Eliud Kipchoge ashinda taji la kila mwaka la BBC la mwanamichezo bora wa mwaka 2019

Taji la BBC ''Mwanamichezo Bora wa mwaka Duniani'' 2019

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, Taji la BBC ''Mwanamichezo Bora wa mwaka Duniani'' Jumapili 15 December, 2019

Mwanariadha Eliud Kipchoge amejishindia taji la BBC la kuwa ''Mwanamichezo Bora wa mwaka Duniani''.

Kipchoge alikuwa mtu wa kwanza katika historia ya mbio za Marathon kukimbia kilomita 42 kwa muda wa chini ya saa mbili Oktoba, 2019.

Raia huyo wa Kenya, 35, alikamilisha muda wa kilomita 42.2 katika saa moja dakika 59 na sekunde 40 katika shindano la Ineos Challenge mjini Vienna nchini Austria.

Miezi sita kaba ya ushindi wake, Kipchoge alikuwa ameshinda ubingwa wa London Marathon mara nne mfululizo.

Kipchoge, alipata medali ya dhahabu katika mbio za Marathon, Rio 2016, na kuvunja rekodi yake mwenyewe ya London aliyoiweka 2016, kwa sekunde 28.

Kupitia kura zilizopigwa kwa njia ya mtandao, Kipchoge amewashinda mwanariadha wa mazoezi ya viungo Simone Biles, nahodha wa timu ya taifa ya Raga ya Afrika Kusini Siya Kolisi, mchezaji Kriketi wa Australia Steve Smith, mchezaji gofu duniani Tiger Woods na mshambuliaji wa Marekani Megan Rapinoe, ambaye aliongoza tena timu yake katika mashindano ya Kombe la Dunia msimu wa joto uliopita.

Mshindi wa mwaka jana alikuwa mchezaji gofu Francesco Molinari, aliyeshinda mashindano ya Dunia 2018, pamoja na mashindano yote matano ya mechi za kombe la Ryder mjini Paris.

Pia inaweza kusoma: