Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je Christiano Ronaldo ndiye mchezaji bora kuwahi kutokea katika historia ya bara Ulaya
Wakati Cristiano Ronaldo atakapoiongoza Ureno kuivaa Hungary katika mechi yao ya ufunguzi ya fainali za Euro 2020 hapo June 15 mwaka huu, anatarajiwa kuandika rekodi mpya kwenye mashindano hayo.
Nyota huyo anayekipiga klabu ya Juventus ya Italia, mwenye miaka 36, na aliyesaidia timu yake ya taifa ya Ureno, kutwaa kombe la Euro mwaka 2016, ana kila sababu ya kutambulika kama mchezaji bora wa muda wote wa Michuano ya Euro.
Katika historia ya Michuano hiyo, Ronaldo amecheza michezo mingi kuliko mchezaji yoyote yule, amefunga mabao mengi kwenye hatua za kufuzu kuliko mchezaji yoyote, na endapo atafanikiwa kufunga bao moja tu kwenye fainali zinazoanza June 15 mwaka huu, basi atakuwa anaongoza kwa ufungaji wa mabao katika mashindano ya Euro.
Analinganishwaje na magwiji wengine Ulaya? Na je anatarajiwa kuweka rekodi gani mpya?
Ufungaji wa Mabao
Kwa sasa Ronaldo amefungana na Michel Platini kama vinara wa kufumania nyavu katika historia ya michuano hiyo ya Euro, akiwa na mabao tisa aliyopachika katika michezo 21 aliyoichezea Ureno kwenye fainali nne tofauti. Akiwa mchezaji pekee kufumania nyavu katika fainali nne tofauti za Euro.
Gwiji la Ufaransa Platini, akiwa nahodha alifunga mabao yake tisa katika michezo mitano tu aliyoichezea timu yake ya taifa ya Ufaransa (Les Bleus) katika fainali za Euro 1984, hakuwahi kucheza fainali zingine. Fainali za mwaka huo, zilikuwa fainali pekee ambazo Les Bleus ilishiriki kati ya mwaka 1960 na 1992.
Ronaldo alipachika mabao mawili katika fainali za mwaka 2004, moja katika fainali za mwaka 2008, na katika fainali za mwaka 2012 na 2016 - alipachika mabao matatu matatu, akiwa mchezaji pekee kufunga mabao matatu katika fainali za Euro mbili tofauti.
Rekodi nyingine ni kwamba, magoli yote tisa ameyafunga akiwa ndani ya boksi - huku matano yakiwa ya vichwa, ambayo pia ni rekodi.
Mabao sita ya Ronaldo kati ya hayo tisa yamepatikana katika hatua za makundi, moja akifunga kwenye robo fainali za Euro 2012 dhidi ya Czech Republic, mawili akifunga kwenye nusu dhidi ya Uholanzi mwaka 2004 na mawili mengine dhidi ya Wales mwaka 2016.
Kama atakuwa na michuano mizuri ya Euro mwaka huu, mfaransa Antoine Griezmann anaweza kuifikia na kuipiku rekodi hiyo ya mabao ya Ronaldo na Platini. Antoine Griezmann ana mabao 6 kwenye michuano hiyo, matatu nyuma ya Ronaldo na Platini, yote akiyafunga kwenye fainali za Euro 2016, alipoibuka mfungaji bora na kutwaa kiatu cha dhahabu.
Ronaldo pia anaongoza kwa mabao kwenye hatua ya kufuzu za michuano hiyo, ukiacha 9 aliyofunga kwenye fainali za michuano hiyo ya Euro, katika hatua ya kufuzu amepachika jumla ya mabao 31, ikiwa ni rekodi mpya akiivunja rekodi ya mabao 23 ya gwiji wa Ireland, Robbie Keane, ya September 2019.
Mafanikio
Ronaldo ametwaa kombe la Euro akiwa na Ureno kwenye fainali za mwaka 2016, wakati Ureno ilipoichapa Ufaransa kwenye mchezo wa fainali, - kitu ambacho mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi - hajawahi kushinda kombe kwenye michuano mikubwa akiwa na timu yake ya taifa ya Argentina.
Kwenye mchezo huyo wa fainali, Ronaldo alicheza kwa dakika 25 tu kutokana na majeraha , lakini wakati wote wa mchezo alisimama kusaidia kuwaelekeza wachezaji wenzake katika mchezo huo ambao Ureno ilishinda bao 1-0.
Ronaldo ni mmoja wa wachezaji 44 kuwahi kuchezaji fainali mbili katika michuano ya Euro - mwaka 2004 na 2016. Hakuna mchezaji aliyewahi kuchezaji fainali tatu. Lakini ni Ronaldo na Bastian Schweinsteiger wa ujerumani waliowahi kucheza nusu fainali tatu za michuano hiyo.
Kama atafanikiwa kutwaa ubingwa akiwa na Ureno katika fainali za mwaka huu, basi ataungana na Rainer Bonhof wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1972 and 1980) na nyota 12 wa timu ya taifa ya Hispania waliokuwa katika vikosi vya Euro 2008 na 2012 - kama wachezaji pekee kuwahi kushinda mara mbili kombe la Euro.
Ronaldo pia anaongoza kwa kushinda michezo mingi katika fainali za Euro akishinda michezo 11 akifungana na wahispania Cesc Fabregas na Andres Iniesta - kama Ureno atashinda mchezo mmoja katika fainali za mwaka huu, atawapiku wahispania hao.
