Musiba vs wastaafu ni filimbi ya uchaguzi 2020 na kielelezo cha mtafaruku CCM?

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Barua iliyoandikwa na makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama tawala CCM, Kanali Abdulrahman Kinana na Luteni Yusuf Makamba imetanabahisha kuwa hali ya mambo si shwari ndani ya chama hicho.

Malalamiko ya viongozi hao wastaafu hadharani ambao mara kadhaa wametuhumiwa kuwa wanamhujumu Rais Dkt. John Magufuli pasipo kuwasilishwa ushahidi wowote wala kueleza umma mbinu zinazotumika, yanaweza kutafsiriwa kuwa imeshindikana kupatikana usuluhishi ndani ya CCM na serikali yake hivyo kufahamisha umma mfarakano unaoendelea kwenye chama hicho.

Aidha, Kinana na Makamba wameelezwa kulifikisha sakata hilo mbele ya Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi wakuu wastaafu, Pius Msekwa na Mwenyekiti wake Rais Ali Hassan Mwinyi ambaye aliongoza serikali ya awamu ya pili nchini Tanzania (1985-1995).

Kinana na Makamba ni watu wazito kwenye siasa na uongozi nchini Tanzania kwa ujumla wake.

Yusufu Makamba amekuwa Katibu mkuu wa CCM kati ya mwaka 2007 hadi 2011 ambapo alipokea kijiti kutoka kwa Philip Mangula.

Kwa upande wake Kanali Kinana alipokea wadhifa wa ukatibu mkuu mnamo mwaka 2012 hadi 2018 kutoka kwa Wilson Mukama aliyehudumu nafasi hiyo kati ya mwaka 2011-2012. Pia amepata kuhudumu kama Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.

Malalamiko yenye majibu

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na viongozi hao, aya ya pili inathibitisha hali si shwari ndani ya CCM. "Tumetafakari kwa kina kabla ya kuamua kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na uzushi alioutoa Cyprian Musiba dhidi yetu katika nyakati mbili tofauti," inasema sehemu ya barua hiyo.

Tafsiri inayopatikana hapa ni kwamba kisiasa viongozi hawa wawili hawakutaka suala hilo liishie kwenye vikao vya ndani ya chama.

Pili, Kinana na Makamba wameonyesha kufahamu kinachoendelea na nani anamtuma mwanaharakati huyo kuwatuhumu viongozi wastaafu kuwa wana nia ya kuhujumu serikali. Kuthibitisha hilo, katika aya ya pili ya barua yao wanaeleza kuamini mtu anayewatuhumu amefanya hivyo kwa kutumwa kutekeleza maagizo kama kipaza sauti.

"Yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu." Sentensi hii peke inadhihirisha kuwa viongozi hawa wastaafu wana mengi mioyoni mwao ama wamechoshwa kukaa nayo pamoja na kuendelea kuvumilia kuchafuliwa na kuvunjiwa heshima kama walivyosema. Kwamba yupo mtu au kundi la watu ambao linamtumia mwanaharakati huyo kuwatuhumu viongozi wastaafu. Mantiki inatuelekeza kuwa Kinana na Makamba wanazo taarifa juu ya 'mtu' aliyeko nyuma ya harakati za zinazorushwa kwao, hivyo badala ya kuzitamka mwenyewe ameamua kutumia "wakala".

Eneo hili ndilo linaibua mtafaruku wa kisiasa kati ya makundi mawili; 'kipaza sauti' na wastaafu ambao wanasikitishwa kuvunjiwa heshima. Wastaafu hawa wanaelekea wamemsaka mtu huyo hivyo nia yao ni kutaka atoke huko gizani na aje hadharani kuonyesha uhalisi wake.

Tafsiri tunayopata katika eneo hili ni mtafaruku mkubwa baina ya kambi mbili, pamoja na kuibuka na kundi ambalo litakuwa linawatetea wastaafu kutokana na heshima pamoja na urithi wao waliouacha kwa vijana kisiasa na uongozi ndani ya CCM na serikalini.

Baraza la ushauri linaundwa na akina nani?

Baraza hili liliundwa na mwenyekiti mstaafu wa CCM Jakaya Kikwete kama njia rasmi ya kuendelea kuwatumia viongozi wastaafu kwenye shughuli za chama, kwa kufanya mashauriano na wale wanaokuwa madarakani.

Baraza hilo linaundwa na viongozi waandamizi wastaafu, wakiwa chini ya Katibu Mkuu, Pius Msekwa.

Msekwa amewahi kuwa Katibu mkuu wa CCM, Spika wa Bunge na nyadhifa nyingine mbalimbali.

Mwenyekiti wa baraza hilo,ni rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Wajumbe wao ni pamoja na rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, raismstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na viongozi mbalimbali wakuu wa CCM na serikali.

'Vita' ya makundi CCM

Kama alivyowahi kusema mwanafalsafa wa kale wa Urumi, Marcus Tullius Cicero, "mtu mwerevu huelekea kutoa uamuzi wa kuzingatia mantiki,".

Hicho ndicho kilichofanywa na Kinana na Yusufu Makamba, ambao walikuwa chini ya utawala wa awamu ya nne ya rais na mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete.

Duru za kisiasa zinaeleza kuna makundi mawili, la kuwatetea makatibu hao wa Kikwete dhidi ya kundi jipya la kiongozi wa sasa wa nchi na CCM.

Makundi hayo mawili yatakuwa na kazi ya kulinda urithi mzuri wa viongozi wastaafu wakati lingine litakuwa na wajibu wa kulinda masilahi ya mwenyekiti wa sasa wa CCM na kuliambia lile la kwanza muda wao wa kuwa madarakani umepita.

Kuibuka kwa 'vita' ya makundi imethibitishwa na taarifa ya Kinana na Makamba katika aya ya 14 inayosema, "Sisi tumeamua kutokwenda Mahakamani, walau kwa sasa, kwasababu mbili; kwanza, jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwahiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa. Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia. Kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia."

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu Sokoine, amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa: "Ni dhahiri katibu mkuu wa sasa anafuga matatizo, rekodi zinaonyesha amekemea karibu kila kitu isipokuwa hatua za mwanaharakati huyu anayewatuhumu viongozi wastaafu kwa mambo mbalimbali. Mwaka 2020, kwa mazingira ya sasa ya makundi kati ya CCM ya zamani na CCM ya sasa, naamini kunaweza kutokea mtafaruku mkubwa ndani ya chama hasa kama hawa wastaafu wanahusika hivi wanavyotuhumiwa na wakapata kuungwa mkono na majeruhi wengine,".

Viongozi wastaafu wamepuuzwa?

Kwa sasa kuna kesi inayoendelea kuunguruma mahakamani iliiyofunguliwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje, Bernard Membe dhidi ya 'mwanaharakati' yule yule anayelalamikiwa na Kinana na Makamba.

Membe ametuhumiwa kumhujumu Rais, pia Katibu Mkuu wa CCM, Dk.Bashiru Ali alimtuhumu waziri huyo wa zamani kuwa na nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao 2020 kupitia CCM. Membe mwenyewe hajatamka nia hiyo.

Katika aya ya 6 katika taarifa hiyo, viongozi hao wamesema, "Tuliamini kabisa kwamba, pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu, na huku mtu huyo akajinasibisha na serikali pamoja na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma,"

Wanaongeza katika aya 7 kwa kusema, "Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawakuchukua hatua zozote kuhusu jambo hili. Na zaidi, mtu huyu ameendelea kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wastaafu na watu wengine wengi katika jamii,"

Je, wanaweza 'kumhujumu' Rais Magufuli?

Mwezi Oktoba mwaka 2020 Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani.

Tuhuma kubwa zinazoelekezwa kwa Kinana, Makamba, Membe, watendaji wa serikali na watu binafsi zimekuwa zikitolewa na mwanaharakati huyo kuwa wana mipango ya kumhujumu Rais kwenye uchaguzi mwakani na kukwamisha juudi zake za maendeleo. Je,ni kweli watu wasio na madaraka au mamlaka yoyote ndani ya nchi wanaweza kumhujumu rais?

Majibu ya swali hilo yanapatikana katika sentensi mbili zilizomo kwenye aya ya tano; "Na pili haiingii akilini kwamba wastaafu wawili walio majumbani kwao eti wana uwezo wa kumzuia Rais, Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa Chama kutekeleza majukumu yake,"

Aya ya sita inaeleza, "Tumesimamia michakato ya kupitisha wagombea katika nafasi ya Urais na nafasi nyinginezo". Hizi ni kauli kutoka kwa mabingwa wa mikakati ya kisiasa na uchaguzi waliohudumu chama tawala. Kwamba wanafahamu mbinu, rafu, mikakati na mipango ya kuweza kushinda uchaguzi. Lakini pia wanakiri kukosa nguvu za kuzuia uamuzi, mipango na mamlaka ya Rais wa Tanzania, hivyo uwezo wa kumzuia asigombee urais muhula wa pili mwaka 2020 ni mdogo.

Kwa kipindi chote ambacho mwanaharakati huyo amekuwa akiwatuhumu viongozi na watu binafsi mbalimbali ambao lilionekana kama vile ni jambo la mzaha. Majeruhi wa matamshi ya mwanaharakati huyo ni wengi kuanzia ndani ya nchi na nje.

Hatua iliyochukuliwa sasa inaonyesha kuwa Kanali Kinana na Makamba wamefanya hivi baada ya kuguswa na tuhuma za mwanaharakati huyo. Kwamba kama viongozi walipaswa kukemea kwa nguvu ili kuepusha matatizo kuota mizizi.

Mwanaharakati na mtia nia ya ubunge Jimbo la Moshi Vijijini mwaka 2015 ndani ya chama kikuu cha upinzani Chadema, Godlisten Malisa amemwambia mwandishi wa makala haya, "Naamini wazee wapo sahihi ila wamechelewa sana. Musiba alipaswa kukemewa mapema kuliko sasa. Viongozi hawa wamemuacha akaota mizizi ndio wanamkemea, jambo ambalo haliweza kuwa tija sana. Pengine hawakukemea mapema kwa sababu walikuwa hawajaguswa...Lakini kwa sasa waraka wao hauwezi kumshtua Musiba wala wanaomtumia. Kinyago walichokichonga wenyewe, sasa kimeanza kuwatisha,".

*Makala haya ni mawazo binafsi ya mchambuzi na si msimamo wa BBC.