Qatar 2022 : Tanzania yazuiliwa na Burundi mechi ya kufuzu kombe la dunia

Chanzo cha picha, FIFA TV/SCREENGRAB
Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars hii leo imeandikisha sare 1-1 na timu ya taifa ya Burundi Intamba Murugamba katika mechi za kufuzu kwa kombe la dunia nchini Qatar 2022.
Licha ya kutawala kipindi cha kwanza cha mchezo Tanzania ilishindwa kuona lango la wenyeji wao huku washambuliaji hodari Mbwana Samatta anayeichezea klabu ya Genk nchini Ubelgiji na Simon Msuva wakishindwa kuwika katika lango la Burundi.
Kipa wa Burundi Jonathan alikataa katakata kufungwa na wachezaji hao wawili kupitia uokoaji wa hali ya juu.
Udhaifu wa Burundi ulionekana katika utoaji pasi sawala lililopelekea kipindi cha kwanza kukamilika kwa sare tasa.
Burundi hatahivyo ilitawala kipindi cha pili cha mchezo mbele ya mashabiki wao baada ya kocha wake Olivier Niyungeko kufanya baadhi ya mabadiliko miongoni mwa wachezaji wake.
Mbwana Samatta alikosa bao la wazi akiwa amesalia na kipa wa Burundi aliyepangua shambulizi lake na kuisaidia pakubwa Intamba Murugamba.
Hatahivyo kunako dakika ya 81 ni Burundi ndio ilioanza kuona lango la wageni wao kupitia mchezaji Cedric Hamissi anayechezea soka yake nchini Tanzania ambaye alipokea pasi muruwa kutoka kwa Mohamed Amissiwari aliyeingia katia nafasi ya Bienvenue kanakimana.
Hatahivyo Tanzania waliimarisha mashambulizi yao kunako dakika hizo za lala salama na haikuchukua muda mrefu wakati Simon Msuva aliposawazisha dakika tatu baadaye.
Mechi ya marudio iutachezwa nchini Tanzania wikendi ijayo tarehe 8 mwezi Septemba.
Mshindi wa mechi hiyo atafuzu kwa raundi ya pili ya michuano hiyo.













