Utata juu kukamatwa kwa 'shujaa' wa filamu ya mauaji ya Rwanda.

Baada ya Paul Rusesabagina kuonyeshwa mbele ya waandishi wa habari na maafisa wa upelelezi wa serikali ya Rwanda (RIB) sasa familia yake inasema kuwa alikuwa safarini Dubai wakidai kuwa alitekwa nyara.

Akizungumza na BBC mtoto wa kike wa Bwana Rusesabagina -Anaïse Kanimba alisema :''alitekwa nyara alipokuwa safarini Dubai ", katika Muungano wa nchi za kiarabu (UAE).''

"Alifika Jumanne, ndio mara ya mwisho tulipozungumza nae akituambia kuwa amefika salama, hatukumsikia tena hadi tulipoona kuwa amekamatwa na utawala wa Rwanda.

"Hatujui alifikaje huko na kilichotokea, ndio maana tunafikiria kuwa alitekwa kwasababu asingeenda Rwanda kwa hiari yake."

Anaishi uhamishoni Marekani na ni raia wa ubelgiji , aliongeza.

"Kwahiyo tungependa nchi hizi mbili zitusaidie kumrudisha nyumbani.

"Mashitaka wanayomshitaki hayana msingi ," Bi Kanimba aliongeza katika mahojiano na kipindi cha BBC Newsday

Bwana Rusesabagina, 66, ni mkosoaji mkubwa wa rais Paul Kagame.

Unachosema Muungano wa kisiasa unaoongozwa na Rusesabagina

Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda Faustin Twagiramungu na mkosoaji mkuu wa serikali ya Kigali ambaye ndiye msemaji wa Muungano wa vyama vya upinzani,unaoongozwa na Rusesabagina -MRCD-Ubumwe, ameiambia BBC pia kwamba alitekwa nyara:

"Tunafahamu vyema kuwa alikamatwa katika miji alikotoka, hatukufahamu kuwa alikuwa amesafiri Dubai . Alikua katika matembezi yake ya kibinafsi sio kuhusu vyama vyetu hivi."

Serikali ya Rwanda imesema nini.

Kwa upande wa serikali ya Rwanda, inasema kwa muda mrefu jina la Bwana Rusesabagina lilikua miongoni mwa majina yaliyopo kwenye waranti ya kimataifa, kwa ajili ya kukamatwa na kuwasilishwa katika mahakama za Rwanda.

Ofisi ya Rwanda ya upelelezi (RIB) ilisema kuwa amekamatwa kwa ushirikiano wa kimataifa.

'' Rusesabagina anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikiwa ni pamoja na ugaidi, utekaji, kuchoma moto mali na mauaji'' , alisema kaimu msemaji wa Ofisi ya Rwanda ya upelelezi (RIB) Dkt Thierry Murangira .

Bwana Murangira aliwaambia waandishi wa habari kuwa uhalifu anaodaiwa kuufanya aliutekeleza dhidi ya Wanyarwanda ambao hawakuwa na silaha, wasio na hatia kwenye ardhi ya Rwanda ikiwa ni pamoja na mashambulizi yaliyotekelezwa katika wilaya ya Nyaruguru Juni 2018, Nyungwe, na Wilaya ya Nyamagabe Disemba 2018.

Waziri wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda , Johnston Busingye alisema kuwa kukamatwa kwa Rusesabagina ni ujumbe wa wazi kwa yeyote anayeua au kufanya ugaidi dhidi ya Rwanda atakamatwa.

"Wale wanaoshukiwa kuua na kufanya ugaidi dhidi ya Wanyarwanda , wale wanaopanga, kudhamini kwa pesa ugaidi dhidi ya Wanyarwanda wataletwa mbele ya sheria," alisema.

Waziri Busingye alipongeza ushirikiano wa kimataifa na juhudi zilizofanyika katika kumkamata Bwana Rusesabagina.

Ni kwanini Rusesabagina amekamatwa sasa?

Paul Rusesabagina, ni kiongozi wa muungano wa kisasa MRCD-Ubumwe ambao Rwanda inauhusisha na mashambulio ya ugaidi yaliyowauwa Wanyarwanda katika kituo cha polisi cha mjini Kigali.

Rusesabagina alipata umaarufu baada ya kucheza filamu ya Hollywood kwa jina Hotel Rwanda iliyotolewa mnamo mwaka 2004.

Katika filamu hiyo , Paul Rusesabagina aliangaziwa kama mtu aliyetumia ushawishi wake - na rushwa- kuwashawishi maafisa wa kijeshi kuwapa njia salama ya kuwatorosha karibu watu1,200 ambao walitafuta maficho katika Hôtel des Mille Collines, ambayo alikuwa meneja wake wakati wa mauji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Baada ya filamu hiyo kutolewa Bw. Rusesabagina alitunukiwa medali ya Rais wa Marekani ya Uhuru 2005,George Bush.

Hata hivyo kundi la manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Ibuka lilisema kuwa alitilia chumvi jukumu lake la kuwasaidia wakimbizi kujificha hotelini katika siku 100-za mauaji ya kikatili mwaka 1994.

Jina la Rusesabagina hivi karibuni lilikuwa katika kesi ya ugaidi nchini. Mahakama ilisikiliza madai kwamba kundi la waasi wa the National Liberation Front (FLN), lilipokea msaada kutoka kwa rais wa Zambia Edgar Lungu kwasababu ya urafiki wake wa karibu na Bwana Rusesabagina. Msemaji wa Bwana Lungu alikana madai hayo katika mahojiano na BBC.

Mwaka 2011, Bwana Rusesabagina alishutumiwa kudhamini kundi na muungano wa makundi ya ugaidi yenye silaha na itikadi kali.

Rusesabagina ni Naibu kiongozi wa muungano wa vyama vya kisasa vinavyoipinga serikari ya Kigali wenye makundi ya kijeshi -FLN -unaoendesha harakati zake mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mwaka 2018, kundi la FLN lilidai kufanya mashambulizi kwenye ardhi ya Rwanda kwenye maeneo ya msitu wa Nyungwe ambapo watu wengi waliuawa.

Unaweza pia kusoma: