Nabii Shepherd Bushiri: Kasri ya Mchungaji milionea Bushiri na mkewe Mary imeshikiliwa na mahakama ya Afrika Kusini

Nabii milionea wa Malawi Shepherd Bushiri anayehubiri nchini Afrika Kusini na mkewe Mary wamejipata pabaya baada ya mahakama ya Afrika Kusini kuamuru kushikiliwa kwa nyumba yao baada ya kukwepa kesi ya dhamana.

Kasri hiyo ya kifahari iliyopo karibu na mji wa Pretoria ina thamani ya randi milioni 5.5 za Afrika Kusini sawa na dola 350,000 au pauni 260,000, kwa mujibnu wa taarifa.

Jaji aliwaamuru Nabii Bushiri na mke wake kutoa stakabadhi za nyumba wakati mahakama hiyo ilipowapa dhamana kufuatia tuhuma za utakatishaji wa fedha na ufisadi zinazowakabili.

Hatua hii ya mahakama inakuja wakati Mchungaji huyo maarufu akikabiliwa na mashitaka 419 na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini.

Wakati huo huo mahakama ya Malawi ilimuachilia huru nabii Shepherd Bushiri na mke wake baada ya kukamatwa mapema leo.

Afrika Kusini bado inawataka Bushiri na mke wake ambao walitorokea nchini kwao Malawi warejee Pretoria kukabiliana na mashitaka dhidi yao.

Nabii Shepherd Bushiri na mke wake Mary Bushiri ambaye pia ni Nabii walikanusha tuhuma dhidi yao mwishoni mwa juma, kupitia ujumbe walioutuma kwenye mitandao ya kijamii wakidai walikuwa nchini Malawi kwa kuhofia usalama wao.

Tayari Afrika Kusini imekwishatoa kibali cha kuwakamata wawili hao na wanataka mamlaka za Malawi ziwarejeshe nchini Afrika Kusini kukabiliana na kesi yao .

Shepherd Bushiri ni nani ?

Nabii Mchungaji Shepherd Bushiri ni mzaliwa wa Malawi ambaye huendesha shughuli zake za "unabii" katika makanisa mbalimbali kuanzia Ghana hadi Afrika Kusini.

Anadai kuwa anatibu virusi vya Ukimwi/HIV na kuwafufua watu, kwa mujibu wa magazeti ya Afrika Ksuini ya Mail & Guardian yaliyotolewa 2018.

Bushiri aliwahi kubashiri kuwa Uingereza itagawanyika, "majimbo" na itaingia vitani na kuwa katika "vurugu", jarida la Maravi Post lilisema katika moja ya ripoti zake.

Na katika moja ya video zake alionekana akitembea hewani, video ambayo ilisambaa sana katika mitandao ya kijamii .

Bushiri alimwambia mwanasiasa wa Zimbabwe Kembo Mohadi kuwa atapata "madaraka " hata kabla ya kutangazwa kuwa makamu wa rais, kulingana taarifa ya New Zimbabwe.

Mchungaji Shepherd Bushiri ni muanzilishi wa kanisa la Afrika Kusini lenye matawi yake katika nchi nyingine.

Wengi husema Mchungaji milionea ndiye kiongozi wa kidini tajiri zaidi barani Afrika.

Mchungaji Bushiri alikulia katika mji wa Mzuzu, uliopo Malawi kabla ya kwenda Pretoria nchini Afrika Kusini.

Taarifa zinasema kuwa alipigwa marufuku kukanyaga katika ardhi ya Botwana kwasababu ya "pesa za miujiza".

Amekuwa maarufu sana kutokana na mikusanyiko mikubwa ya wafuasi wake wanaojaa katika viwanja vikubwa vya michezo.

Lakini watu wanamshutumu kuwa anawatumia vibaya masikini wanaotaka kubadili hali zao za maisha kwa kuwauzia "mafuta ya muujiza" .

Akifahamika kama Major 1 au Nabii Shepherd , Bushiri alizaliwa tarehe 20 Februari, 1983.

Mamlaka za Botwana zilifunga kanisa lake baada ya madai kuwa alikuwa anawataka watu wampatie pesa bila huduma yoyote, kitu ambacho kilikuwa ni kinyume na sheria za fedha nchini humo.

Mke wa Nabii Bushiri Mary ni nani?

Mary Bushiri ni mke wa Shepherd Bushiri. Anafahamika zaidi kama [Prophetess Mary Bushiri].

Alikuwa akifanya kazi kama muhasibu katika moja ya mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali . Lakini sasa amekuwa muhubiri sawa na mumewe.

Mary Bushiri na Shepherd Bushiri walioana Julai 2011.

Harusi ya Nabii Shepherd Bushiri ilifanyika katika uwanja wa michezo wa Mzuzu ,na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Kesi yake imefikia wapi?

Bushiri, na mke wake na watu wengine wawili wanakabiliwa na shutuma za kutakatisha fedha na mashitaka mengine 419.

Wapelelezi wa uhalifu wanasema kesi hiyo inahusu ina thamani ya randi ya Afrika kusini milioni 102 ($6.6m).

Alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Pretoria tarehe 21 Oktoba na kesi yake ilitarajiwa kuanza Mei.

Akifahamika kama Major 1 au Nabii Shepherd , Bushiri alizaliwa tarehe 20 Februari, 1983.

Mamlaka za Botwana zilifunga kanisa lake baada ya madai kuwa alikuwa anawataka watu wampatie pesa bila huduma yoyote, kitu ambacho kilikuwa ni kinyume na sheria za fedha nchini humo.