Wanawake 100 wa BBC: Wanawake wanaouawa siku moja maeneo tofauti duniani

Takriban wanawake 137 kote duniani huuawa na waume na pia wapenzi wao au watu wa familia kila siku, kwa mujibu wa data mpya zilizotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu (UNODC).
Wanasema nyumbani ndilo eneo ambapo kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa mwanamke kuuawa.
Zaidi ya nusu ya wanawake 87,000 waliuawa mwaka 2017 waliripotiwa kufa mikononi mwa watu walio karibu nao.
Kati ya idadi hiyo takriban wanawake 30,000 waliuawa na wapenzi wao na wengine 20,000 waliuawa na watu wa familia.
BBC 100 walitaka kujua zaidi wanawake waliojipata kwenye takwimu hizi. Tunakupa hadithi kuhusu baadhi ya mauaji haya na jinsi yaliripiotiwa.

Idadi ya wanaume wanaouawa bado ni ya juu
Data iliyokusanywa na UNODC ilionyesha kuwa wanaume kote duniani wako na uwezekano mara nne zaidi kuliko wanawake kupoteza maisha kutokana na kuuliwa makusudi
Umoja wa Mataifa unasema kuwa wanaume wanachangia vifo 8 kati ya 10 kote duniani.
Pia ripoti hiyo hiyo inasema kuwa zaidi ya vifo 8 kati ya 10 vya muaji yaliyofanywa na wapenzi ni dhidi ya wanawake.

Wanawake arobaini na saba, nchi 21, siku moja
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinachambua matokeo ya mwaka 2017 yanayotokana na takwimu za mauaji kutoka kwa serikali.
BBC 100 Women na BBC Monitoring walichukua hatua ya kufahamu zaidi kuhusu wanawake walioathiriwa.
Tulifuatilia wanawake waliouawa na watu wengine Oktoba mosi mwaka 2018 kote duniani. Wanawake 47 walihesabiwa kuuliwa kwa sababu zinazohusu jinsia kwenye nchi 21 tofauti na mengi ya mauaji haya bado yanachunguzwa.
Hivi ni visa vitano vilivyoripotiwa na vyombo vya habari na kisha kuidhinishwa na mamlaka mabzo BBC iliwasiliana nazo.

Chanzo cha picha, Family handout
Judith Chesang, 22, Kenya
Jumatatu 1 Oktoba Judith Chesang na dada yake Nancy walikuwa shambani wakivuna mtama.
Judith, mama wa watoto watatu alikuwa ametengana na mume wake Laban Kamuren na kuamua kurudi kwa wazazi wake katika kiji kilicho kaskazini mwa nchi.
Mara dada hao walianza kufanya kazi, aliwasili katika shamba la familia akashambulia na kumuua Judith.
Polisi wanasema Laban aliuawa na wanakijiji.

Afrika ndilo eneo wanawake wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kuuawa na wapenzi wao au na mtu wa familia kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa. Ilifanyika kwa watu 3.1 kati ya watu 100,000.
Asia ilikuwa na idadi ya juu zaidi ya wanawake waliouwa na wapinzani au watu wa familia mwaka 2017, kwa jumla wanawake 20,000.

Chanzo cha picha, Manohar Shewale
Neha Sharad Chaudury, 18, India
Neha Sharad Chaudury aliuawa wakati siku yake ya kuhitimiza miaka 18. Alikuwa ameenda kusherehekea na mpenzi wake. Polisi waliiambia BBC kuwa wazazi wake hawakukubaliana na uhusiano huo.
Wazazi wake na mwanamume mmoja wa familia wanalaumiwa kwa kumuua akiwa nyumbani usiku huo.
Uchunguzi unafanywa na watatu hao wako kuzuizini wakisubiri kushtakiwa.
BBC iligundua kutoka kwa wakili anayewakilisha wazazi wa Neha na mwanamume wa familia kuwa wanataka kukana mashtaka hayo.

Chanzo cha picha, Private via Amnesty International
Zeinab Sekaanvan, 24, Iran
Zeinab Sekaanvan alinyongwa na mamlaka za Iran kwa kumuua mume mwake.
Zeinab alizaliwa kaskazini magharibi mwa Iran kwenye familia moja maskini eneo la Kurdi. Alikimbia nyumbani akiwa msichana kuolewa akiwa na matumaini ya kupata maisha mazuri.
Amnesty International inasema mume wake alikuwa anadhulumu na alikataa kumpa talaka na kwamba malalamiko yake yalipuuzwa na polisi.
Alikamtwa kwa kumuua mume wake akiwa na umri wa miaka 17.
Waliomuunga mkono wakiwemo Amnesty wanasema aliteswa ili akiri kumuua mume wake, akapigwa na polisi na hakupata hukumu yenye haki.

Chanzo cha picha, Reproduction / Facebook
Sandra Lucia Hammer Moura, 39, Brazil
Sandra Lucia Hammer Moura aliolewa na Augusto Aguiar Ribeiro akiwa na miaka 16.
Wanandoa hao walikuwa wametengana kwa miezi mitano wakati mume wake alimuua.
Polis huko Jardim Taquari waliiambia BBC kuwa alichomwa kisu shingoni.
Walipata video ya mume wakae kwenye simu yake. Kwenye video hiyo alisema Sandra alikuwa na urafiki na mwamamume mwingine na alihisi kuhujumiwa.
Pia alisema kuwa hawezi kukamatwa kwa sababu wote watanda kwa Mungu pamoja. Kisha akajinyonga kwenye chumba chao cha kulala.

Chanzo cha picha, PHOTOPQR/LE PROGRES/Photo Jean-Pierre BALFIN
Marie-Amélie Vaillat, 36, Ufaransa
Marie-Amélie alichomwa kisu na kuuawa na mume wake, Sébastien Vaillat.
Wanandoa hao walikuwa wametengana baada ya miaka minne ya ndoa.
Alimshambulia kwa kisu kabala ya kukiri kwa polisi. Siku chache baadaye alijiua akiwa gerezani.
Nje ya mlango wa duka la Marie-Amélie Vaillat eneo la Rue Bichat, wenyeji waliacha maua na kupanga kufanya matembezi kwa heshima kwake.

Chanzo cha picha, PHOTOPQR/LE PROGRES/Photo Jean-Pierre BALFIN
Inagharimu nini kisa cha kuuliwa mwanamke kuripotiwa?
Kukusanya ripoti hizi, mtandao ya waandishi wa habari wa BBC Monitoring na watafiti walichambua televisheni, radio, magazeti na mitadao ya kijamii kote duniani, wakiangalia ripoti za wanawake waliouawa tarehe 1 Oktoba mwaka 2018.
Walipata jumla ya ripoti 47 za wanawake walioauawa kote dudiani. Tumechapisha baadhi ya visa hivi. Kuna vingine vingi ambavyo nia yao haijulikani au waliotekeleza hawajatambuliwa.

Je wanawake 100 ni nini?
BBC 100 Women huwataja wanawake 100 wenye ushawishi na wenye kutia moyo kote duniani kila mwaka na tunaangazia hadithi zao.
Umekuwa mwaka wenye umuhimu katika masuala ya haki za wanawake kote duniani, kwa hivyo mwaka 2018 msimu wa Wanawake bora 100 wa BBC, utaangazia wanawake waasisi wanaotumia ari, hasira na ghadhabu kushinikiza mageuzi halisi duniani.












