Umefika wakati mwili wa binadamu uteketezwe badala ya kuzikwa kaburini?

    • Author, Na Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC News Swahili

Kuuchoma mwili wa binadamu baada kifo limekuwa ni jambo la kawaida kwa miaka mwingi miongoni mwa jamii za India na Nepal ambapo mchakato huu umekua ukifanyika mahala palipo wazi na utamaduni wa tangu enzi za kale . Kuanzia karne ya 19 , uchomaji wa maiti ulianza kutekelezwa katika maeneo mengine ya dunia .

Hata hivyo katika nyakati hizi , mchakato wa kuchoma maiti umekuwa ukifanyika kwenye matanuru au mahala pa faragha palipofungwa palipotengwa maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu idadi ya wa maeneo ya Afrika mashariki ambao wamechaguwa kuchomwa kwa miili yao kama njia ya kuihifadhi miili yao baada ya kifo badala ya njia ya kawaida ya kuzikwa kaburini.

Katika miezi ya hivi karibuni, kumeibua hisia tofauti katika eneo la Afrika Mashariki hususan nchini Kenya kuhusu kuchomwa kwa maiti baada ya mtu kufariki.

Wale wanaounga mkono uteketezwaji wa maiti wanasema mfumo huo wa mazishi ni wa kisasa na unapunguza gharama ikilinganishwa na maiti inapozikwa.

Kwa upande mwingine, wanaopinga wanadai kwamba utamaduni wa kuteketeza maiti ni wa kigeni unaoenda kinyume na mila na desturi za Kiafrika.

Chimbuko la mjadala huu ni kuteketezwa kwa miili ya watu mashuhuri ; aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi Safaricom, Robert "Bob" Collymore, na mbunge wa upinzani Ken Okoth.

Wakenya wengine mashuhuri ambao miili yao ilitekekezwa kwa moto ni aliyekuwa mshindi wa tuzo ya Nobel na mwana mazingira Profesa Wangari Mathaialiyefariki mwaka wa 2011 na aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenneth Matiba.

Mwili wa aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana nchini Kenya pia ulichomwa mwaka wa 2005.

Je mchakato wa kuuchoma mwili ni upi?

Kuna aina mbili za kuuchoma mwili wa binadamu, kulingana na Bwana Patel, afisa katika kituo cha kuchoma miili cha kariokor mjini Nairobi Kenya. ''Mwili ukifika hapa kwenye kituo chetu ndugu huchagua ni vipi mwili utachomwa, tuko na mashine na tuna kuni mnachagua kulingana na utashi wenu'', ameiambia BBC Bwana Harish Patel.

Kuchoma mwili kwa njia ya mafuta ya dizeli:

Kulinganza na Bwana Patel kuna mashine maalum zinazoweza kulinganishwa na tanuru ambapo mwili huingizwa ndani na kuchomwa kwa muda wa saa tatu hadi utakapoteketea kabisa na kuwa jivu. ''Tunauingiza mwili ndani ya mashine na kuchomea mwili ukiwa ndani ya jeneza kama ulivyoletwa hatubadilishi kitu. Mtu mmoja wa familia huchaguliwa ili awashe umeme anawasha na kisha tunasubiri mpaka saa tatu ziishe ili mwili uwe umeungua kabisa''.

Baada ya saa tatu mifupa ya marehemu huwa bado haijaungua ndani ya mashine hiyo na mifupa huondolewa kwenye mashine ya kuchoma mwili na kuwekwa kwenye mashine nyingine maalumu inayofanya kazi ya kusaga mifupa ya marehemu na kuifanya kuwa majivu, anasema Bwana Patel.

Kuchoma mwili kwa njia ya kuni:

Katika mchakato wa uchomaji wa mwili wa binadamu kwa njia ya kuni, mwili huwekwa kwenye kifaa cha chuma kilichotengenezwa mithili ya kichanja cha kuanika vyombo kisha rundo la kuni hupangwa juu na chini ya mwili, na kisha mwili hupakwa mafuta ya siagi na ufuta ili kuwezesha joto la moto kuuteketeza mwili kwa haraka.

Kulingana na Bwana Harish Patel gharama ya kuuchoma mwili wa binadamu iwe kwa njia ya dizeli au kuni ni dola 400 za kimarekani.

Historia fupi ya kuchomwa maiti:

  • Kuteketeza maiti kama sehemu ya mfumo wa mazishi kumefanyika tangu jadi zaidi ya miaka 10,000 iliyopita.
  • Nchini China miili imekuwa ikiteketeza kuanzia miaka 8000BC yaani -kabla kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
  • Huko Ugiriki, uteketezaji maiti umekuwa ukifanyika tangu mwaka 480BC na nchini Sweeden desturi hiyo imekuwepo tangu jadi na kukomesha yapata miaka 1,000 iliyopita baada ya dini ya Ukristo kuingia huko.
  • Baada ya injili ya Kristo kuenezwa barani Ulaya, desturi hiyo ilififia kwani Wakristo waliitaja kuwa kinyume na maadili ya dini.
  • Utamaduni wa kuteketeza maiti ni maarufu katika jamii ya Wahindi ingawaje katika sehemu nyingine za ulimwengu hasa Ulaya na Marekeni desturi hiyo inaendelezwa kutokana na gharama ya chini.
  • Hadi miaka ya 1900, Kanisa Katoliki lilijitokeza na kupinga desturi hiyo.
  • Mfumo wa kisasa wa kuteketeza maiti ulianza miaka ya 1800 baada ya kuvumbuliwa kwa tanuri ya kisasa na moto na Professor Brunetti, aliyeiwasilisha katika maonyesho makubwa ya Elimu na Utamaduni mjini Vianna, Austria mwaka 1873.
  • Leo hii uteketezaji wa maiti unafanyika katika maataifa 31 ulimwenguni ambapo zaidi ya asilimia 75 ya wafu nchini Uswizi huteketezwa.
  • Dini ambazo zimekubali desturi hiyo ni Hindu, Jain na Sikh huku Wakristo na Waislam wakiipinga.
  • Katika eneo la Afrika mashariki, Kenya inaonekana kuegemea sana utamaduni huu wa uchomaji maiti.
  • Kuna takriban vituo 18 vya tanuru za uteketezaji maiti.
  • Nchini Tanzania na Uganda, utamaduni huu wa kuteketeza maiti bado unachukuliwa kama desturi ya kigeni na wengi katika mataifa haya huzika maiti kwenye makaburi.