Matokeo Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya UEFA: Liverpool 3-2 PSG, Barcelona 4-0 PSV Eindhoven Messi akifunga hat-trick, Inter Milan 2-1 Tottenham Hotspur

Chanzo cha picha, Getty Images
Roberto Firmino alifunga bao dakika za mwisho na kuwawezesha miamba wa Anfield, Liverpool, kupata ushindi dhidi ya Paris St-Germain ya Ufaransa katika mechi ya kwanza Kundi C Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mechi hiyo ilichezewa Anfield.
Firmino hakuwa sawa kabisa kucheza na mechi ikianza alikuwa kwenye benchi kutokana na jeraha la jicho alilolipata wakati wa mechi ambayo walilaza Tottenham 2-1 Jumamosi katika Ligi Kuu ya England.
Lakini aliingia uwanjani dakika ya 72 na kuwasaidia vijana hao wa Jurgen Klopp kupata ushindi ambao walidhani ungewaponyoka baada ya Mfaransa Kylian Mbappe kusawazishia PSG.
Daniel Sturridge, aliyekuwa amejaza pengo la Firmino kikosi cha kuanza mechi, alikuwa amewafungia la kwanza kwa kichwa kutoka kwa krosi ya Andrew Robertson dakika ya 30.
James Milner aliongeza la pili kupitia penalti dakika sita baadaye baada ya Georginio Wijnaldum kuchezewa visivyo eneo la hatari.
Thomas Meunier aliwakombolea PSG bao moja kabla ya mapumziko dakika ya 40, lakini baada ya Liverpool kufanikiwa kuwadhibiti Neymar na Mbappe kwa kipindi kirefu mechi hiyo Liverpool walikuwa na matumaini makubwa.
Mohamed Salah alitumbukiza mpira wavuni lakini bao lake likakataliwa kwa sababu ya madhambi yaliyokuwa yamefanyika kabla afunge.

Chanzo cha picha, AFP
Vijana hao wa Klopp walishangazwa Mbappe alipoponyoka na kumbwaga kipa Alisson mechi ikiwa imesalia dakika saba kunako dakika ya 83.
Lakini Firmino aligeuka mkombozi na kuwawezesha Liverpool kuanza kampeni yao Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu kwa ushindi. Alimbwaga kipa Alphonse Areola kwa kombora la chini dakika ya 90+1.

Matokeo kamili ya mechi za Jumanne 18 Septemba 2018
- Barcelona 4-0 PSV Eindhoven
- Inter Milan 2-1 Tottenham
- Club Brugge 0-1 Borussia Dortmund
- Monaco 1-2 Atletico Madrid
- Red Star Belgrade 0-0 Napoli
- Liverpool 3-2 Paris Saint Germain
- Schalke 1-1 FC Porto
- Galatasaray 3-0 Lokomotiv Moscow


Chanzo cha picha, Getty Images
Mechi itakayofuata ya Liverpool Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya itakuwa ugenini Napoli tarehe 3 Oktoba
Napoli walitoka sare 0-0 na Red Star Belgrade mechi hiyo nyingine ya Kundi C.
Messi moto wa kuotea mbali: Barcelona 4-0 PSV

Chanzo cha picha, EPA
Kwingineko, Lionel Messi alifunga hat-trick yake ya 48 na kuwasaidia Barcelona kuwabomoa mabingwa wa Uholanzi PSV Eindhoven mechi yao ya kwanza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, dakika za 31, 77 na 87.
Nahodha huyo wa Barca alifunga kwanza kupitia frikiki kabla ya Luis Suarez kutikisa mwamba wa goli.
Ousmane Dembele aliwapiga chenga mabeki wawili na kufunga bao la pili la Barca.
Messi aliongeza la tatu kupitia frikiki ya Ivan Rakitic kabla ya beki wa Barcelona Samuel Umtiti kufukuzwa uwanani kwa kuoneshwa kadi mbili za manjano dakika ya 79.
Hata wakiwa wachezaji 10 uwanjani, Barca waliongeza la nne pale Suarez alipomfikishia Messi mpira, na mchawi huyo wa Argentina akambwaga kipa Jeroen Zoet akiwa hatua 15 kutoka kwenye goli.
Inter Milan wawashangaza Spurs San Siro
Katika mechi hiyo nyingine ya Kundi B, Inter Milan walitoka nyuma na kuwalaza Tottenham 2-1 uwanjani San Siro.

