Neymar na Paris St-Germain: Je ipi hatma ya mchezaji ghali zaidi duniani?

Neymar anaonekana kuwa mtu aliyekata tamaa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Neymar alijiunga na PSG mwezi Agosti 2017 na ameshinda mataji mawili ya ligi ya daraja la kwanza na mabingwa hao wa Ufaransa

Ulikuwa uhamisho ambao ulimfanya Neymar kuondoka katika kivuli cha nyota wa Barcelona Lionel Messi.

Hatahivyo raia huyo wa Brazil amegonga vichwa vya habari kwa sababu tofauti tangu alipojinasua kutoka katika mabingwa hao wa Uhispania na kuelekea PSG.

Amefunga magoli 34 kati ya mechi 37 ili kuwasaidia kushinda taji la ligi ya daraja la kwanza.

Lakini pia amepigwa marufuku kutoshiriki mechi tatu kwa kumkaripia shabiki mmoja baada ya PSG kubanduliwa katika kombe la ligi ya Ufaransa, alidaiwa kushiriki katika kizazaa kilichotokea katika chumba cha maandalizi na wachezaji wenzake na atakaosa kushiriki katika mechi tatu za Yuropa kwa kuwatusi maafisa.

Na tayari amepokonywa unahodha wa timu ya taifa ya Brazil kabla kuanza kwa kombe la Copa America nchini Brazil.

Huku ikiwa hajamaliza hata miaka miwili tangu aliponunuliwa kwa dau la juu zaidi duniani la £200m , huenda huduma zake katika uwanja wa Parc des Princes zinakaribia kikomo.

''Sitaki kuchezea tena PSG nataka kurudi nyumbani kwangu, ambapo nisingeondoka'', alidaiwa kumwambia rais wa PSG Nasser Al-Khelaifi katika ujumbe , kulingana na gazeti la Uhispania la Mundo Deportivo.

Sasa ataelekea wapi? Barcelona? ama pengine aelekea kaika ligi ya Uingereza?

Akizungumza na BBC Radio 5 waandishi Tim Vickery , Miguel Delaney na Ben Haines wanazungumzia kuhusu hatma ya mchezaji huyo.

Je ni mchezaji aliyeharibika ama ni rahisi kumpenda?

Vickery: Wachezaji wakuu wa kikosi cha Barcelona wangefurahia sana kumkaribisha Neymar.

Yeye ana uhusiano mzuri na Messi, Suarez na Gerald Pique-Wachezaji watatu ambao ndio nguzo ya Barcelona na nadhani hilo linampatia fursa.

Sidhani kama kuna mchezaji ambaye alichukiwa zaidi ya Neymar na naweza kuelewa hilo.

Ni mchezaji ambaye anaponekana kana kwamba ameharibika lakini nadhani pia kuna upande mwengine wake mzuri.

Cha kushangaza ni kwamba wachezaji wenzake hususan katika klabu ya Barcelona na wale wa timu ya Brazil wamekuwa na uhusiano mzuri naye-wakimpenda sana.

Delaney: Nilikuwa nikizungumza na jamaa mmoja ambaye ametumia wakati wake mwingi na Neymar siku moja.

Walisema licha ya anavyochukuliwa , unapokutana naye moja kwa moja ana upande wake mzuri.

Ni mtu ambaye ni rahisi kumpenda na anaweza kukusaidia. lakini swala hapa ni vipi anachukuliwa kama mtoto na watu wake , akiwemo babake.

Hilo linaweza kutoa ubaya wake kama tulivyoona akiichezea PSG.

Vickery: Kuna uamuzi unaochukuliwa na watu wake wa karibu ambapo huwezi kujua iwapo ni yeye anayefanya uamuzi huo au la.

Lakini unashangaa iwapo uhusiano wake na babake anafaa kuupa kisogo ili kujisimamia. Ningependa kumuona akilivua joho la kuwa Neymar mdogo na badala yake kuwa mtu mzima.

Je uhamisho wake kuelekea PSG ulikuwa makosa makubwa?

Delaney: Sasa amegundua kwamba uhamisho wa kuelekea PSG ulikua makosa makubwa

Baada ya kuzungumza na watu wachache ambao wameshirikiana na Neymar ama watu wake wa karibu, kuna wasiwasi kuhusu kule ambako mchezo wake unaelekea.

Kuna madai mengi kwamba pia hafanyi mazoezi.

Kwamba amejishirikisha sana katika klabu ya PSG hadi kiwango cha mchezo wake kimeshuka.

Baadhi ya wale walio na wasiwasi zaidi wanasema kuwa kipindi chake cha mchezo kipo hatarini kuangamia. Nadhani hiyo ni mojawapo ya sababu ambazo anahitaji kuondoka katika mazingira hayo.

Vickery: Niko tayari kukosolewa lakini nadhani kulikuwa na lengo fulani katika uhamisho wa mchezaji huyo kuelekea PSG. Pengine lengo la kutaka kushinda taji la mchezaji bora duniani.

Wachezaji wengi wa Brazil walishinda taji hilo la Ballon d Or miaka ya nyuma . Je angelishinda vipi taji hilo wakati ambapo amekuwa akicheza chini ya kivuli cha Lionel Messi .

Nadhani alikuwa na lengo la kuelekea PSG ili kuwa kiongozi wa timu hiyo. Bahati mbaya ni kama kana kwamba kandarasi yake katika klabu hiyo haijaanza.

Alisajiliwa kwa kitu kimoja pekee. Kuisaidia timu hiyo kusonga mbele katika awamu ya kimakundi katika kombe la ligi ya mabingwa.

Kufikia sasa amecheza mara moja kutokana na majeraha swala ambalo sio kupenda kwake.

Neymar akisherehekea wakati alipokuwa Barcelona

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Neymar alishinda mataji mawili ya La Liga na moja la ligi ya mabingwa akiwa na Barcelona

Je anaelekea Uhispania ama wapi?

Vickery: Ana nafasi chache kuhusu ligi atakayojiunga nayo. Kwa sababu ni wapi anaweza kuelekea? Kitu ambacho hatujakitaja ni ligi ya Uingereza.

Ligi hiyo ni mojawapo ya ligi yenye ushindani mkali duniani na klabu zilizo na uwezo wa kumnunua-lakini je watahatarisha fedha zao?

Je umewahi kufikiria Neymar akijiunga na ligi ya Uingereza? Unaweza kufikiria ghadhabu atakazopata atakapojiangusha kama ilivyo kawaida yake?

Sasa Real Madrid wamempata Eden Hazard je watamuhijitaji Neymar pia?

Delaney: Sidhani. wamemnunua mchezaji Luca Jovic hivyobasi wametatua tatizo lao la safu ya mshambulizi.

Nadhani inaonekana kwamba Neymar alikuwa mchezaji wa pili ama wa tatu kwa ubora duniani katika kipindi cha miaka michache iliopita na Madrid hawana haja naye tena.

Nakumbuka kusikia mwaka mmoja uliopita vile rais wa Real Florentino Perez alivyokuwa akisaka saini ya mchezaji huyo na hilo limekwisha hali ya kwamba unaweza kumsikia Neymar pekee akilizungumzia badala ya mtu yeyote kutoka Madrid.

Meli imeondoka na sasa itategemea iwapo atarudi Barcelona kwa sasa.