Matokeo UEFA Champions League PSG v Liverpool: Neymar asaidia miamba wa Ufaransa kuwalaza Liverpool 2-1

Chanzo cha picha, EPA
Liverpool wana kibarua kigumu kufuzu kwa hatua ya muondoano katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kujipata hoi mikononi mwa miamba wa Ufaransa Paris St-Germain na kupokezwa kichapo cha 2-1.
Mambo yalivyo sasa, vijana hao wa Jurgen Klopp waliofika fainali msimu uliopita, walio katika nafasi ya tatu Kundi C watahitaji kuwalaza Napoli wanaoongoza kundini katika mechi itakayochezewa Anfield mwezi ujao ndipo waweze kufuzu.
Vijana hao wa Serie A waliwalaza Red Star Belgrade 3-1 katika mechi hiyo nyingine kundi hilo.
Liverpool walizidiwa nguvu kwa vipindi virefu katika mechi hiyo iliyochezewa Paris, na mkwaju wa penalti wa James Milner uliozalisha bao lao la pekee mechi hiyo muda mfupi kabla ya mapumziko ilikuwa ndiyo mara yao ya pekee kulenga goli la PSG.

Chanzo cha picha, Rex Features
Kufikia wakati huo, walikuwa tayari wako mabao mawili nyuma, bao la kwanza wakifungwa na Juan Bernat baada ya utepetevu wa Virgil van Dijk na la pili wakafungwa katika shambulio la kujibu mashambulizi.

Matokeo mechi za UEFA Jumatano 28 Novemba, 2018
- Atletico Madrid 2-0 Monaco
- Borussia Dortmund 0-0 Club Brugge
- PSV Eindhoven1-2 Barcelona
- Tottenham 1-0 Inter Milan
- Napoli3-1 Red Star Belgrade
- PSG (Paris Saint Germain) 2-1 Liverpool
- FC Porto 3-1 Schalke
- Lokomotiv Moscow 2-0 Galatasaray


Chanzo cha picha, Getty Images
PSG wangekuwa na mabao mengi zaidi kipindi cha pili lakini bao la Marquinhos lilikataliwa kwa kuwa alikuwa ameotea.
Na kiungo huyo wa kati mlinzi pia alikosa bahati pale kipa mwenzake kutoka Brazil, Alisson, alipouzuia mpira wake wa kichwa kwa ustadi mkubwa.
Liverpool wanahitaji nini?
Pole, kuna hesabu hapa...
Sheria za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya zinaeleza kwamba iwapo timu zimetoshana nguvu kwa alama hatua ya makundi, basi hutenganishwa na matokeo ya mechi klabu zilipokutana.
Napoli waliwalaza Liverpool 1-0 nyumbani mechi ya kwanza.
- PSG wakiwalaza Red Star mechi yao ya mwisho, basi watasonga, maana kwamba Liverpool watahitaji mambo yafuatayo dhidi ya Napoli:
- Ushindi wa 1-0 utawawezesha kufuzu kwa sababu ya rekodi yao walipokutana na klabu nyingine.
- Ushindi wa mabao mawili au matatu utawawezesha kusonga kwa sababu ya matokeo mazuri dhidi ya Napoli.
- Hata hivyo, wakishinda 2-1 au 3-2, watatupwa nje, kwani Napoli watakuwa wamefunga bao au mabao ya ugenini, hivyo ndio watakaosonga kwa kufuata matokeo ya mechi klabu hizo zilipokutana.
Nini kinafuata?
Liverpool wana mechi nyingine muhimu, dhidi ya mahasimu wao wa Merseyside, Everton, katika Ligi ya Premia Jumapili.