Chanzo cha picha, Reuters
Spurs walikuwa wamefunga dakika ya 53 kupitia Christian Eriksen, wakadhani wamefika.
Lakini walifanya mapinduzi kupitia mabao ya Mauro Icardi na Matias Vecino dakika ya 85 na 90+2.
Tottenham hawajakuwa na rekodi nzuri Italia, kwani wameshinda mechi moja pekee kati ya 10 walizocheza ugenini dhidi ya klabu ya Italia karibuni zaidi. Walitoka sare mechi nne na kushindwa tano kati ya hizo.
Christian Eriksen wa Spurs sasa amefunga mabao matatu katika mechi tano alizocheza karibuni zaidi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, bao moja zaidi yamabao aliyofunga katika mechi 24 alizocheza awali michuano hiyo.
Kwa Harry Kane, mambo si mazuri. Aliondoka uwanjani bila kumjaribu kipa kwa mara ya pili tangu mwanzo wa msimu uliopita katika mechi ambayo amecheza dakika 45 na zaidi. Alifanya hivyo pia dhidi ya Man City Aprili 2018.
Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Spurs kushindwa mechi tatu mtawalia mashindano yote chini ya Mauricio Pochettino, na pia mara ya kwanza tangu Machi 2014 walipokuwa chini ya Tim Sherwood.
Diego Costa awasaidia Atletico kujikwamua

Chanzo cha picha, Reuters
Atletico Madrid nao walitoka nyuma na kuwalaza Monaco 2-1 katika mechi ya kwanza Kundi A katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Samuel Grandsir alikuwa ametangulia kuwafungia wenyeji baada ya makosa ya Saul na Angel Correa.
Diego Costa alifunga kutokana na pasi ya Antoine Griezmann naye Jose Gimenez akafunga kwa kichwa kutokana na kona ya Koke na kuwakabidhi wageni uongozi.
Lakini Atletico, ambao meneja wao Diego Simeone alikuwa amekaa na mashabiki, karibu wapokonywe tonge dakika za mwisho pale Kamil Glik alipopata fursa, lakini alituma nje mpira wake wa kichwa.
Raia huyo wa Argentina, Simeone, alikuwa anatumikia marufuku ya mechi yake ya mwisho kati ya mechi nne alizokuwa amepigwa marufuku kutokana na mfarakano uliotokea mechi kati ya Atletico na Arsenal nusufainali ya Europa League msimu uliopita.
Atletico - ambao uwanja wao wa nyumbani wa Wanda Metropolitano utakuwa mwenyeji wa fainali msimu huu, wanajaribu kuepusha masaibu ya msimu uliopita walipoondolewa uwanjani hatua ya makundi.
Katika mechi hiyo nyingine ya Kundi A, Borussia Dortmund waliwalaza Club Brugge 1-0 kutokana na bao la Christian Pulisic, aliyekuwa anasherehekea miaka 20 tangu kuzaliwa kwake.
Kipa wa FC Porto Iker Casillas naye aliibuka kuwa mchezaji wa kwanza kushiriki katika misimu 20 tofauti Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya alipowachezea mechi iliyomalizika sare ya 1-1 na Schalke Kundi D. Katika mechi hiyo nyingine kundi hilo, Galatasaray waliwalaza Lokomotiv Moscow 3-0.
Mwaka wa Messi na Barcelona?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Barcelona wameshinda mechi 25 kati ya 27 za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya walizochezea Nou Camp, mechi hizo nyingine mbili zikiisha kwa sare. Mara yao ya mwisho kushindwa huko ilikuwa Mei 2013 mikononi mwa Bayern Munich (3-0).
- PSV Eindhoven hawajashinda mechi hata moja kati ya tisa walizocheza karibuni Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (Sare 4 Kushindwa 5).
- Messi amefunga dhidi ya klabu 30 tofauti Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya - ni Raul (33) na Cristiano Ronaldo (32) wamefunga dhidi ya wapinzani zaidi.
- Messi amefunga frikiki nane za moja kwa moja 2018 - idadi ya juu zaidi kwake katika mwaka mmoja.
- Raia huyo wa Argentina amefunga hat-trick nyingi kushinda mchezaji mwingine yeyote yule historia ya michuano ya ubingwa Ulaya (8). Amefungia Barcelona jumla ya hat-trick 42 na Argetina hattrick sita.












