Zlatan Ibrahimovic: Mshambuliaji wa Sweden afunga bao la kushangaza Marekani, ajiunga na Ronaldo na Messi

Chanzo cha picha, Getty Images
Zlatan Ibrahimovic amejiunga na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na kuwa miongoni mwa wachezaji ambao bado wanacheza ambao wamefunga mabao 500 na zaidi wakichezea timu kubwa ya klabu na taifa.
Alifanya hivyo kwa kufunga bao la kushangaza dhidi ya Toronto nchini Marekani.
LA Galaxy walikuwa nyuma 3-0 kabla ya mapumziko, lakini mshambuliaji huyo wa Sweden aliupiga mpira kwa kisigino cha mguu wake ukiwa ungali hewani na kuutumbukiza wavuni.
Ukitazama picha iliyo hapa juu utaona misuli yake ilivyojikaza, ishara kwamba halikuwa jambo rahisi kufunga bao kama hilo.
Mwenyewe hujiita Simba.
Bao lake hata hivyo halikuwasaidia LA Galaxy kwani Toronto mwishowe waliibuka washindi wa 5-3.
"Nawafurahia Toronto kwa sababu watakumbukwa kama waathiriwa wangu wa 500," Ibrahimovic aliambia runinga ya TSN baada ya mechi hiyo.
Lilikuwa ni bao la 17 kwa Ibrahimovic kuwafungia LA Galaxy tangu ajiunge nao kutoka Manchester United mwezi Machi mwaka huu.
Kwa sasa, ndiye mfungaji mabao bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Marekani na Canada (MLS) msimu huu.
Ibrahimovic, 36, amecheza mechi 747 za ushindani.
Amefunga jumla ya mabao 438 akichezea Malmo, Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, AC Milan, Paris St-Germain, United na LA Galaxy.
Mabao 62 ameyafunga katika mechi 114 za kimataifa alizochezea taifa lake la Sweden.

Mshambuliaji wa Juventus na Ureno Ronaldo anaongoza kwa wachezaji ambao bado wanacheza waliofunga mabao mengi zaidi duniani.
Anafuatwa na nyota wa Barcelona na Argentina Lionel Messi. Wachezaji wote wawili wamefunga zaidi ya mabao 600 katika timu kubwa wakichezea klabu na timu za taifa.
Rekodi ya dunia anaishikilia nani?
Ni nyota wa zamani wa Brazil na klabu za Santos na New York Cosmos Pele ambaye kwa mujibu wa Guinness World Record alifunga mabao 1,279 katika mechi 1,363 alizocheza kati ya 1956-1977.

Chanzo cha picha, Zlatan Ibrahimovic/Twitter












