Fahamu wachezaji watano waliohama klabu zao na kuwaacha watu vinywa wazi

Messi

La liga imehitimisha uchumba uliodumu kwa miaka 21 wa Leonel Messi na Barcelona. Uchumba ulioleta mafanikio lukuki kwa pande zote mbili, yakiwemo makombe zaidi ya 30 kwa Klabu yake hiyo pekee aliyoitumika katika maisha yake yote ya soka mpaka sasa na tuzo binafsi zilizojaza kabati lake.

Pengine ni moja ya wachezaji wachache wakubwa duniani waliopata mafanikio zaidi kwenye soka, ukiachilia mbali makombe 10 ya Laliga, 7 ya Copa del Rey na 4 ya ligi ya mabingwa, amefanikiwa kutwaa tuzo binafsi zikiwemo sita za mwanasoka bora wa dunia 'Ballon d'Or na sita za mfungaji bora wa Ulaya.

Messi amefunga magoli yaliyoweka rekodi La liga, akiifungia Barcelona magoli 474. Kwa ujumla katika maisha yake yote ya soka amefunga ujumla wa mabao 750 kwa nchi yake na klabu yake hiyo.

messi

Chanzo cha picha, EPA

Pamoja na Barcelona na yeye mwenyewe kutaka kubaki kuichezea klabu hiyo ya Hispania, Kanuni za fedha zinazoongoza Ligi ya Hispania 'La liga' zinamtoa Messi Barcelona. Ili Messi asalie Barcelona wanapaswa kupunguza mishahara ya wachezaji inayofikia Pauni 172 milioni kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa mno.

Ingawa haijawa wazi anaelekea wapi, Klabu ya PSG ya Ufaransa imeanza kumfuatilia. Kuondoka kwake Barcelona kumewashangaza wengi, na hakuna aliyetarajia kwa sababu ya uaminifu wake kwa klabu hiyo, uwezo wake, kupendwa kwakwe, mapenzi yake na rekodi zake. Pamoja na mshituko huo kwa Messi, anayetajwa na wengi kama mchezaji bora wa soka wa muda wote, kuna wachezaji ambao waliwahi pia kuleta mshtuko kwa mashabiki wa soka wa klabu zao na duniani kwa ujumla.

mm

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mfano Ronaldinho Gaucho aliyetoka Milan kwenda Flamingo mwaka 2011, Andrea Pirlo (Inter kwenda AC Milan, 2001) Gigi Buffon (Parma -Juventus,2001), Ashley Cole (Arsenal - Chelsea, 2006), Diego Maradona (Barcelona-Napoli, 1984) Robin Van Persie (Arsenal - Man Utd, 2012) au Paul Pogba aliyevunja rekodi ya uhamisho mwaka 2016 akitoka Juventus kwenda Manchester United.

Ukiacha hao, uhamisho wa wachezaji wafuatao ulikuwa miongoni mwa ulioshitua zaidi dunia na kubakisha watu midomo wazi.

  • Roberto Baggio Fiorentina - Juventus, 1990

" Kama huwezi kuwashinda ungana nao" ni usemi maarufu ambao Roberto Baggio aliutumia wakati alipohama kutoka Fiorentina kwenda Juventus baada ya kushindwa kuisaidia timu yake ya Fiorentina kuifunga Juventus katika fainali ya kombe la UEFA mwaka 1990.

Roberto Berggio

Uhasama wa kishabiki baina ya timu hizi mbili ni wa hali ya juu kabisa, na hata ada ya uhamisho iliyoweka rekodi ya dunia ya £8m haikuwatuliza mashabiki wa Fiorentina wasifanye vurugu na kuandamana kupinga uhamisho wa gwiji huyo.

Walitumia siku kadhaa kufanya vurugu kuonyesha hasira zao kwa uongozi, kukubali kumuuza Baggio kwenda Juventus.

Lakini Baggio akatua kwa vibibi vizee hao wa Turin na kwenda kushinda Scudetto na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia ya Ballon d'Or.

Pamoja na hilo lakini hakuacha kuonyesha mapenzi yake ya wazi kwa Fiorentina, akikataa kupiga penati katika mechi ya kwanza dhidi ya Fiorentina katika uwanja wa Artemio Franchi. Na akavaa skafu ya timu yake hiyo ya zamani, baada ya kupumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na mtu mwingine.

Lakini kocha wa Juventus wakati huo, Luigi Maifredi alisema, ulikua uamuzi wa jumla wa Baggio asipige penati kwa sababu mlinda mlango wa Fiorentina wakati huo, Mareggini alimjua vizuri Baggio kwenye penati kwa sababu kucheza naye muda mrefu Fiorentina.

Mechi hiyo iliisha kwa Juve kulala 1-0 na kushindwa kufuzu michuano ya Ulaya, huku Fiorentina ikiponea chupuchupu kushuka daraja.

  • David Beckham (Real Madrid - LA Galaxy, 2007)
david

Ligi ya Marekani (MLS) inazidi kupata umaarufu kwa sasa, lakini umaarufu wake hakika umejengwa na uhamisho wa nahodha wa zamani wa England na Manchester United, David Beckham.

