Thembi Nkambule: Mwanamke mwenye ukimwi anayewasaidia wengine 'kufa kifo kizuri'

Chanzo cha picha, SHALI REDDY
Thembi Nkambule amekuwa akiwahudumia mamia ya watu wanaofariki kutokana na Ukimwi Eswatini - nchi ambayo mtu mmoja kati ya wanne ana HIV. Haya ndio mambo aliyojifunza juu ya maana ya "kifo kizuri".
Thembi anaangazia vifo vya aina tatu.
Cha kwanza ni kile ambacho ni cha kawaida. Mtu anamwangalia machoni na kusema peupe "Imeisha. Nimekata tamaa." Thembi anashudia wanapofunga macho na kuaga dunia. Maisha walioishi kisiri yakiisha kwa fedheha. Hiki ni kifo kibaya.
"Alafu kuna aina ya pili ya kifo," Thembi anasema. "Mtu ana ujumbe, au tahadhari, kwa watu anaowaacha nyuma. Kuna somo walilojifunza ambalo wanataka kuwasilisha."
Aina ya tatu ni kifo kizuri. Mtu anayekaribia kufariki akijua kwamba ataacha famililia yake na jamii katika hali nzuri ikiwa mizozo yoto imesuluhishwa. Kifo cha aina hii hakihitaji uwepo wa Thembi, ijapokuwa yeye huwepo mara kwa mara katika dakika za mwisho za mgonjwa yeyote.
Nchi ya Eswatini ambayo - zamani ilikuwa ikijulikana kama Swaziland - imetajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa "kitovu cha janga la UKIMWI duniani "- wataalam wa janga hilo wanasema hali inazidi kuwa mbaya kutokana na Covid -19.
Ijapokuwa hatua kubwa zimepigwa katika juhudi za kukabiliana na virusi vya Ukimwi katika miongo kadhaa iliyopita, nchi hiyo iliyo na watu milioni 1.3 bado ina kiwango cha juu cha maambukizi ya HIV, inakadiriwa kuwa asilimia 26.
Lakini hali ilikuwa mbaya sana miongo kadhaa iliyopita.

Chanzo cha picha, SHALI REDDY
"Kifo kilikuwa kila mahali wakati huo," Thembi anasema.
Anakumbuka vizuri sana mara ya kwanza alipogundua kwamba amepata HIV.
Ilikuwa kati kati ya miaka ya 90 na ndio mwanzo alikua ameolewa na kuwa mama akisoma chuo kikuu cha Swaziland. Kulikuwa na mpango wa utoaji damu nchini. Baadhi ya marafiki wa Thembi walikua wametoa damu, lakini wiki chache baadae waliacha masomo, na hawakuwahi kurudi tena.
"Kulikuwa na uvumi kwamba damu yao iligunduliwa kuwa na virusi vya ugonjwa hatari," anasema. "Hakuna kitu kilichothibitishwa na serikali au mamlaka, lakini uvumi ulikuwa mtu akipatikana na ugonjwa huo, hakuna matumaini ya kupona, ni kifo tu."
Hofu ilizonga chuo kizima, Thembi na baadhi ya marafiki zake hawakujitolea damu.
"Tulihofia kutoa damu tusije tukaambiwa kwamba damu yetu ina virusi, kwa hiyo tulikuwa salama."
Miaka kadhaa baadae, wakati Thembi akifanya kazi ya ualimu katika shule ya upili, alianza kusikia mengi kuhusu HIV. Wakati huo ilikuwa imeathiri sehemu kubwa ya nchi, wakiwemo waalimu, marafiki zake, na cha kutia wasi wasi zaidi, wanafunzi wake.

