AFCON 2019: Majirani DRC na Uganda kuminyana Jumamosi

Chanzo cha picha, Getty Images
Kipute cha Kombe la Afrika Mashariki na Kati kimewadia, na kuna mechi zinazokutanisha mataifa jirani ambazo ukali wake hauishii kwenye viwanja na wachezaji 22 wanaopambana.
Kipute cha kwanza cha namna hiyo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kitatokea siku ya Jumamosi, ambapo majirani Uganda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wataumana kwenye mchezo wa pili wa Kundi A.
Nani ataibuka mbabe wa mechi hiyo? Si rahisi kupata jibu kabla ya 90, lakini yawezekana takwimu zinaweza kusaidia kutatua fumbo hilo.
Uganda imekuwa na kiwango bora kwa siku za hivi karibuni kwa nchi za Afrika Mashariki.
Ilikuwa timu pekee iliyoshiriki michuano hiyo miaka miwili iliyopita kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hata Hivyo waliishia kwenye hatua ya makundi na kuambulia alama moja.
Kikosi cha Uganda kinaongozwa na nanodha na mlinda mlango Denis Onyango, anayecheza kandanda la kulipwa nchini Afrika Kusini na ni moja kati ya makipa bora barani Afrika kwa kizazi kilichopo.
Onyango pamoja na kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Sebastien Desabre wanaamini wanaweza kushinda mchezo huo.
"Yawezekana hatuna kiwango sawa lakini tunaweza kuwahimili uwanjani. Kushinda mchezo wetu wa kwanza litakuwa jambo kubwa sana kwetu. Mashindano yaliyopita yalikuwa magumu kwetu...lakini sasa tuna wachezaji wenye uzoefu," amesema Onyango.

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Lakini je, mawazo ya nahodha na kocha wa Uganda yana uhalisia kwa kiasi gani.
DRC ni moja ya miamba ya soka barani Afrika, washawahi kufuzu Kombe la Dunia na ni mambingwa mara mbili wa michuano ya bara la Afrika, mwaka 1968 na 1974.
Wakati Uganda ikiishia raundi ya kwanza AFCON 2017, DRC ilifika hatua ya robo fainali na kutolewa na Ghana baada ya kufungwa goli 2-1.
Miaka miwili nyuma, 2015, DRC ilimaliza mashindano ya AFCON katika nafasi ya tatu, walifanya hivyo pia mwaka 1998.
Hata kwa kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, DRC wamewaacha mbali Uganda.
Ni dhahiri kuwa, kiwango na historia vipo upande wa DRC dhidi ya Uganda.
Na endapo historia itajirudia, basi huenda DRC wakafika mbali kwenye mashindano haya.
Mara ya mwisho kuchukua kombe hilo mwaka 1974, DRC ilifanya hivyo nchini Misri, na mwaka huu mashindano yamerejea Misri.
Timu hizo zipo Kundi A, ambalo linaunda pia na wenyeji Misri na Zimbabwe.
Ni rahisi kutabiri kuwa Misri na DRC watamaliza kwenye nafasi mbili za juu.
Lakini mpira hudunda, na matokeo ya dakika 90 aghlabu hushangaza wengi.












