kuamini katika matumizi ya njia nyingine zaidi kwenye kushughulikia mizozo mbalimbali.
Moja ya njia muhimu anayoiamini Akhunzada katika kushughulikia mizozo na iliyoanza kuonekana katika utawala wae ni 'utatuzi wa kisiasa' kwa maana ya kukaa chini na kuzungumza.
Mwezi Julai, 2021 kundi hilo lilikaa chini na viongozi wa serikali ya Afghanistan, huko Doha ikiwa ishara muhimu kwa mazungumzo ya Amani yaliyokwama kwa muda mrefu.
Akhunzada ana uwezo wa Kumaliza mapigano yaliyodumu karne na karne?
Baada ya Marekani kuondoa vikosi vyake nchini Afghanistan, kundi la Taliban limeendelea kutawala kwa kufanya mashambulizi dhidi ya majeshi ya Serikali na kutwaa maeneo mengi ya nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi hilo chini ya Akhunzada limeshika udhibiti wa karibu nusu ya wilaya 400 za nchi hiyo, na maeneo kadhaa ya mipaka ya nchi hiyo, wakiendelea na mashambulizi kutaka kutwaa makao makuu ya majimbo muhimu ya nchi hiyo.
Swali linasalia, kwa namna gani kiongozi huyu wa kundi la Taliban na ataweza kushawishi kundi lake na hasa viongozi waandamizi kukubaliana na matakwa ya jumuiya za kimataifa ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 40?













