Virusi vya corona: Shule nchini Uganda kuendelea kufungwa kwa mwezi mmoja zaidi

Chanzo cha picha, State House Uganda/Twitter
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa Shule, makanisa, misikiti, vilabu, vilabu vya usiku, maeneo ya kufanyia mazoezi na saluni za urembo zitaendelea kufungwa ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Museveni amesema kuwa si rahisi kwa maeneo hayo kufuata masharti ya kutochangamana.
Amri ya kutotembea usiku
Rais Museveni pia amesema muda wa kuwa ndani ya nyumba utaendelea kuwa kuanzia saa moja usiku mpaka saa kumi na mbili kamili asubuhi kwa siku 21 zaidi.
Makanisa, vilabu vya pombe, vilabu vya usiku , maeneo ya kufanya mazoezi na sauna yataendelea kufungwa kwa siku 21, huku kufungua shule kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani kukiwa kumeahirishwa wakisubiri kwa mwezi mmoja.
''Tumeamua kuahirisha kufunguliwa kwa shule kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani kwa mwezi mmoja zaidi tukijiandaa zaidi na kutazama hali ilivyo''.Alisema
Kulegezwa kwa masharti ya usafiri
Siku ya Alhamisi usafiri wa Umma utaanza tena nchini Uganda lakini kwa masharti.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Wenye magari ya dalala wamemaliza miezi miwili na nusu bila kazi tangu marufuku ilipowekwa mwezi Machi.
'Kuanzia tarehe nne nitaruhusu kuanza tena kwa usafiri wa Umma wa mabasi , usafiri wa abiria wa treni na dalala kuchukua abiria idadi ya nusu''. Alisema Rais Museveni.
Viwanja vya ndege vitaendelea kufungwa pia magari binafsi hayataruhusiwa kufanya kazi katika maeneo ya mpakani
Viongozi wa dini mwishoni mwa Juma lililopita waliomba nyumba za ibada baada ya kuchukua hatua ya kufungua masoko , kilio ambacho hakijasikilizwa na kiongozi huyo akiwataka waumini waendelee kusali kwa njia za televisheni wakiwa katika nyumba zao.

Taarifa zaidi kuhusu virusi vya corona:

Hatua zilizochukuliwa na Uganda kuzuwia maambukizi ya corona
Mwezi Machi Rais Museveni alitangaza kufunga taasisi za elimu, mikusanyiko nchini Uganda
Museveni alizuwia raia wa Uganda kusafiri kuelekea kwenye nchi zilizo na maambukizi ya virusi vya corona.

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Uganda wanaowasili kutoka nje wanatakiwa kujiweka karantini kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe.
Museveni aliamuru kufungwa kwa shule za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu kuanzia Ijumaa tarehe 20 mwezi Machi, kwa muda wa mwezi mmoja, lakini sasa muda huo umeongezwa.
Nyumba zote za ibada zimeamriwa kuahirisha mikusanyiko.
Mikusanyiko ya umma ikiwemo mikutano, mikutano ya kuhusu uchaguzi, mikutano ya kawaida, ya kitamaduni pia imepigwa marufuku.
Wakati huo huo rais Museveni pia mwezi huu alitangaza kuwa itakua ni 'uendawazimu' kuendesha uchaguzi wakati wa mlipuko wa virusi vya corona.
Aliliambia shirika la habari la Uganda NBS kwamba mipango ya kufanya uchaguzi mapema mwaka 2021 haitakuepo kama virusi vya corona havitadhibitiwa itatakiwa kuangaliwa upya.
Mikutano ya umma mkiwemo ya kisiasa imepigwa marufuku kama sehemu ya hatua za kutosogeleana na kukaa nyumbani zilizowekwa nchini humo kwa ajili ya kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona.

Takriban wagombea 24 wametangaza nia yao ya kugombea kiti cha urais na wamewasilisha maombi yao kwa Tume ya Uchaguzi ili kukabiliana na rais Museveni na wameanza mikutano ya kitaifa.
Mikutano hii imeahirishwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Kauli za Bwana Museveni sasa ziliibua swali juu ya ikiwa mchakato mzima wa uchaguzi utaahirishwa au la.
Unaweza pia kutazama:













