Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tyson Fury v Dillian Whyte: Mfalme wa Gypsy ahifadhi taji la WBC huko Wembley na kuapa kustaafu
Bingwa wa ndondi wa uzani wa juu na mshikilizi wa ukanda wa WBC Tyson Fury amethibitisha angali moto wa kuotewa mbali baada ya kumdondosha sakafuni Muingereza mwenzake Dillian Whyte katika raundi ya sita ya pigano lililoshuhudiwa na mashabiki 94,000 katika ukumbi wa Wembley.
Fury alitawala pambano hilo akichanganya makonde mazito ya kushoto kulia kisha akaachia 'uppercut' ya kulia.
Whyte, kwa kustaajabisha, alisimama huku refa akiendelea kuhesabu ila akapepesuka na kumwangukia mwamuzi ambaye bila kupoteza wakati alisitisha pambano hilo ilikumuokoa kutokana na kipigo hicho kikali.
"Hili linaweza kuwa pambano la mwisho la Mfalme wa Gypsy," Fury alisema baada ya pigano hilo.
Baadaye aliongeza: "Nimetumia muda mwingi katika ulimwengu wa ndondi. Nimekuwa mbali na familia yangu kwa muda mrefu. Nilitimiza kila kitu nilichotamani kutimiza.
"Nitastaafu nikiwa mchezaji wa pili pekee duniani wa uzani wa juu katika historia, baada ya Rocky Marciano, kustaafu bila kushindwa. Sikuwahi kushindwa katika mchezo huu."
Fury - ambaye pia alihifadhi mkanda wake wa Ring Magazine - hajashindwa katika mapambano 33, huku Whyte - akipoteza kwa mara ya tatu katika mapambano 31. Aidha kutokana na kichapo hicho sasa jaribio lake la kwanza la ubingwa wa dunia pia limetibuka.
Ikiwa Fury ataamua kustaafu, bondia huyo mwenye miaka 33-atakosa fursa ya kupigania taji la bondia wa uzani wa heavy atakayeunganisha mikanda yote tatu ya ndondi duniani - pambano ambalo huenda likapangwa baadaye mwaka huu - na nafasi ya kuimarisha hadhi yake kama mchezaji mkubwa zaidi wa uzani ya juu zaidi wa Uingereza.
"Nilimuahidi mke wangu kwamba itakuwa hivyo baada ya pambano la [Deontay] Wilder," aliongeza. "Lakini nilipewa ofa ya kupigana Wembley na nilikuwa na deni kwa mashabiki wangu. Hii ni njia nzuri sana ya kustaafu."
Mke wa Fury, Paris aliiambia BT Sport: "Ningependa astaafu, Hana cha ziada kuthibitisha. Ikiwa angekuwa na chochote cha kufanya, ningesema 'Namn Tyson, fanya hivyo'. Lakini hana chochote cha kuthibitisha.
"Tyson ataendelea na ndondi, kwa sababu moja tu na najua moyoni mwangu, nadhani sababu pekee ambayo Tyson atarudi ulingoni ni kwa ajili ya pambano la kuunganisha mikanda."
Fury, kama ilivyotarajiwa, alichukua kipaza sauti na kuwatumbuiza mashabiki kwa uimbaji wake wa 'American Pie' ulingoni kufuatia ushindi wake.
Ulikuwa wimbo wa kumalizia karamu ya kurudi nyumbani kwa mpiganaji huyo anayeishi Morecambe, ambaye alikuwa anapiga ndondi nchini Uingereza kwa mara ya kwanza tangu 2018.
Kabla ya pambano hilo alisema litakuwa mwisho. Akimaanisha kwamba amefikia kilele chake ndondi huko Wemble .
Lakini wengi walitilia shaka tamko hilo - kwa sababu ni jambo ambalo alishawahi kusema mara kadhaa hapo awali - lakini mara hii inaonekana Fury huenda akatimiza ahadi.
Mtani wake Anthony Joshua huenda akarudiana na bingwa wa WBA wa Ukraine wa WBA, IBF na WBO Oleksandr Usyk msimu huu wa joto.
Ushawishi wa kupigania mshindi wa mikanda yote - na faida itakayotokana na pambano hilo itakuwa kubwa, haswa ikiwa Joshua ataibuka mshindi - anaweza kumshawishi Fury kusitisha mipango yake ya kustaafu.
Pambano hilo lililosadikiwa kuwa kubwa zaidi la uzani wa juu katika historia lilihudhuriwa na mashabiki takriban 94,000.
Mbali na miezi michache baada ya kushindwa kwake na Alexander Povetkin mnamo 2020, ambayo alilipiza kisasi, Whyte mwenye umri wa miaka 34 alikuwa mpinzani wa lazima wa mkanda wa WBC tangu 2017.
"Dillian ni shujaa na ninaamini atakuwa bingwa wa dunia," Fury alisema huku akimkumbatia Whyte baada ya pambano.
"Mmoja wa wakubwa na, kwa bahati mbaya, ilibidi apigane nami usiku wa leo. Hukupigana na mtu hivi hivi bali ulipambana na mtu bora zaidi duniani."
Tangu aliposhindwa kwa mara ya kwanza na mpinzani wake Joshua mwaka wa 2015, Whyte amethibitisha sifa zake za kiwango cha dunia kwa kushinda mastaa kama Joseph Parker na Povetkin.