Arsenal 2-0 Chelsea: Maurizio Sarri anasema wachezaji wa The Blues 'hawashawishiki'

Mkufunzi wa Chelsea Maurizio Sarri ameelezea kuwa vigumu sana kuwashawishi wachezaji wake kufuatia kushindwa na Arsenal.

The Blue ilipoteza 2-0 katika ligi ya Uingereza siku ya Jumamosi katika uwanja wa Emirates na walikuwa na shambulizi moja pekee lililolenga lango.

Chelsea imeshinda mara mbili pekee katika mechi tano zilizopita na sasa wako pointi tatu pekee mbele ya Arsenal waliopo katika nafasi ya tano na Man United iliopo katika nafasi ya sita.

''Nimekasirika sana kuhusu mwelekeo tuliochukua'' , Sarri alisema. Ni mwelekeo ambao hatuwezi kukubali.

Katika mkutano na vyombo vya habari baada ya timu yake kulazwa, Sarri alisema alitaka kuzungumza kwa lugha ya Kitaliano badala ya Kiingereza kwa sababu alitaka kutuma ujumbe kwa wachezaji wake na alitaka kutuma ujumbe wa wazi.

''Nataka kusema nimekasirika sana, nimekasirika sana'', alisema mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 60, ambaye alimrithi raia mwenzake wa Itali Antonio Conte katika uwanja wa Stamford Bridge.

''Tulishindwa kutokana na mafikra yetu zaidi ya chochote kile. hiki ni kitu siwezi kukubali. Hili kundi la wachezaji hawa ni vigumu kuwasukuma'

Hiki sio kikosi kinachojulikana kwa mchezo wake mzuri.

Kikosi cha Sarri dhidi ya Arsenal kilishirikisha wachezaji saba ambao walishinda ligi ya Uingereza chini ya ukufunzi wa Conte 2017 kabla ya kumaliza katika nafasi ya tano msimu uliofuata.

Raia huyo wa Itali alisema hii sio timu ambayo itajulikana kwa mchezo mzuri lakini tunahitaji kuwa timu ilio na uwezo wa kupambana na mazingira kupata shida kwa kati ya dakika 10 ama hata 15 na baadaye kucheza mchezo wetu.

''Unaweza kujipata katika hali mbaya mara kwa mara lakini tunahitaji kuimarika zaidi ya tulivyofanya siku ya Jumamosi''.

Chelsea ilifunga magoli 27 katika mechi 11 za kwanza msimu huu lakini wameishia kufunga magoli 13 katika mechi 13.

Mshambuliaji Olivier Giroud na Alvaro Morata wameshindwa kuonyesha umahiri wao na klabu hiyo imehusishwa pakubwa na uhamisho wa mshambuliaji wa Juventus Gonzalo Higuain ambaye Sarri alishirikana naye akiwa klabu ya Napoli.

Sarri anasema kuwa fikra ya kikosi hicho inaweza kuimarishwa kupitia kupata mchezaji mpya.

''Ni sharti uwashawishi. Inaweza kuwa ni mchezaji mpya anakuja ama hata mchezaji mmoja wa zamani achukue jukumu'', alisema.

''Mchezaji katika kiwango hiki hawezi kuwa muoga kuchukua majukumu''.

Kitu kizuri ambacxho kinaweza kufanyika ni mimi na wachezaji kuzungumza kwa uwazi kuhusu kile kinachofanyika.

''Mimi ndio nimechukua jukumu hili na ni muhimu wao kuwa na tabia hiyo. iwapo hawawezi pengine basi wasicheze katika kiwango hiki''.