Kudumu muda mrefu
Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji kadhaa waliowahi kucheza fainali nne za Euro. Fainali za mwaka huu zitafanya kuwa mchezaji pekee kushiriki fainali tano za michuano hiyo.
Amecheza jumla ya michezo 21 kwenye fainali hizo, michezo mitatu zaidi ya Mjerumani Schweinsteiger, na minne zaidi ya gwili la Italia Gianluigi Buffon. Ronaldo anaongoza zaidi kwa kucheza dakika nyingi za michuano hiyo, akicheza dakika (1,795).
Ni Kinara wa mambo gani mengine?
Ronaldo anaongoza kwa kupiga mashuti. Mreno huyo ameipiku rekodi iliyowekwa tangu mwaka 1980 kwa kupiga mashuti 122, kwenye michuano hiyo, akifuatiwa na gwiji la Ufaransa,Thierry Henry, mwenye mashuti 52.
Katika mashuti yaliyolenga lango, Ronaldo anaongoza pia kwa mashuti 32 - akifuatiwa na Henry na Dennis Bergkamp wenye mashuti 20. Gareth Bale ana mashuti 17 yaliyolenga lango kati ya 26 aliyopiga kwenye fainali za Euro 2016.
Mashuti ya Ronaldo yaliyogonga mwamba ni sita, ambayo ni mawili zaidi kuliko mchezaji yoyote tangu mwaka 1980.
Katika kipindi hicho pia cha tangu mwaka 1980, Ronaldo anafungana na wachezaji wengine wanaoshika nafasi ya pili kwa kutoa pasi za mwisho za magoli, wakiwemo David Beckham wa Uingereza na Karel Poborsky wa Czech Republic. Wote wametoa pasi sita za mabao. Iwapo katika michuano ya mwaka huu, Ronaldo atafanikiwa kutoa pasi moja tu ya bao, basi ataweka rekodi nyingine.
Katika fainali zote za Euro tangu mwaka 1980, Ronaldo anashika nafasi ya pili kwa 'dribo', 'akidribo' mara 83 nyumba ya mreno mwenzake Luis Figo. Lakini ni 'dribo' 31 tu zilizofanikiwa, na kumfanya nahodha huyo wa Ureno kushika nafasi ya 7 kwa 'dribo' zilizofanikiwa.
Mafanikio gani yaliyosalia kwa Ronaldo kwenye Euro?
Ronaldo anaweza kuvunja rekodi kadhaa kwenye mchuano ya Euro 2020. Anaweza kuwa mfungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo na kuwa mchezaji wa kwanza kushiriki fainali tano za Euro.
Anaweza kuwa miongoni mwa nyota wachache kushinda mataji mawili ya Euro na kuwa mchezaji wa kwanza kucheza mechi tatu za fainali za Euro. Na anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kucheza nusu fainali nne za michuano hiyo.
Akiwa na michuano mizuri, rekodi nyingine ambayo huenda akaiwaza ni ile ya mfungaji bora wa muda wote wa mabao kwa timu za taifa, inayoshikiliwa na Ali Daei wa Iran mwenye mabao 109. Kwa sasa Ronaldo yuko nyuma kwa mabao 6, akiwa na mabao 103 aliyoifungia timu yake ya taifa ya Ureno.
Matukio yakukumbukwa ya Ronaldo kwenye Euro
Portugal 2-1 Netherlands, ilikuwa nusu fainali ya Euro 2004 - Ronaldo aliifungia Ureno bao la kuongoza la kichwa na baadaye kutengeneza la pili na la ushindi lililopachikwa na Maniche.
Portugal 1-0 Czech Republic, Robo fainali ya Euro 2012 - Ronaldo alicheza soka la hali ya juu na kufanikiwa kumfunga kwa kichwa cha nguvu, mlida mlango, Petr Cech.
Portugal 3-3 Hungary, Mchezo wa hatua ya makundi Euro 2016 - Ronaldo alipachika mabao mawili likiwemo la kusawazisha la kichwa, na kuisaida Ureno ikitoka nyuma kukwepa kuondolewa mapema kwenye fainali hizo.
Portugal 1-0 France, Mcheo wa fainali Euro 2016 - Licha ya kwamba aliumia katikati ya kipindi cha kwanza na kutolewa nje, Ronaldo alijivika majukumu makubwa kuisaidia timu yake kuichapa Ufaransa na kutwaa kombe. Alikuwa akitoa malekezo katika muda wote wa mchezo.
Yapo pia matukio machache yenye doa yakukumbukwa
Greece 1-0 Portugal, Fainali za Euro 2004 - Ureno ilishindwa kweye mchezo wa fainali dhidi ya Ugiriki kwenye ardhi ya nyumbani, huku Ronaldo akipoteza nafasi ya wazi ya kuisawazishia Ureno.
Portugal 2-3 Germany, Robo fainali ya Euro 2008 - Miroslav Klose alifanikiwa kumzuga Ronaldo na kuipa uongozi wa mabao 2-0 Ujerumani, na kusababisha Ureno kuondolewa katika robo fainali hizo.
Portugal 0-0 Spain (2-4 pen), Nusu fainali za Euro 2012 - Ronaldo akiwa mpigaji wa penati ya tano, bahati mbaya, haikufika huko, Ureno ilichapwa kwa mikwaju ya penati 2-4 dhidi ya majirani zao Hispania.