Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, China ingelipishwa fidia kiasi gani kwa mlipuko wa roketi yake kwenye makazi ya watu?
Dunia ilikuwa imekaa kwa tahadhari mwishoni mwa juma lilopita wakati mapande makubwa ya roketi ya Kichina yalipokuwa yakianguka kwa kasi katika uso wa dunia yakitokea anga za mbali.
Haikujulikana mabaki hayo yangeangukia wapi na upi ungekuwa ukubwa wa madhara yake. Ilikuwa ni suala la kusubiri na kuona kitakachotokea.
Katika hali ambayo ilishusha pumzi za malaka za China na watu mbali mbali waliokuwa wakifuatilia tukio hilo, shirika la anga za mbali la nchi hiyo likatangaza jana kuwa mabaki hayo yameangukia katika Bahari ya Hindi, karibu na visiwa vya Maldives.
Je, ingekuwaje kama roketi ingeangukia kwenye makazi ya watu?
Hili ni suali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza, je nini kingetokea kama mabaki hayo yasingeliangukia kwenye bahari. Nini kingetokea katika ardhi na je China ingelipa fidia?
Bila shaka kama mabaki ya roketi hiyo yangelianguka katika eneo la makaazi ya watu kungelikuwa na athari kubwa kwa uhai wa watu na mali zao.
Ifahamike kuwa si kosa katika sheria za kimataifa kwa vyombo vya safari za anga za juu kuangusha uchafu ama mabaki duniani, lakini hilo ni suala la kimaadili ambalo nchi nyingi wamekuwa wakilitilia mkazo ili kufanya dunia kuwa eneo salama lisiloathiriwa na shughuli za anga za mbali.
Kuhusu fidia na namna ya kushughulikia ajali kama hiyo, kuna mikataba miwili ya kimataifa ambayo ilipitishwa mwaka 1967 na mwaka 1972 ambayo inatoa muongozo wa nini cha kufanyika.
Mkataba wa mwaka 1972 ni juu ya dhima za nchi ambazo zinafanya shughuli katika anga za mbali pale endapo kuna jambo lolote litatokea kupitia vifaa vyake.
Nchi mbalimbali za Ulaya, Malekani na hata China zimetia saini mkataba huo. Na kukubali dhima haimaanishi kuwa nchi imevunja sheria, bali inatambua wajibu wake wa kimaadili kwa kile kilichotokea na ipo tayari kushughulika janga ama ajali hiyo.
Je, kuna nchi ambayo imewahi kulipishwa?
Takriban miaka 43 iliyopita, Canada ilitumia vifungu vua mkataba huo kuiwajibisha nchi ya Umoja wa Kisovieti (Urusi ya sasa).
Mwaka 1978, satelaiti ya Usovieti Kosmos 954 ilipata hitilafu ikiwa katika anga za juu na mabaki yake kuangukia katika eneo la kaskazini magharibi ya Canada, na kusambaza taka za sumu ardhini.
Awali Usovieti ilijaribu kukanusha kuwa satelaiti hiyo haikuwa yao lakini baada ya majadiliano wakakubali kulipa Dola milioni 6 za Canada. Hakuna ushahidi kama kiasi hicho kililipwa chote.
Je, vyombo vya anga za juu vya Marekani vimeshawahi kuanguka?
Mwezi Machi mwaka huu, sehemu ya roketi ya Marekani ya mradi wa Space X ilianguka karibu na makaazi ya watu.
Sehemu ya mabaki hayo yalianguka katika shamba huko Washington baada ya roketi hiyo kushindwa kurejea duniani kwa utaratibu sahihi.
Mabaki makubwa zaidi ya chombo cha juu cha Marekani yalianguka mwaka 1979. Nchi nyingi duniani kuanzia Ulaya mpaka Asia zilikuwa katika hali ya hofu juu ya madhara yake endapo mabaki yangeangukia katika maeneo yao.
Hatimaye tani 77 zilianguka baharini karibu na Australia. Mabaki ya chombo hicho yalitapakaa katika eneo la kilomita takribani 7,400 baharini, hali iliyomlazimu Rais wa Marekani wa wakati huo Jimmy Carter aliomba radhi.