Ingawa inaonekana ni ligi inayokimbiliwa na wachezaji wa Ulaya wanaomalizia muda wao kwenye soka, lakini Beckham alipotangazwa kujiunga na LA Galaxy mwaka 2007 - ilikuwa mshangao wa dunia, na kuipa sura ningine ligi hiyo.

Hakuna aliyetarajia kama Beckham angekwenda huko. Kwa sababu hiyo Kocha wa Real Madrid wakati huo, Fabio Capello awali alisema Muingereza huyo asingekanyaga tena na kuiwakilisha los Blancos, kabla ya kubadili kauli na kumruhusu Beckham kurejea wiki chache baadae.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United akaenda kuichezea Galaxy jumla ya michezo 113 katika miaka mitano aliyokuwepo Marekani. 

  • Neymar (Barcelona - PSG, 2017)
ney

Chanzo cha picha, Getty Images

Naymar ni miongoni mwa vipaji vya maana na vyenye ladha kutoka Brazil. Kuhama kwake kutoka Barcelona kwenda PSG mwaka 2017, kulivunja rekodi ya uhamisho ya dunia iliyowekwa awali na Paul Pogba. Ada yake ilikuwa £109m.

Barcelona iliweka kipengele chenye fedha kubwa kwa klabu itakayomtaka, na hakuna aliyedhani kwamba kiasi hicho che fedha kwa wakati huo kingekuwa rahisi

Neyma

Chanzo cha picha, Getty Images

kupatikana na kutolewa na klabu yoyote Ulaya. PSG ikajitokeza na kuushangaza ulimwengu, Neymar akahamia Ufaransa.

Ingawa inaonekana kama alihama kwa kutafuta fursa ya kushinda tuzo ya mwanasoka bora wa dunia ya Ballon d'Or, kutokana na kufunikwa na kivuli cha Lionel Messi pale Barcelona, Neymar amekuwa nyota wa kutegemewa pale Parcdes Princes akisaidiana na Mfaransa Kylian Mbappe.

Ingawa hajaweza kushinda tuzo hiyo, lakini klabu yake inamuelekeo mzuri, na mshangao wa watu hautakuwa mkubwa kama Messi ataungana nae pale PSG, baada ya kuachana na Barcelona, lakini litabaki swali kama Messi atatua PSG Je Neymar atakimbia tena kivuli cha Muargentina huyo?

  • Sol Campbell (Tottenham - Arsenal, 2001)
arsenal

Chanzo cha picha, Getty Images

Arsenal na Tottenham ni mahasimu wa kutupwa nchini Uingereza , timu zinazotoka katika jiji la London.

Sio rahisi mchezaji kutoka Arsenal kwenda Spurs ama Spurs kwenda Arsenal, kwa sababu ya uhasama uliopo.

Emmanuel Adebayor alitoka Arsenal, akaenda Manchester City kabla ya kutua Spurs, ingawa hakuhamia moja kwa moja, alipitia City, bado alisakamwa sana na kuzomewa na mashabiki wa Arsenal, hilo tu linakuonyesha kwamba uhasama baina ya timu hizi sio wa kawaida.

Kwa Campbell, baada ya mkataba wake kumaliza Tottenham, akahamia Arsenal, akiwa mchezaji wa kwanza kutoka White Hart Lane kwenda Highbury tangu Pat Jennings.

Hakuna aliyeamini kirahisi kwamba Campbell ameenda Arsenal kutoka Spurs tena bure, kutokana na uhasama baina ya vilabu hivyo, lakini akaenda kuwa mchezaji mkubwa wa timu hiyo na kusaidia kutwaa makombe na kuwa sehemu ya kikosi kilichocheza michezo yote ya ligi bila kufungwa na kutwaa ubingwa wa ligi kuu katika msimu wa 2003/2004.

  • Luis Figo (Barcelona - Real Madrid, 2000)
kandanda

Chanzo cha picha, Getty Images

"Kama mchezaji ndani ya Barcelona, kamwe hakuwahi kuficha chochote," maneno ya mmoja wa wachezaji wenzake wa zamani na Figo, baada ya uhamisho wake wa utata ulioshangaza dunia kutoka Barcelona kwenda Real Madrid. Uhamisho huu wa mwaka 2000 uligharimu £36.2m.

Sasa kasheshe ikawa, mreno huyo aliporudi kwenye dimba la Camp Nou mwezi Oktoba mwaka 2001 kucheza dhidi ya timu yake ya zamani Barceloba- Kila alipogusa mpira alitukanwa, kuzomewa na kurushiwa kila aina ya uchafu kuanzia maganda ya machungwa, chupa za maji na soda, vipisi vya sigara na viberiti.

Mwaka mmoja baadae, kwenye mechi kama hiyo alirushiwa kichwa cha nguruwe, yote ni kuonyesha chuki ya mashabiki dhidi yake. Hawakutarajia kama angehama na angehama kirahisi kwenda kwa mahasimu wao, Real Madrid.

Lakini kuwasili kwa Figo pale Real Madrid, kukawa mwanzo wa awamu mpya ya kizazi cha nyota wakali 'Galacticos' pale Madrid; Zinedine Zidane, Ronaldo na David Beckham walisajiliwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyofuata, na kufanya timu iliyosheheni vipaji vikubwa vya soka wakati huo.