Mzozo wa Israel na Palestina: Kwa nini Israeli na Palestina wote wanasherehekea ushindi?

Pande zote mbili za mapigano na wafuasi wao zasherehekea zikidai ushindi kufuatia kusitishwa kwa mapigano. Kundi la Shia la Hezbollah huko Lebanon limesifu upande wa Palestina kwa "makabiliano ya kishujaa".

"Upinzani wa Palestina... ulianzisha sheria mpya ammbazo zitakuwa mwongozo katika kufikiwa kwa ushindi mkubwa zaidi," kundi la Hezbollah limesema.

Limeongeza kuwa "ushindi... utakuwa na mkakati muhimu sana, athari za kisiasa na kitamaduni katika hatma ya migogoro eneo hilo."

Hezbollah, ambalo limejihami na linalofadhiliwa na mahasimu wa Israel la Iran, ndio kikosi chenye nguvu kubwa huko Lebanon pamoja na jeshi la Lebanon na kwa pamoja na washirika wake wakisiasa, ni kikosi chenye ushawishi mkubwa serikalini.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniya ametangaza ushindi pia na kusema mapambano haya amedhihirisha kuwa "mazungumzo hayawezi kuwa suluhu."

Haniya ameahidi, baada ya ushindi huo wa kijeshi na kisiasa, kundi hilo pamoja na wanaharakati wengine watajitoa kuijenga upya tena Gaza.

Netanyahu - Tumefanya kazi bora na mambo mapya

Bwana Netanyahu amekuwa akielezea lengo la Israel katika kuanzisha operesheni yake huko Gaza wiki jana. Amesema "lilikuwa pigo kubwa dhidi ya makundi ya kigaidi na imefanikiwa kurejesha utulivu''.

"Sio kila kitu kilichotokea kinajulikana na umma hadi kufikia sasa, sio Hamas, lakini kuna mafanikio makubwa ambayo yatawekwa wazi kadiri muda unavyokwenda," amesema, kulingana na gazeti la Jerusalem Post.

"Naweza kusema kwamba tumefanya yaliyobora na mapya - kama kulikuwa na ulazima wa kufanya uvamizi wa ardhini, tungefanya hivyo lakini nilifikiria kwamba tunaweza kufikia lengo letu kwa njia salama zaidi."

Pia, Israeli imesema kuwa sasa imebadilisha mkondo na kundi la Hamas, na itafanya kundi hilo kuwa makini zaidi siku za usoni kuhusu kuvamia Israel.

Bwana Netanyahau ameelezea kampeni ya mashambulizi ya anga kama "mafanikio ya kipekee", kulingana na gazeti la Times la Israel.

Imesema kwamba imeharibu mtandao wa kwenye handaki chini ya ardhi wa Hamas na kuubadilisha kuwa "mtego wa kifo", na pia imekabiliana vikali na uwezo wa kundi hilo wa kurusha makombora kuelekea miji ya Israel na maeneo yake.

Bwana Netanyahu amesema kuwa wanamgambo 200 wakiwemo maafisa waandamizi 25waliuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa na Israeli, na kuongeza kuwa: "Na wale ambao hawakufariki dunia wajue kwamba tunaweza kuwafikia - ama iwe juu au chini ya ardhi."

Bwana Netanyahu pia amesisitiza kuwa jeshi la Israeli lilijitahidi kwa kila namna kuzuia raia kujeruhiwa, na kuchukua hatua ambazo hakuna nchi nyingine yoyote duniani imewahi kuchukua.

Wizara ya afya ya Palestina huko Gaza imesema watoto 66 na wanawake 39 ni miongoni mwa raia 243 waliouawa katika mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Israeli.

Na nchini Israel watu 12, wakiwemo watoto 2 waliuawa katika mashambulizi ya roketi yaliyotekelezwa na Palestina, huduma yake ya afya imesema.

Mapambano kusitishwa

Mashambulizi baina ya Israel na Palestina yamesimamishwa leo baada ya siku 11 za ghasia kati ya pande hizo mbili.

Israeli imeukubali mpango wa Misri wa kusitisha mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2014, na imekubali bila masharti yoyote.

