Man United vs Valencia: Jose Mourinho anyimwa raha Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Real Madrid wachapwa Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester United walishindwa kumpunguzia shinikizo meneja wao Jose Mourinho baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Valencia katika mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya iliyochezewa ugani Old Trafford.
United, ambao wanapitia mwanzo mbaya zaidi wa ligi katika kipindi cha miaka 29, walianza vyema kutokana na nguvu za Marcus Rashford na Alexis Sanchez waliorejeshwa kikosini.
Hata hivyo, wageni hao kutoka Uhispania waliimarika kadiri mechi ilivyosonga na wenyeji wakaanza kusambaratika.
Valencia ndio waliopata nafasi nzuri kabla ya mapumziko na baada ya mapumziko kabla ya United kuanza kuimarika tena.
Rashford alitikiza mwamba wa goli kwa frikiki, lakini Valencia walifanikiwa kulinda lango lao hadi mwisho wa msimu.
Sasa, United wamecheza mechi nne bila kupata ushindi.
United wamo nafasi ya pili katika Kundi H wakiwa na alama nne, mbili nyuma ya viongozi Juventus waliowalaza vijana wa Uswizi Young Boys 3-0 na ambao watakuwa wageni wa mashetani hao wekundu Old Trafford mnamo 23 Oktoba.
Mchezaji wa zamani wa United Cristiano Ronaldo anatarajiwa kucheza mechi hiyo.

Matokeo ya Jumanne 2 Oktoba, 2018
- Hoffenheim 1-2 Man City
- Juventus 3-0 Young Boys
- AEK Athens 2-3 Benfica
- Bayern Munich1-1 Ajax
- Lyon 2-2 Shakhtar Donetsk
- CSKA Moscow1-0 Real Madrid
- Roma5-0 Viktoria Plzen
- Man Utd 0-0 Valencia


Chanzo cha picha, Reuters
Tabasamu bila raha kwa Mourinho
Baada ya mechi ya Jumamosi ambapo walichapwa 3-1 na West Ham, matokeo yaliyowaacha United wakiwa nafasi ya 10 katika Ligi ya Premia, Mourinho alikuwa amesema kwamba hakuwa na wasiwasi kuhusu kazi yake.
Lakini kwenye maelezo yake kuhusu mechi kabla ya mechi hiyo kuanza, Mreno huyo alitoa wito kwa wachezaji wake kujizatiti na kuhakikisha kwamba wanakabiliana na wapinzani kila wanapokuwa na mpira.
Aidha, aliwataka "kunyenyekea, na kwamba mwisho wa kila mechi kila mchezaji anafaa kuwa amechoka sana kutokana na bidii aliyoitia mchezoni, kwa ajili ya klabu, mashabiki na wachezaji wengine."
Hata kama Mourinho analihisi joto la kupata matokeo mabaya, hakuonyesha dalili hata kidogo.
Alikuwa amevalia mavazi ya rangi nyeusi na akitafuna chingamu, alitokea uwanjani na kumkumbatia mkufunzi wa Valencia Marcelino na pia akamkumbatia Michy Batshuayi, mshambuliaji wa Chelsea aliye Valencia kwa mkopo, alipokwenda kuurusha mpira tena uwanjani.
Mourinho alisalia makini pembeni mwa uwanja, na alinong'onezana na Pogba wakati mmoja na baadaye kwenye mechi alionekana kuwatia moyo wachezaji wake wasilegee.
Muda ulipokuwa unayoyoma na Rashford akagonga mwamba wa goli, Mourinho alirejea kwenye kiti chake.
Lakini kipenga cha mwisho kilipopulizwa, alijinyanyua na kumsalimia Marcelino.

Chanzo cha picha, Reuters
Mourinho bila shaka aliwasikia baadhi ya mashabiki waliokuwa wakimzomea kutokana na hali kwamba United hawajashinda mechi hata moja ya ushindani kwao nyumbani katika kipindi cha karibu miezi miwili.
Mourinho alisema nini baada ya mechi?
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho alisema: "Wachezaji walijaribu. Waliongeza kiwango cha juhudi zao. Waliongeza kasi na msukumo wao kwenye mechi licha ya kwamba hatujakuwa na wachezaji wengi wenye msukumo sana kikosini. Hatuna kiwango cha kutosha cha kiufundi kwenye kikosi kutuwezesha kupanga mchezo kuanzia ngome yetu.
"Tulipojaribu kufanya jambo, tulilifanya vyema, ambalo ni kuzima timu yenye kasi sana kwenye kaunta. Tulijua kwamba hatungefanikiwa kuunda nafasi 20 za kazi. Wachezaji wetu washambuliaji hawamo katika nafasi nzuri zaidi, hawajiamini na hilo ni hata katika kiwango cha mchezaji binafsi.
"Tufikiri kwamba kwa kupata fursa tatu au nne hivi, tungefunga na kushinda mechi."
Masaibu ya Mourinho
- Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ameongoza klabu mechi nne za ushindani nyumbani bila ushindi kwa mara ya kwanza katika maisha yake kama mkufunzi .
- Manchester United hawajashinda mechi zao nne za karibuni zaidi Old Trafford - mkimbio mrefu zaidi tangu walipo Desemba 2015 (chini ya Louis van Gaal).
- Hiyo ilikuwa sare ya pili kwa Valencia katika mechi 18 walizocheza karibuni hatua ya makundi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (Walishinda nane, wakatoka sare 8). Sare hiyo nyingine ilikuwa Novemba 2012 dhidi ya Bayern Munich (1-1).
- Manchester United wamekutana na Valencia mara nyingi zaidi bila kushindwa kuliko mpinzani mwingine yeyote Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (wamecheza mara 7, wakashinda 2 na kutoka sare 5).
- Mechi tatu kati ya nne za karibuni zaidi za Manchester United didi ya klabu za Uhispania Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ziliisha kwa sare ya 0-0 (awali dhidi ya Real Sociedad mnamo Novemba 2013 na Sevilla Februari 2018).
Nini kinafuata?
United watawakaribisha Newcastle United uwanjani Old Trafford Jumamosi kabla ya kuwepo kwa mapumziko mengine ya kimataifa.
Mechi yao inayofuata Ligi ya Mabingwa Ulaya ni mechi ya nyumbani dhidi ya Juventus walio na Cristiano Ronaldo 23 Oktoba.
Valencia watakutana na Barcelona katika La Liga Jumapili kisha wakutane na Young Boys mechi yao itakayofuata Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.












