Kifo cha Magufuli: Hayati John Magufuli azikwa Chato

Ni safari ya mwisho ya Hayati Rais John Pombe Magufuli , amelazwa katika nyumba yake ya milele, ni huzuni na simanzi tele kwa watanzania.

Amezikwa kwa taratibu zote za kijeshi ambazo anapaswa kupatiwa Amiri Jeshi Mkuu.

Mizinga 21 imepigwa ikiashiria heshima kubwa kwa kiongozi huyu.

Hayati Magufuli amezikwa katika makaburi ya familia mjini chato , mkoani geita.

Watu wa karibu na familia pamoja na viongozi ndio wameshiriki moja kwa moja katika mazishi haya kwa kufika Geita na wengine kufuatilia moja kwa moja kwenye matangazo ya Televisheni.

Vilio vimetawala kutoka familia, viongozi, na wananchi wa kawaida.

Mapema hii leo Hayati magufuli, aliagwa kwa misa maalum, ambayo ilifanika katika kiwanja cha wazi, Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Rais wa awamu ya nne, jakaya kikwete anamkumbuka rais Magufuli kama rafiki, ndugu na kiongozi ambae alikua mchapakazi sana.

Akieleza mahusiano yake na hayati Magufuli tangu alipokuwa waziri wake, Kikwete amesema alikuwa 'jembe lake'.

Nilipokuwa Rais, Magufuli alikuwa Waziri wangu kwa miaka 10, alikuwa mmoja wa mawaziri niliowaamini na kumtumaini.

''Alikuwa jembe langu ndio maana nilimuweka kwenye wizara tatu zilizokuwa ngumu ili anyooshe mambo.'' Alisema Kikwete.

''Yalikuwa matumaini yangu na matarajio yangu angemaliza kipindi chake cha uongozi salama, akastaafu na kuishi maisha marefu baada ya hapo na kupata nafasi ya kutuzika sisi watangulizi wake ambao ni kaka zake, hili la kututoka kabla ya kumaliza muhula wake na sisi kumzika yeye ni jambo ambalo sikuwahi kulifikiria kabisa.'' Alisema Kikwete.

Naye rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, alitoa hotuba yake ambayo ilipunguza huzuni iliyotanda, kwa maneno yake ambao yalifurahisha, na waombelezaji walionekana kufurahia na kusahau kwa muda uchungu wa kumpoteza mpendwa wao.

Rais Magufuli alifariki tarehe 17 machi kutokana na maradhi ya moyo wakati alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza Watanzania kuzika rais aliyefariki akiwa madarakani katika miaka 60 ya Uhuru.

Hayati rais Magufuli amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za ungozi, ubunge , uwaziri katika wizara mbalimbali na baadae rais wa Tanzania ambapo aliongoza kwa miaka sita.

Atakumbwa na watanzania kwa sera zake za kizalendo na kuweka Tanzania kwanza katika uamuzi wake.

Lakini pia jamii ya kimataifa itamkumbuka kwa jinsi alivyopambana na virusi vya corona kwa namna ya tofauti na mataifa mengine.