Waridi wa BBC:Sonona ilivyopelekea nile kinyesi changu

Esther Wanjiku

Chanzo cha picha, Esther Wanjiku

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Esther Wanjiku Kabeni ni mjane tangu mwaka 2016 , mume wake alifariki katika kile anachokitaja kuwa kifo cha ghafla. Mume wake alikuwa ni afisa wa ulinzi wa mipaka katika jeshi la Kenya (KDF).

Esther anasema kifo cha mume wake kilibadilisha maisha yake na ilifikia hatua asijue iwapo anarudi nyuma au anakwenda mbele kwa miaka kadhaa baada ya tukio hilo .

Baada ya kifo cha mume wake alishuhudia mabadiliko makubwa kutoka kwa shemeji zake na jamaa wengine kutoka upande wa marehemu mumewe.

Walikuwa na nia ya kumpokonya mali zote alizopata na marehemu mumewe.

Kwa mujibu wa mwanamke huyo, ndugu za marehemu mume wake walidai kuwa kila mali aliyokuwa nayo ilikuwa ni ya marehemu mume wake na hivyo haimuhusu.

" Tulipokwenda kwenye chumba cha kuhifadhi maiti ili kuthibitisha kuwa kweli mume wangu alikuwa ameaga dunia , nikiwa pale mmoja wa ndugu za mume wangu waliwapigia wazazi wangu simu na kuwaeleza kuwa walikuwa wanahitaji funguo za nyumba yetu , ili wachukue mali zake . Mimi nilijibu wazazi wangu kuwa wakati huo ulikuwa ni wa maombolezo na wala sio wa kugawa mali na hapo ndipo ulipokuwa uhasama na mashemeji zangu " anakumbuka Esther

Mwanamke huyu anasema kuwa kilichofuata baada ya siku nyingi za kilio , kero na uchungu usioeleweka alihangaishwa asikumbuke hata jina lake .

Ugonjwa wa mume wake ulivyoanza

Esther Wanjiku

Chanzo cha picha, Esther Wanjiku

Esther anasema kuwa mume wake kama afisa wa jeshi alikuwa anatumwa kwenye oparesheni za kijeshi huko Somalia.

Na wakati mwingi mume wake alikuwa anarejea nyumbani baada ya miezi kadhaa ya kuwa nchini Somalia ambapo baadhi ya maafisa wa jeshi la nchi ya Kenya walitumwa kama walinda usalama hasa maeneo ya mpaka wa Somalia na Kenya .

" Kuna wakati mmoja mwaka 2015 mume wangu alirudi nyumbani baada ya kuwa Somalia kwa miezi kadhaa.

Nakumbuka nilikuwa naandaa mapishi jikoni , na niliporejea sebuleni alipokuwa ameketi, nilimkuta ameanguka sakafuni . Nilimuuliza ni nini kilichofanyika na hapo ndipo alisema kuwa hakuwa na uwezo wa kuhisi sehemu ya chini ya mwili wake .Cha mno alikuwa amaeenda haja ndogo na kubwa pale pale . Nilichofanya ni kumuosha na kumrejesha kwenye kochi" anakumbuka Esther

Mwanadada huyu anasema kuwa pandashuka za maradhi ya mume wake zilianzia hapo, Esther aliwapigia simu baadhi ya marafiki na wandani wa mumewe ambao walikuwa kwenye jeshi akiitisha msaada wao . Alishauriwa kumsafirisha hadi hospitali ya wanajeshi mjini Nairobi ambako alilazwa .

Wiki ya kwanza mume wake Esther alikuwa kwenye wadi ya kawaida huku akiwa kwenye uangalizi wa wahudumu wa afya , Wiki ya pili afya ya mume wake iliendelea kudhoofika na alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi baada ya figo zake kuonekana kuwa na shida .Wiki ya tatu alitolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi yaani ICU na kurejeshwa wadi ya kawaida , wiki ya nne alikuwa ameanza kuimarika na kuonekana kuwa na unafuu . Ghafla wiki ya tano mume wake aliporejeshwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi aliaga dunia .

"Desemba mwaka wa 2015 nilikuwa nahangaika na hali ya mume wangu pekee yangu , Mume wangu alikuwa kifungua mimba nyumbani kwao , ndugu zake hawakuwa wanashughulika mno naye wakati amelazwa hospitalini , kiufupi hawakufika hata kwenye wadi kumjulia hali kaka yao , mama yake mzazi alifika kwa siku tatu pekee yake. Niliachiwa mzigo wa kumuangalia mgonjwa wangu, "anakumbuka Esther.