Misri sasa inatarajiwa kutuma wajumbe nchini Israeli na Ukanda wa Gaza katika siku chache zijazo kwa lengo la kuumaliza kabisa mgogoro huu.

Maafisa wa Hamas wanasema huenda makubaliano ya sasa yakawa na nguvu iwapo tu Israel itaacha kutumia nguvu katika masuala ambayo yanahitaji diplomasia, huku Israel ikisema Hamas inahitaji kushauriana vyema na mamlaka ya Palestina ili kunusuru machafuko mengine.

Nchi kadhaa zimehusika katika majadiliano hayo ya muda mrefu ikiwemo Misri, ambayo ni mshirika wa karibu wa pande zote mbili kwa sasa.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema mazungumzo ya siku 11 yamesaidia kufikia mafanikio hayo.

Baada ya habari hiyo kutangazwa, kulikuwa na mashambulio zaidi ya anga ya Israeli huko Gaza na makombora yalirushwa kuelekea Israeli. Wakati huo huo, uwanja mkuu wa ndege wa nchi hiyo, Ben Gurion, ulifungwa kwa muda mfupi kutokana na hofu ya usalama.

Inaarifiwa kuwa muda mfupi baada ya kutangazwa kusitishwa kwa mapigano, mamia ya watu wameanza kurejea katika makazi yao, licha ya miundombinu na nyumba zao kuharibiwa vibaya.

Hamas imeadhibiwa, na Wapalestina wa Gaza wameteseka sana. Wachambuzi wa siasa za Mashariki ya kati wanasema ili kuepuka mgogoro mwingine, ni vyema mahitaji ya pande hizi mbili yakafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Rais Biden alisema nini ?

Akiongea katika Ikulu ya White House, Rais Joe Biden alisema alimpongeza Bw Netanyahu kupitia simu baada ya kutangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

"Marekani inaunga mkono kikamilifu haki ya Israeli ya kujilinda dhidi ya mashambulio ya roketi ya kiholela kutoka Hamas na vikundi vingine vya kigaidi vya Gaza ambavyo vimeua watu wasio na hatia nchini Israeli," Bwana Biden alisema.

Alisema waziri mkuu wa Israeli alitambua kama yeye mfumo wa ulinzi unaojulikana kama Iron Dome, "ambao mataifa yetu yalitengeneza pamoja na ambao umeokoa maisha ya raia wa Israeli - wote Waarabu na Wayahudi".

Bwana Biden pia alimsifu Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kwa kufanikisha kusitisha mapigano, kabla hayajasababisha maafa ya watu wengi.

"Natuma pole zangu za dhati kwa familia zote, Israeli na Palestina, ambao wamepoteza wapendwa wao na kuwatakia afueni ya haraka kabisa waliojeruhiwa," alisema.

Rais alisema Marekani "inaendelea kujitolea kufanya kazi na Umoja wa Mataifa" katika kutoa msaada wa kibinadamu kwa Gaza na katika juhudi za ujenzi wa eneo hilo. Aliongeza kuwa hii itafanywa "kwa ushirikiano kamili na Mamlaka ya Palestina, sio Hamas".

Rais Sisi alisema alikuwa amepokea simu ya Bwana Biden na "furaha kabisa", na kuongeza kuwa "walibadilishana maono kuhusu jinsi ya kutafuta suluhisho ya kudumu kwa mzozo wa Gaza.

Nini kilipeleka mapigano kusistishwa?

Pande zote mbili zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jamii ya kimataifa kumaliza uhasama.

Siku ya Jumatano, Rais wa Marekani Joe Biden alimwambia Bw Netanyahu "kwamba alitarajia kushuka kwa kiwango kikubwa kwa mapigano'.

Misri, Qatar na UN vimekuwa na jukumu la kuongoza mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israeli na Hamas, ambayo inatawala Gaza.

Rais Sisi aliamuru makundi ya jumbe mbili za usalama kwenda Israeli na maeneo yaliyokaliwa ya Palestina kufanya kazi ili kufanikisha usitishaji wa vita, kulingana na Televisheni ya serikali ya Misri.