Uhaba wa mafuta ya kupikia Tanzania

    • Author, Eagan Salla
    • Nafasi, BBC Swahili

Tangu mwishoni mwaka 2020 kumekuwa na ongezoko la bei ya mafuta ya kupikia kutokana na kuadimika kwa bidhaa hiyo muhimu kwenye soko la dunia.

Kiwango kikubwa cha mafuta ya kupikia yanayotumika Tanzania huagizwa kutoka nchini Malyasia ambako kutokana na athari za maambukizi ya virusi vya Covid 19 uzalishaji umedorora na kupelekea uhaba uliosababisha kupanda kwa bei.

Awali lita moja ya mafuta haya ilikuwa ikipatikana kwa kati ya shillingi 3000 mpaka 4500 wastani wa dola mbili za marekini lakini sasa lita moja ni shilingi ni 6500 hadi 7000 sawa na dola tatu za kimarekani hivyo kuwaathiri pakubwa watumiaji wa mafuta haya.

Kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa chakula almaarifu mama ntilie wenyewe wanasema kwa sasa wanafanya biashara kwa mazoea tu kwani hawawezi kupandisha bei za chakula sababu wengi wateja wao ni watu wa hali ya chini na hawatamudu kununua chakula kwa gharama za juu.

Uhaba huu si kwa watumiaji wamwisho pekee bali hata kwa wengi wa wafanya biashara wadogo wadogo ambao huyapata kwa uchache na kwa bei juu toka kwa wafanyabiashara wa jumla.

Serikali imelitolea ufafanuzi swala hili na kueleza kuwa itaendelea kuhakikisha mafuta yaliyo agizwa yanafika kwa wakati na kushushwa kwa kipaumbele licha ya kukiri kuwa athari za virusi vya corona kwingineko duniani zimechangia, akikaririwa na vyombo vya habari vya ndani mwezi mmoja ulipita waziri wa viwanda na biashara nchini Tanzania.

Godfrey Mwambe amesema wana weka mikakati madhubuti ya kumaliza tatizo hilo ikiwemo kuwapatia mashamba wafanya biashara wakubwa ili kulima mazao kama michikichi yanatumika kuzalishia mafuta ya kupika ili kuondokana na uhaba huo siku zijazo.

Uhaba huo na kuongezeka kwa bei kulianza kushuhudiwa mwishoni mwa mwaka jana na huenda hali ikazidi kuimarika kani serikali licha ya kusimamia uagizwaji imekemea vikali wafanya biashara wachache wanaoyaficha mafuta hayo ili kusababisha upungufu utakaopelkea ongezeko la bei.