Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simulizi katika mtandao wa Instagram kuhusu mapenzi haramu
Nchini India, mapenzi na ndoa kukosolewa kwasababu ya matabaka na dini kwa kipindi kirefu limekuwa jambo la kawaida lakini hilo huenda limepata pigo baada ya kuanzishwa kwa mpango mpya wa kukabiliana na vizuizi vya imani, tabaka, dini na jinsia katika mapenzi.
Mwanahabari wa BBC Geeta Pandey kutoka Delhi ametuandalia taarifa hii.
Kwa miaka mingi, nchini India ndoa zimekuwa zikikutana na kizingiti cha dini huku wanaojadiliwa sana ikiwa ni ndoa kati ya wanawake wa Kihindi na wanaume Waislamu.
Ni hivi majuzi tu ambapo mjadala ulizuka pale kampuni kubwa ya kuuza vito vya thamani ilipofuta tangazo lake lililokuwa linahusisha wanandoa wa dini tofauti baada ya ukosoaji mkubwa kutoka watu katika mitandao ya kijamii.
Tangazo hilo lilijumuisha hafla ya mama anayetarajiwa kupata mtoto iliyoandaliwa na wakwe zake wa dini ya Kiislamu na yeye mwenyewe akiwa ni wa dini ya Kihindu.
Tangazo hilo dhamira yake ilikuwa ni kuonesha umoja kwa watu mbalimbali lakini kilichojitokeza ni kinyume chake - na kutonesha kidonda katika jeraha ambalo tayari lilikuwepo kwenye jamii nyingi India.
Makundi ya Kihindi yenye msimamo mkali yalisema kuwa tangazo hilo linahamasisha "mapenzi ya jihad" - neno la Kiislamu linalotumika kuonesha kuwa Wanaume wa Kiislamu wanapanga njama ya kuona wanawake wa Kihindi lengo lao likiwa moja tu, wabadilishe dini zao hadi Uislamu.
Wito unaotolewa kwenye mitandao ya kijamii ni kususia bidhaa za kampuni iliyotoa tangazo hilo hasa katika mtandao wa Twitter.
Aidha kampuni hiyo imesema imefuta tangazo hilo kwa kutilia maanani usalama wa wafanyakazi wake.
Wiki mbili tu baada mzozo wa tangazo hilo, mwanahabari Samar Halarnkar na mke wake Priya Ramani kwa ushirikiano na rafiki yao Niloufer Venkatraman ambaye pia ni mwanahabari wakazindua mradi wa ''India Love Project'' katika mtandao wa Instagram na kuuelezea kama wenye lengo la "kusherehekea ndoa za wapenzi wa dini na matabaka tofauti tofauti na umoja katika nyakati za mgawanyiko zilizojaa chuki".
Bwana Halarnkar ameiambia BBC "wamekuwa wakiufikiria mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na utata uliosababishwa na kampuni ya Tanishq umefanya kuwa wakati mwafaka kuuzindua.
"Kumekuwa na dhana kwamba nia ya kuingia kwenye ndoa ni tofauti na mapenzi ya dhati na pia mapenzi yamekuwa yakitumika kama silaha. Lakini hakuna anayejulikana kwa kuwa na nia tofauti ya kuingia katika ndoa zaidi ya mapenzi."
Katika jukwaa la India Love Project, alisema, "tunachofanya ni kutoa jukwaa ambapo watu watakuwa wanashirikishaka simulizi zao", mwanzilishi wa mradi huo amesema.
Miaka ya hivi karibuni, serikali iliyo madarakani nchini India ikiwa ya Kihindi, wenye msimamo mkali wamekuwa wakiungwa mkono huku mgawanyiko wa kidini ukiendelea.
Ndoa nyingi zinazoathirika zikiwa ni zile za wanawake Wahindi wanaoolewa na wanaume Waislamu.
Mradi wa ''India Love Project unatoa wito wa watu kushirikishana waliopitia kwenye ubaguzi wa kindoa.
Na ndani ya maneno 150, simulizi zinaandikwa kwa upendo na usheshi; na wanandoa wanaoamini kuwa mapenzi hayatambuliwi kwa mipaka ya mwanadamu.
Rupa, ambaye ni Mhindi ameandika vile mama yake alivyojibu wakati alipomuambia kuwa anapanga kumuoa Razi Abdi, Mwislamu.
"'Talaq, talaq, talaq' mara tatu kisha anakutoa ndani ya nyumba yake," mama yake alisema, akiwa na wasiwasi juu ya tabia ya Waislamu ya kutalakiana papo hapo ambayo sasa hivi imepigwa marufuku nchini India.
"Hata hivyo wazazi wangu walipokutana na Razi na kutambua jinsi alivyo na utu, wasiwasi wao uliondoka," anaandika na kuwaelezea kama "wenye uwazi wa fikra".
Sasa ni miaka 30 tangu Rupa na Razi walipooana.
Wamebarikiwa na vijana wawili wakubwa na husherehekea sikukuu ya Kiislamu ya Eid pamoja na ile ya Kihindi ya Diwali.
Akiandika kuhusu ndoa yao, Salma ambaye ni mwanahabari anasema katika nyumba yake, dini haijawahi kuwa angalizo kubwa kama ilivyo kwa vyakula vya "wali na biriani ya nyama ya kondoo!"
"Mimi nakula mboga mboga, yeye anafurahia nyama ya kondoo na mapenzi yetu yamekuwa moto moto daima."
Wenyewe wanasema, simulizi kama hizi ndio zinazowafanya kuhisi vizuri zaidi juu ya dunia na India.
Hizi ni baadhi ya simulizi zinazoelezea uhalisia wa hali ilivyo nchini India. Watu wanafuata njia tofauti tofauti kwasababu ya mapenzi. Ni ukumbusho wa vile India ilivyo.