Motsepe na vihunzi vinne vinavyomkabili CAF

Bilionea Patrick Motsepe (59) ametangazwa rasmi siku ya Ijumaa kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kupitia Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo utakaofanyika Jumamosi, huko Rabat, Morocco.

Baada ya Motsepe kuibuka kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika Uchaguzi ambao ulienda sambamba na Mkutano Mkuu wa CAF, kutokana na yeye kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo jambo litakalowafanya wajumbe kumpigia kura za ndio au hapana tu.

Bilionea huyo raia wa Afrika Kusini anayemiliki klabu ya Mamelodi Sundowns alijikuta akiwa peke yake katika kinyang'anyiro hicho kufuatia kujiondoa kwa wagombea watatu ambao awali walionekana kama tishio kwake kabla hawajachukua uamuzi huo.

Wagombea hao waliojitoa ni Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Jacquise Anouma kutoka Ivory Coast, Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Senegal (SFA), Augustin Senghor na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Mauritania (MFF), Ahmed Yahya.

Inatajwa kuwa ushawishi wa Rais wa FIFA, Gianni Infantino umechangia kwa kiasi kikubwa Ahmed Yahya, Senghor na Anouma kujiondoa katika mchakato huo wa uchaguzi kwa kile kinachodaiwa kuwa bosi huyo wa chombo hicho kinachoongoza mchezo huo wa soka duniani anamuunga mkono Motsepe ambaye pia ni mfanyabiashara wa madini.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes ana utajiri unaokadiriwa kufikia kiasi cha zaidi ya Dola milioni 3 unaomfanya ashike nafasi ya tisa katika orodha ya matajiri barani Afrika huku kidunia akiwa nafasi ya 1513.

Lakini haiishii kwa ushawishi wa Infantino tu bali pia wagombea hao bila shaka wanaona kama Motsepe ni mtu sahihi wa kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu barani Afrika na kuimarisha ustawi wa mchezo huo kama alivyonukuliwa Senghor katika taarifa yake ya kujiengua kuwania nafasi hiyo.

"Kujiondoa kwangu katika ugombea wa Urais wa CAF kwa faida ya mgombea mwingine hakuwezi kukubalika na wote kwa sababu mbalimbali.

Ninalifahamu hilo lakini naamini ni uamuzi mzuri na sahihi," alinukuliwa Senghor.

Uamuzi huo wa watatu hao kujiondoa unaweza kuwa ishara ya imani ambayo wanayo kwa Motsepe kwamba anaweza kufanya yale ambayo wao kila mmoja kwa njia tofauti alikuwa akifikiria kuyatekeleza kwa ajili ya kuinua mchezo wa soka Afrika

Ni wazi kwamba Motsepe ana kibarua kigumu cha kuhakikisha kile ambacho wenzake ambao wamempa imani na Waafrika kiujumla anakitekeleza ndani ya kipindi cha uongozi wake.

Katika kuhakikisha hilo linatimia, Motsepe katika uongozi wake anapaswa kufanya kazi ya ziada kutibu matatizo manne sugu ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakichangia kurudisha nyuma mchezo wa soka ambao barani Afrika hapana shaka ndio unaongozwa kwa kupendwa na idadi kubwa ya watu wake.

Rushwa

Licha ya ahadi nyingi zilizotolewa na Marais waliopita wa CAF kuondoa tatizo la rushwa, bado limeendelea kuwa kansa inayotafuna soka na kadri siku zinavyozidi kusogea mbele limekuwa likiongezeka.

Kuanzia ngazi za nchini katika nchi wanachama wake hadi ndani ya shirikisho hilo, vitendo vya rushwa vimeonekana kukithiri kwa watu wa kada tofauti zinazohudumia mpira wa miguu.

Eneo ambalo rushwa katika soka inaonekana limejikita ni katika chaguzi mbalimbali za viongozi wa vyama na mashirikisho ya mpira wa miguu katika nchi tofauti ambazo ni wanachama wa CAF.

Iko mifano mingi ya namna chaguzi za soka zilivyogubikwa na rushwa na jinsi viongozi ama maofisa wanaosimamia mpira wa miguu wanavyojihusisha kwa namna moja au nyingine

Aliyekuwa Rais wa CAF, Ahmad Ahmad ambaye awamu yake iko ukingoni, mwaka jana alipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano na kwa kosa la rushwa ambayo alitoa kama ushawishi kwa wajumbe kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.

