Polisi waingilia kati baada ya umma kuchukua sheria mkononi dhidi ya walawiti Uholanzi

Mkuu wa Polisi wa uholanzi ametoa wito wa kumalizika kwa kile kinachoitwa "uwindaji wa walawiti wa watoto"baada ya mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 73 kupigwa na wanafunzi wake vijana wadogo hadi kufa kutokana na madai ya kulawiti.

Oscar Dros amesema kuwa kuna hatari kwamba watu zaidi wanaweza kufa na amewaomba watu waache haki itekelezwe na mamlaka.

Mwanaume huyo kutoka katika mji wa Arnhem alidanganywa hadi akaingia kwenye mawasiliano ya kingono na mvulana mdogo alipokuwa katika mazungumzo ya mtandaoni ya wapenzi wa jinsia moja.

Haijafahamika iwapo alifahamu kwamba mvulana aliyekuwa anaongea nae alikuwa na umri wa miaka 15.

Haijawa wazi pia iwapo mwalimu huyo wa zamani alikuwa kweli mlawiti au la.

Shambulio hilo katika mji wa Arnhem Uholanzi ni la hivi karibuni katika msururu wa matukio yanayohusiana na kile kinachojulikana "wawindaji wa walawiti " katika nchi ya Uholanzi, kulingana na taarifa.

Ni nini hasa kilichotokea katika mji wa Arnhem

Taarifa zinasema kuwa kikundi cha vijana wadogo kimekuja na wazo la kuwawinda wabakaji baada ya kusoma hadithi kuhusiana na matukio ya ulawiti kutoka katika maeneo mengine ya Uholanzi.

Mwalimu wa zamani aliwasili katika eneo walilokubaliana kukutana na vijana hao tarehe 28 Oktoba na baadaye aliondoka kuelekea nyumbani kwake.

Alipigwa na kikundi cha wavulana na kufa baadaye katika hospitali.

Meya wa Arnhem- Ahmed Marcouch amezungumzia kuhusu "uhalifu mbaya " akasema umekuwa na athari miongoni mwa jamii za eneo hilo .

Makumi kadhaa ya majirani, marafiki na wanafunzi wa zamani wa mwalimu huyo walishiriki katika kumkumbuka muathiriwa huyo mwishoni mwa juma lililopita.

Wakili wa mvulana mwenye umri wa miaka kumi na mitano aliyekuwa na mazungumzo na marehemu aliuambia wavuti wa eneo hilo De Gelderlander kwamba wazo la kuwawinda walawiti "lilijitokeza kutokana na upweke uliosababishwa na kipindi cha corona ".

Mteja wake alishabikia sana wazo hilo lakini binafsi hakushiriki katika shambulio la marehemu.

Jamil Roethof alidai kuwa vijana hao wadogo walio katika umri wa barehe walitaka tu kukabiliana na mwanaume na hawakuwa na nia ya kumshambulia.

Anasema alikufa tu kwa bahati mbaya.

Vijana wadogo kumi na saba walikamatwa, sita kati yao wakiwa na umri wa miaka 18, na wawili wanashikiliwa mahabusu.

Polisi imesema nini ?

Mkuu wa polisi kanda ya Uholanzi Mashariki Oscar Dros amewaomba raia wa Uholanzi kuacha kujichukulia sheria mkononi dhidi ya walawiti :

"Acheni uwindaji wa walawiti, muache kuwafunga, muache uchokozi-mtuachie sisi jukumu hili."

Bw Dros ameliambia gazeti la Algemeen Dagblad kwamba tangu Julai matukio yapatayo 250 yamerekodiwa juu ya uwindaji wa kibinafsi wa walawiti, na huenda yakawawepo mengine mengi zaidi.

Uwindaji huo sasa umepigwa marufuku na polisi na waendesha mashitaka wa serikali.

Watu wamekuwa wakifukuzwa bararani, kupigwa, kutishiwa na kuaibishwa mbele kwenye mitandao ya umma ya kijamii, alisema .

Makundi ya Facebook yameibuka kila upande wa nchi, yenye majina pedohuntnl, na baadhi yamewavutia maelfu ya wafuasi.

Mjumbe wa kikundi kimoja aliliambia shirika la habari la umma NOS kwamba "tunafanya hili kuwakinga watoto wetu ".

Dakika kadhaa baada ya kuingia katika mazungumzo ya mtandao, alidai kuwa wanaume watano kati ya sita watajaribu kufanya mazungumzo na wewe , huku wakifahamu fika kuwa una umri mdogo .

"Hilo sio sahihi kabisa."

Makundi sawa na hayo yameonekana pia nchini Uingereza, na mkuu wa polisi amekwisha sema kuwa shughuli kwa ujumla za makundi ya aina hiyo "sio nzuri ".

Mkuu wa polisi wa Uholanzi alisema kuwa tabia za makundi ya aina hiyo ya kujilinda "hazina faida, kwasababu ushahidi wananchi hawa wanaouamini mara nyingu huwa ni mdogo sana ".

Alisema anafahamu mfano mmoja tu wa mlawiti aliyeishia kupatikana na hatia.