Mfahamu aliyegundua ‘kisanduku cheusi’ cha ndege, kinachookoa mamilioni ya maisha ya watu duniani

Kifaa kinachorekodi mwenendo na taarifa za ndege kinajulikana kama "kisanduku cheusi". Inapotokea ajali taarifa za ndege na taarifa za sauti zilizorekodiwa katika kisanduku hiki cheusi husaidia kutoa ushahidi wa kina na sahihi kwa wataalamu wa anga kuchambua sababu ya ajali.

Hii ndio sababu wakati wowote ndege inapoanguka kwa bahati mbaya, wachunguzi wanajaribu kadiri ya uwezo wao kukipata kwanza kisanduku cheusi.

Uchambuzi wa data wa kutoka kisanduku cheusi ili kujua hatari za usalama umefanya usalama wa ndege za kisasa kuendelea kuboreshwa, na usafiri wa anga umekuwa njia salama zaidi ya usafirishaji katika nyakati za kisasa.

Kwa hivyo, "kisanduku cheusi" kinaweza kuokoa maisha yako. Lakini unajua nani aliyevumbua kisanduku hiki cheusi?

Ilianzia kwenye ajali ya ndege.

Ijumaa ya Oktoba 19, 1934, ndege ya abiria iliyopewa jina la Miss Hobart ilianguka baharini kutoka angani. Wanaume nane, wanawake watatu na mtoto mmoja wa kiume walianguka pamoja na ndege hiyo wanaaminika walizama majini baada ya kuanguka katikati ya tasmania na Australia.

Mabaki ya ndege hiyo hayajawahi kupatikana. Mmoja wa abiria alikuwa Mmisionari mwenye umri wa miaka 33, mchungaji Hubert Warren, ambaye alikuwa njiani kuelekea kwenye Parokia mpya ya Enfield, Sydney.

Mkewe Ellie na watoto wake wanne walibaki nyuma, wakikusudia kumfuata kwa mashua. Zawadi ya mwisho ambayo kuhani huyo alimpa mwanawe wa miaka minane, David, ilikuwa redio ya kioo ambayo David aliitunza.

David Warren, aliyekuwa anasoma katika shule ya bweni ya wavulana ya huko Launceston, Tasmania, aliifungua fungua redio baada ya kutoka darasani kutaka kujua inavyofanya kazi. Pia alikuwa akiwatoza kiasi kidogo cha fedha marafiki zake ili kusikiliza matangazo ya mechi za kriketi.

David, alikuwa kijana mcheshi na anayezungumza kwa ushawishi. Familia yake ilikuwa ya kidini sana na ilitamani awe mhubiri injili.

Lakini hilo halikuwezekana. Zawadi ya heshima ya radio alioachiwa na baba yake Hubert ilichochea shauku yake kwenye sayansi. Na yaliyofuata baadaye yalionekana kuwa ya umuhimu mkubwa kwa kuokoa maisha duniani.

Akiwa katika umri wa miaka 20s, David Warren alikuwa anasoma shahada ya sayansi ya Chuo Kikuu cha Sydney, na shahada ya uzamivu( PhD) ya Kemia katika chuo cha Imperial College London. Alikuwa mtaalamu katika sayansi ngumu 'rocket science' na baadaye alifanya kazi kama mtafiti katika maabara ya ARL, chini ya Wizara ya Ulinzi ya Australia, iliyolenga katika utafiti wa ndege.

Mwaka 1953, David aliyetoka kutunukiwa shahada yake ya Uzamivu alihamishwa na wizara hiyo kupekekwa kwenye kikosi kazi maalumu. Kikosi kazi hicho kilipewa jukumu la kufuatilia kwanini ndege za "halleland comet" zilikua zikipata ajali na kuanguka kila leo.

Karne moja na nusu iliyopita, sio ndege za Boeing zilizokuwa zikitamba kwenye soko la anga bali British Havilland Airlines kupitia ndege zake za British de Havilland Comet Jet. Ndege hizi zilikuwa zinaruka umbali mrefu kutoka Uingereza mpaka Australia, jambo ambalo kwa wakati huo hakuna mtu ambaye angeweza kufikiri.

Lakini zilikuwa zikipata ajali na kukatazwa kusafiri safari hizo, ambazo zilikuwa maarufu kitalii.

Kidokezo kwenye Kisanduku

Timu ya utafiti ilichunguza viashiria vya ajali, walijitahidi kwa akili zao lakini hawakuweza kufanya chochote. Siku moja, mmoja wa wajumbe wa timu hiyo alijisemea tu kuwa ajali ya hivi karibuni huenda ilitokana na kutekwa kwa ndege hiyo.