Mwanadada huyu anasema kuwa baada ya habari kutoka kuwa mume wake alikuwa ameaga dunia , kukurukakara kati yake na ndugu wa mume wake zilianzia pale pale hospitalini. Walifika wakishinikiza kuwa Esther awape funguo za nyumba yao , wakisisitiza kuwa walihitaji kutoa mali zao .

Bi Esther anasema kuwa majibizano yalijiri palepale lakini alikaa na hakuwapa funguo za nyumba yao .

Na kuanzia hapo alihisi kuwa huenda kukawa na shida , alifululiza nyumbani kwa haraka kuokoa kile ambacho walikuwa wamekichuma na mume wake.

Bi Esther anasema kuwa shemeji zake walikuwa wanasisitiza kuwa wapewe vitu mbalimbali vilivyokuwa ndani ya nyumba yao , huku wakidai kuwa ni mali ya mtoto wao .Mwanadada huyu anasema kuwa ni hapo ambapo aliamua kuhamisha vyombo vya nyumba hadi sehemu nyingine na pia kuripoti kisa hicho kwenye kituo cha polisi ili kupata ulinzi .

"Wakati tunatayarisha kumpumzisha mume wangu nilikuwa nimehamisha vitu vyote vya nyumbani na kuvificha sehemu nyingine , ni ajabu kuwa mipango yote ilifanywa wakati kwangu hakuna viti wala meza . Ni majirani zangu walionisaidia kupika na pia viti vilitoka kanisani "anakumbuka Esther

Esther Wanjiku

Chanzo cha picha, Esther Wanjiku

Siku tano baada ya mume wake kufariki Bi. Esther hakutangamana na shemeji wake kwa kuwa tayari kulikuwa na uhasama ,kikundi kimoja kilikuwa na matanga sehemu moja naye Bi Esther na kikundi chake walikuwa na yao sehemu nyingine tofauti .Mwanadada huyu anakumbuka kipindi kizito cha kupanga mazishi ya mume wake akiwa ametengwa kama mke, asijue la kufanya.

"Tangu kifo cha mume wangu nilianza kudhoofika kiafya kwa kiasi kuwa ilibidi nifike hospitalini kwa matibabu , lakini hakuna shemeji yangu hata mmoja aliyenishughulikia , kipindi cha maziko kilichukua wiki mbili hivi ila hakuna mtu alinijali iwapo niko salama au vipi , kwa hiyo nilijipa nguvu .

Mwezi Januari mwaka 2016 , ilikuwa ndio siku walisafiri hadi nyumbani kijijini alikozaliwa mume wake , kulingana na mwanadada huyu anasema kuwa aliona huzuni kwa kuwa karamu kubwa iliyoandamana na vyakula mbalimbali ilikuweko , kinyume na kasi ya kumshugulikia mume wake wakati akiwa hospitalini akipigania maisha yake.

Cha kushangaza mno ni kuwa wakati wa sherehe au ibada ya mazishi Esther anasema kuwa baadhi ndugu za mume wake , waliopewa fursa ya kuzungumza katika mazishi hayo , walitoa maneno yakumkosea heshima wala utu wa kuwa ni mjane anayeomboleza mume , matamshi yaliomdhalilisha na kusakama nguvu aliokuwa nayo .

"Wakati wa hotuba katika mazishi ilielekezwa kuwa mimi bado nilikuwa mrembo , na kwa hiyo baada ya mazishi nilikuwa huru kuolewa nikitaka , niliyabeba matamshi hayo kama ya kuniambia kwaheri kutoka maisha ya jamii ya marehemu mume wangu "anakumbuka Esther

Esther alirejea mjini Nairobi , na kuanza maisha upya , kwa muda aliishi na dada yake bila shaka anasema kuwa maisha ya kuishi na watu sio rahisi na changamoto zilipoibuka aliamua kujikusanya na kurejea katika nyumba yake aliokuwa anaishi na marehemu mume wake .

Kipindi cha Sonona

Esther Wanjiku

Chanzo cha picha, Esther Wanjiku

Esther alirudisha vyombo vya nyumba alivyokuwa ameficha , kuanza kuishi katika nyumba yao na marehemu mume wake - haikuwa rahisi kwake .

Kipindi hicho cha februari mwaka wa 2016 alishikwa na sonona mbaya mno iliyompelekea wakati mwingi kujisemesha mwenyewe , Esther anakiri kuwa na tabia na mienendo ya kutisha kwa mfano alikuwa anakula kinyesi chake mwenyewe.

