Félicien Kabuga: Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa

Félicien Kabuga, mmoja wa washukiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, amekamatwa karibu na mji wa Paris, wizara ya sheria ya Ufaransa imetangaza.

Bwana Kabuga ameshikiliwa na polisi mjini Asnières-Sur-Seine, eneo ambalo alikuwa anaishi kwa kutumia majina bandia.

Marekani ilitoa dau la dola milioni 5 kwa atakayeweza kutoa taarifa kuhusu bwana Kabuga ili aweze kukamatwa.

Mahakama ya kimataifa ya mauji ya kimbari yaliyotokea Rwanda yamemshtaki bwana Kabuga mwenye umri wa miaka 84 kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Anadaiwa kuwa mfadhili mkuu wa wahutu ambao waliuwa watu 800,000 mwaka 1994.

Walikuwa wanawalenga kundi dogo la jamii ya Tutsi pamoja na wapinzani wao siasa.

Kabuga ni nani?

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alichukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biasahara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'mbo.

Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari , alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi RTLM ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.

Kutokana na utajiri wake, baada ya mauaji ya kimbari Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, alifanikiwa kujificha katika mataifa mengi hadi alipokamatwa Mei 16,2020.

Hatua hiyo imepokelewaje

"Kila mmoja amefurahia hatua ya kukamatwa kwake, kila mmoja amekuwa akisubiri habari hizi kwa sababu alikuwa katika orodha ya washukiwa wa mauaji ya kimbari" - Valerie Mukabayire kiongozi wa chama cha wajane wa mauaji ya kimbari AVEGA aliiambia BBC.

"Ni jambo la kutia moyo sana kwamba hatimaye atafikishwa mbele ya haki kuwajibikia kile alichokifanya" - aliongeza.

Ahishakiye Naphtal, Katibu mkuu wa Ibuka, chama Tanzu cha wahathiriwa wa mauaji ya kimbari anasema hizi ni habari njema kwa waliopona mauaji hayo, kusikia Kabuga amekamatwa baada ya miaka 26.

Bwana Ahishakiye anasema Ufaransa chini ya uongozi wa rais Emmanuel Macron imebadili mtazamo wake kuhusu watuhumiwa waliotoka katika mauaji ya kimbari ya Rwanda, 'Hali ambayo imechangia hatua ya kumkamata' anasema.

"Tunaomba angelifunguliwa mashitaka Rwanda, ingelitoa ujumbe muhimu kwa Wanyarwanda wote hususani waliopanga na kutekeleza mauaji ya kimbari" - Bw. Ahishakiye aliongeza.

Mahakama ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda imesema ilikuwa imetoa waranti ya kumkamata na kutangaza kukamata.

Mahakama hiyo ina vitengo mjini Arusha, Tanzania na The Hague, Uholanzi.

Kitengo cha mshataka nchini Rwanda kimepongeza kukamatwa kwa Bw. Kabuga katika Twitter yake, ikiongeza kuwa "Rwanda itaendelea kushirikiana na mahakama maalum ya ya umoja wa mataifa kuhakikisha haki ina inatolewa".

Mwendeshaji mkuu wa mashtaka wa kitengo cha mahakama ya Umoja Wa mataifa kwa ajili ya Rwanda-'International Residual Mechanism for Criminal Tribunals' (IRMCT) mjini Hague - mahakama inayosikiliza kesi za uhalifu wa vita za Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia - alisema polisi wa Ufaransa walimkamata bwana Kabuga siku ya Jumamosi, baada ya matokeo ya operesheni ya pamoja ya uchunguzi wa muda.

"Kukamatwa kwa bwana Félicien Kabuga leo hii inatukumbusha wale ambao walihusika katika mauaji ya kimbari kuwa wanapaswa kuwajibishwa hata kama ni baada ya miaka 26 baava ya uhalifu waliotenda," Serge Brammertz alisema katika taarifa yake.

"Katika sheria za kimataifa, kukamatwa kwa Kabuga kunaonyesha kuwa tunaweza kufanikiwa kama tunakuwa na msaada ya kimataifa kukabiliana na hilo," aliongeza.

Bwana Brammertz ameelezea shukrani zake kwa Ufaransa , lakini alisema hatua hii imefikiwa kwa mchango uliotolewa na Rwanda, Ubelgiji , Uimngereza, Ujerumani, Netherland, Austria, Luxembourg, Switzerland, Marekani, Europol pamoja na Interpol.

Kufuatia taratibu ambazo ziko chini ya sheria ya Ufaransa, hukumu ya bwana Kabuga inatarajiwa kuhamishwa kwenda kitengo cha mahakama ya Umoja Wa mataifa kwa ajili ya Rwanda IRMCT, eneo ambalo kesi yake itasikilizwa.

Mwaka 1997, Bwana Kabuga alitajwa katika mahakama ya kimbari mara saba , kuhusika na mauaji ya kimbari , kwa kusuka mipango, kuua, kutishia kuua wakati wa kimbari.

Marekani ilisema bwana Kabuga alikuwa miongoni mwa waasisi na mwenyekiti wa chama cha Fonds de Défense Nationale (FDN), ingawa anadaiwa kutoa ufadhili kwa serikali ya Rwanda katika utekelezaji wa mauaji ya kimbari mwaka 1994 .

Alidaiwa pia kutoa msaada wa vifaa kwa wanamgambo waliofanya mauaji hayo kwa kuwapa silaha na sare na kuwapatia usafiri.