Ahmad alibainika kutoa fedha kiasi cha Dola 90,000 kutoka akaunti za CAF kuwalipia baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho hilo gharama za safari ya kwenda katika ziara ya Hijja huko Saudi Arabia, fedha jambo ambalo lilihusishwa na harakati za kiuchaguzi

Mwaka 2018 kamati ya maadili ya FIFA ilimfungia aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya baada ya kumkuta na hatia ya kupokea zawadi za rushwa kutoka kwa Mohammed Bin Hammam aliyekuwa akitajwa kuwa katika mpango wa kuwania Urais wa FIFA.

Matumizi mabaya ya Madaraka

Tatizo lingine ambalo limekuwa likiutafuna mpira wa Afrika ni matumizi yasiyo sahihi ya ofisi za mpira wa miguu ndani ya CAF na hata kwa nchi wanachama wake.

Viongozi wamekuwa wakitumia mamlaka yao vibaya kufanya maamuzi ambayo yamekuwa yakiwanufaisha wao binafsi na watu wanaowazunguka huku maendeleo ya mpira wa miguu yakishindwa kuonekana

Hili la matumizi mabaya ya ofisi ni miongoni mwa makosa yaliyopelekea Ahmad Ahmad Rais aliyepita wa CAF kukumbana na rungu kutoka FIFA la kufungiwa kutojihusisha na soka sambamba na faini.

Kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa na kamati ya maadili ya FIFA, Ahmad alikutwa na hatia ya kutumia mamlaka yake vibaya kuipa tenda kampuni ya Tactical Steel ambayo kati ya Disemba 2017 hadi Januari 2019, aliamrisha ilipwe kiasi cha Dola milioni 4.4 kwa matumizi ambayo hayakueleweka.

Lakini pia nchini Tanzania, aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo, Jamal Malinzi naye alikutwa na hatia na vyombo vya sheria vya nchini humo ya matumizi mabaya ya ofisi na ubadhilifu.

Motsepe anaonekana kulifahamu vyema hili na ndio maana ameliweka kuwa moja ya vipaumbele vyake katika kampeni.

"Tunahitaji ukweli na uwazi ili tujenge imani. Tukiweka akilini kwamba tunahitaji mpira wa miguu kuunganisha watu," alisema Motsepe.

Ukata

Hapana shaka hali ya kiuchumi kwa vyama na mashirikisho mengi ya mpira wa miguu Afrika sio nzuri lakini pia hata klabu nyingi nazo zimekuwa zikikabiliwa na hili.

Haishangazi kuona kiwango cha fedha za zawadi kwa washindi na washiriki wa mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na CAF kiko chini kulinganisha na mashirikisho kama UEFA na hata lile la Asia (AFC)

Kwa mfano wakati timu inayofuzu tu mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inakuwa imejihakikishia kiasi cha Euro 230,000 hata ikitolewa katika hatua za awali, katika Liginya mabingwa Afrika, fedha zinatolewa kuanzia katika hatua ya makundi ambapo timu inayotinga inakuwa imejihakikishia kiasi cha Dola 550,000 huku zile zinatolewa katika hatua za awali zinakuwa hazipati chochote tofauti na ilivyo kwa Ulaya.

Hili limekuwa likipelekea uwepo wa pengo kubwa kati ya baadhi ya timu na nyinginezo jambo ambalo limekuwa likichangia kupunguza ushindani katika mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na shirikisho hilo.

Kwa mfano katika mashindano ya ngazi ya klabu, timu kutoka Kaskazini mwa Afrika zimekuwa zikifanya vyema zaidi kulinganisha na zile kutoka kanda nyingine za soka.

Migogoro

Jambo lingine ambalo limekuwa likichangia kurudisha nyuma mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika ni migogoro na mifarakano ya mara kwa mara katika vyama vya michezo na hata ndani ya CAF.

Hii imekuwa ikipelekea makundi baina ya watu waliopewa mamlaka ya kusimamia soka na kufanya shighuli za maendeleo ya mchezo huo kusuasua na wakati mwingine kukwama

Muda mwingi umekuwa ukitumika kutatua migogoro ambayo mara kwa mara chanzo chake huwa ni uroho na tamaa ya madaraka baina ya wadau wa mpira wa miguu