Chanzo cha picha, SHALI REDDY
Aliweza kubaini watu wanapokuwa wagonjwa, kwasababu walitoweka ghafla. Kujitenga na watu na kila mtu. Wiki chache baadae atasoma kuhusu vifo vyao magazetini - ijapokua chanzo cha kifo hakikuwahi kutajwa.
Lakini mwanzo wa miaka ya 2000, HIV ilianza kuripotiwa katika vyombo vya habari na kujadiliwa kwenye redio. Thembi alienda maktaba kusoma kuhusu kirusi hicho, ambacho kimewaathiri watu kote duniani. Alifahamu mengi kuhusu ugonjwa uliosababisha waathirika kunyanyapaliwa katika jamii.
Ilifahamika kwamba virusi vya ugonjwa huo wa ukimwi vingeweza kusambazwa kupitia ngono lakini baadhi ya viongozi katika jamii wakaongeza nadharia zao wenyewe kuhusu ugonjwa huo.
Watu tu wenye maadili mabaya ndio walioambukizwa, baadhi ya viongozi wa kidini makanisani walisema.
Hata hivyo Thembi alijua kwamba hilo sio kweli, kwasababu alimjua mwanamke mmoja ambaye alikuwa na mahusiano ya mapenzi na mume wake tu ambaye aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa ukimwi.
Na badala ya Thembi kuogopa waliopata maradhi hayo kwasababu ilisemekana hao ni wenye tabia za kishetani, wakati huo wakiwa wanatengwa na familia zao na marafiki, aliamua kuchukua hatua ya kuwatembelea majumbani na kuwafariji.
"Wakati mwingine ningegonga mlangoni na mtu hangeniruhusu kuingia," anasema. "Walikuwa wanaona aibu sana. Lakini mimi nilisubiri huku nikiwaambia kwamba iwapo mtu atanihitaji niko nje ya mlango wake. Sikuwaogopa kabisa."
Mwaka 2002 akapatwa na kikohozi ambacho kilidumu. Mara ya kwanza alichukulia kawaida akidhani kwamba ni homa. Lakini homa hiyo iliendelea.
"Pengine," alifikiria akiwa peke yake, "kikohozi hiki kimekataa kuisha kwasababu nina HIV."
Thembi aliamua kwenda kupimwa. Na majabu yakaonesha kwamba ameathirika.
Wiki za kwanza baada ya kupimwa alizongwa na hofu ya ajabu.
"Nilipataje ugonjwa huu?" Thembi akawa anawaza, "Je kipi kitakachotokea kwa watoto wangu watatu?"

Chanzo cha picha, SHALI REDDY
"Nitafariki dunia lini?"
"Nilijua kile ambacho kingenitokea, ningehitaji usaidizi na upendo kutoka kwa wengine niliowapenda," anasema.
Aliwaambia kwamba ugonjwa wake hauwezi kurithishwa kwa mwingine kupitia kumkumbatia mtu au kutumia naye bafu moja. Na kuwaahidi kwamba atakuwa akipata matibabu.
Tangu alipopatikana nao, alikuwa amegundua kuhusu mpango unaofahamika kama 'People Living with HIV', na pia angeshirikiana nao kusaidia waliathirika akiwemo mume wake.
Yeye na mume wake waliwakalisha watoto wao na kuzungumza nao kuhusu hali zao za HIV.
Asijue kwamba miaka michache ijayo ndiye angekuja kuwa mkurugenzi wa mpango huo. Tajriba aliyokuwa nao katika kuishi a ugonjwa huo ilimaanisha kwamba wengi walifungua mioyo yao akiwa nao.
Wengi waliokuwa wanataabika kwasababu ya ukimwi walimuomba kuwa naye wakati wa dakika zao za mwisho maishani.
"Hilo nililichukua kwa uzito mkubwa," anasema, "Nilikiona walichokuwa wanakihitaji wakati huo hata kabla ya kusema nao lolote. Wengine walitaka niwashike mkono. Wengine hawakutaka kushikwa lakini walitaka mtu kuwa karibu nao. Kila mmoja nilimchukulia vile alivyopenda yeye. Na kuwapa heshima zao."
Alitaka wawe na kifo kizuri.
'Kifo kizuri' ni nini?
Dhana ya uwepo wa kifo kizuri imekuwepo kwa muda mrefu. Mwaka 1601 katika kanisa la England, kasisi Christopher Sutton aliandika kwamba kufa vizuri kunajumuisha kufa ukiwa kitandani huku wapendwa wako wakiwa wanakutazama.
Aligusia kwamba katika kifo cha ghafla mtu anakuwa hajapata muda wa kuaga wapendwa wake lakini ingawa kuumwa kwa muda mrefu kando na kwamba kunaumiza pia ni mzigo kwa wengine.
Kulingana na shirika moja lisilo la serikali Marekani, kifo kizuri ni kile ambacho mgonjwa hajaumwa hajakuwa na machungu moyoni.
"Leo hii mwaka 2021, idadi ya wanaopata ugonjwa wa virusi vya ukimwi au kufariki dunia kutokana na virusi hivyo ni ndogo sana nchini Eswatini nikilinganisha na wakati mimi naguduliwa kuwa ugonjwa huo," Thembi amesema, "lakini kwasababu ya kanuni zilizowekwa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, kutokana na kile ninachokisikia, huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Pia inasemekana kwamba kuna ongezeko la visa vya dhulma dhidi ya kwanawake ikiwemo ubakaji.
Kwa Thembi, "kifo kizuri ni amani".
"Kwa wenye HIV na ukimwi, ni vigumu sana kwa waathirika kuwa na amani. Kuondoka katika dunia hii bila majuto," amesema, "Huwa ninawaambia kwamba mwisho wa siku, maisha ni kuwa na amani moyoni mwako kwa maamuzi uliofanya kipindi ulichukuwa.
"Wengine watakuchukulia vile unavyojichukulia," Thembi amesema.
"Hakuna anayeweza kukufanya kuwa na aibu kama mwenye huoni aibu. Na hakuna anayestahili kuona aibu kwasababu ya ugonjwa."