Ilibidi mama yake mzazi atoke kijijini hadi mjini ili kumfariji na kukaa karibu na mwanae kwani msongo wa mawazo ulimpiga mno

"Nilipelekwa hospitalini na baada ya kufanyiwa vipimo niligundulika nilikuwa na sonona iliyokuwa ya hali ya juu mno, nilipewa madawa yaliokuwa sugu mno kukabiliana na hali yangu ya kisaikolojia , kiasi kuwa nilikuwa nalala kila wakati , kwa kipindi cha mwezi mmoja wakati mwingi kazi yangu kuu ilikuwa kulala lala "Esther anasema.

Esther anasema kuwa baada ya kulala kwa mwezi huo mmoja uchungu wa kufiwa na mume wake ulikuwa umepungua japo alikuwa anamuwaza kila siku .

Mwezi Machi, Esther anasema kuwa mahusiano yake yalianza kuporomoka mmoja baada mwingine , kwa mfano wengi wa watu wa jamii yake walikuwa hawako tena , marafiki nao hawakuwa wanapokea simu zake, wala kumjulia hali . Asilimia 90 ya watu aliokuwa anawafahamu kama watu waliokaribu naye walitokomea asijue wakumgeukia. Shemeji nao walimpa kisogo huku safari ya kung'ang'ania urithi wa mume wake kutoka idara ya Jeshi hasa fedha na malimbikizi ya miaka aliyohudumu ilianza . Alianza safari hii bila mtu wa kumpa ushauri au mkono wa kheri .

"Kinachoudhi mno ni kuwa cheti cha kufariki kwa mume wangu kilikuwa mikononi mwa afisa mmoja wa jeshi , ambaye alitwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa malipo , marupurupu na malimbikizo ya mume wangu yanatolewa , lakini sijui ni vipi alishirikiana na ndugu za upande wa marehemu mume wangu na wao ndio walipewa kile cheti chake . Kuanzia hapo ikawa wanauwezo wa kuchukua mali zake hasa fedha kwenye benki , nilikata tamaa na hapo ndipo niliamua kuanza maisha upya kwa kujitafutia riziki yangu badala ya kung'ang'ana na watu, "anakumbuka Esther.

Kuanzisha Wakfu wa wajane

Esther Wanjiku

Chanzo cha picha, Esther Wanjiku

Safari ya kuanzisha wakfu wa wajane kwa jina Royal widow nchini Kenya ilitokana na safari ya mateso na pandashuka zilizomfuata Esther baada ya mume wake kufariki -Esther anasema kuwa wakati mmoja alikosa hadi karo ya kumlipia mwanae, wakati mwingine alikosa njia ya kumpa mtoto wake chakula , wakati mwingine pia alikuwa hana uwezo wa kulipa kodi ya nyumba lakini kipindi hicho ndicho kilimpa ukakamavu na bidii ya kuwa na maisha mapya

Anasema kuwa hali ya kuhangakia maisha kama mjane huku akiwa na watoto wa kuwalea peke yake haikuwa rahisi.

Esther alianza kuwaunganisha kina mama wa miaka na tabaka mbalimbali ambao ni wajane , anasema kuwa ilikuwa rahisi kuwa karibu na wajane wenzake kwani walikuwa wanaelewana kifikra na kihisia .

Mwanadada huyu anasema kuwa ni ajabu sana kwamba waliomsaidia mno wakati wa dhiki walikuwa ni wajane wenzake.

Hata hivyo Esther anasema kuwa , idara ya jeshi ilianza kumpa malimbikizi na malipo ya mume wake baada ya muda , fedha ambazo zilimsaidia sana wakati huo .

Ushauri anaotoa mama huyu mjane ni kuwa jamii iache kuwatenga wajane , kwani wanapitia kero ya kuwapoteza waume wao juu ya hayo wanaanza kuonekana kama mzigo katika jamii .

Wakfu wa Royal Widows umewafikia wajane wengine hasa katika mitaa ya mabanda nchini Kenya , ambapo wanawake hupata jukwaa la kupeana nguvu na kutafuta njia mbadala za kupata riziki.

Mwanasaikolojia Bupe Mwabenga kutoka Tanzania anasema ni jambo linalowezekana kwa mtu anayepitia msonono kufanya mambo ya kushangaza kama alivyofanya Esther .Bupe anasema kwa mtu mwenye tatizo la msonono fikra zake huwa hazimpi mtazamo kama wa mtu anayejua kibaya na kizuri na machoni mwake lolote analofanya ni sawa . Ameongeza kwamba hatua hiyo ndiyo husababisha hata baadhi ya watu wenye msonono kujiua .