Aliyesema alisema tu, lakini aliyesikiliza akaweka moyoni. David Warren kwa sauti akasema: Vipi kama kulikuwa na kinasa sauti kwenye ndege kilichokuwa kinarekodi sauti kwenye ndege hiyo?

Hata kama kilikuwepo lakini uwezekano wa kupatikana ni mdogo kwa sababu ya ukubwa wa ajali na moto unajitokeza kuna uwezekano wa kwamba kimeungua. Lakini vipi kama kuna kinga ya moto na maji kwenye kinasa sauti hicho, labda wanaweza kusikia sauti ya rubani.

David alikuwa na shauku kufuatilia hilo, lakini wakubwa wake walionekana kutoona kama jambo la kulichukulia mkazo. Wakamwambia, kama anataka kufanya utafiti huo, afanye nje ya muda wa kazi na afanye watu wasijue.

Bw. Warren aliingia kwenye karakana ya familia iliyokuwa na makorokoro mengi ikiwemo radio aliyopewa na baba yake kama zawadi ya mwisho miaka 20 nyuma. Hapo ndipo 'Kisanduku cheusi' kinachotumika kwenye ndege leo kilipotengenezwa na kugunduliwa.

Siku moja mnamo mwaka 1958, mtu mmoja bila kualikwa alienda kwenye karakana ya kisayansi ya David. Mara tu alipoingia mlangoni, aliuliza Warren ni nani anataka kuona kifaa alichovumbua.

Aliwaonesha wageni mfano wa uvumbuzi wake: Sanduku la chuma ambalo linaweza kuhifadhi sauti na taarifa za ndege kwa saa 4. Kifaa kinachoweza kufuta chenyewe taarifa zilizorekodiwa nyuma na kurekodi mpya.

Hapo hapo mgeni huyo alimvuta mkono Warren na kumwambia mara moja apande ndege kutoka Australia hadi London.

Mtu huyu alikuwa sir Robert Hardingham, katibu mkuu wa Mamlaka ya Anga ya Uingereza.

'Kisanduku cheusi cha rangi ya chungwa'

Waingereza walivutiwa na uvumbuzi wa Warren. Kipindi cha Televisheni na Redio cha BBC kilimhoji Warren kuhusu uvumbuzi wake.

Mwaka 1958, toleo la kwanza la "kisanduku cheusi" kilianza kuzalishwa. Rangi yake haikuwa nyeusi, ilikuwa ya machungwa, na rangi hiyo imeendelea mpaka leo. Rangi hiyo ya machungwa inayong'aa iliwekwa makusudi ili kukitambua kisanduku hicho kirahisi baada ya kutokea kwa ajali ya ndege.

Kwa nini Sanduku la rangi ya machungwa linaitwa "Kisanduku cheusi au Black Box"?

Warren anakumbuka kwamba wanaopaswa kulaumiwa kwa hilo ni kuwalaumu waandishi wa BBC. Katika kutambulisha uvumbuzi wa Warren waandishi wa BBC walimhoji kwa kutumia kifaa cha kielektroniki kinachojulikana kama "kisanduku cheusi". Tangu wakati huo mpaka sasa jina "Kisanduku cheusi" likawa maarufu na kutumia kama jina la kawaida linalojulikana zaidi kifaa hicho cha kurekodi taarifa za ndege.

''Usifungue"

Mwaka 1960, baada ya ajali nyingine isiyojulikana katika eneo la Queensland iliyoua watu wote 29, Australia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuhitaji kifaa cha kurekodi sauti "kisanduku cheusi" katika ndege zake za abiria.

Leo "Kisanduku cheusi", ni imara hakiingizi maji, hakipati athari kubwa, kinarekodi taarifa zozote za sauti na ndege, na ni kifaa cha lazima kwa sasa kuwepo katika kila ndege duniani kote.

David Warren alikuwa akifanya kazi katika Idara ya ulinzi ya Australia hadi alipostaafu mwaka 1983, na nafasi yake ya mwisho alikuwa kama mtafiti mkuu. Alifariki dunia Julai 19, 2010 akiwa na umri wa miaka 85.

Ingawa alikuja kupata tuzo miaka 50 baadaye baada ya uvumbuzi wake huo, Warren hata hivyo hakuwahi kulipwa chochote kwa uvumbuzi huo wa kisanduku cheusi.

Alikuwa anapuuza jambo hilo, na wakati mmoja alitania kwamba ilikuwa vizuri kwamba Wizara ya Ulinzi ya Australia haikuwahi kumpa fedha, kwa sababu uvumbuzi wake mwingi haukufanikiwa, na serikali haikumlipa.

Kwenye jeneza lake wakati anazikwa, kwa mujibu wa maagizo yake wakati wa uhai wake, alitaka kuandikwe mstari wa onyo: "Mvumbuzi wa rekodi ya ndege: Usifungue."