Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafungaji mabao bora England: Maurizio Sarri asema nyota wa Chelsea Eden Hazard anaweza kufunga mabao 40 msimu huu
Mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard anaweza kufunga mabao 40 msimu huu na kujishindia tuzo ya mfungaji mabao bora Ligi ya Premia, kwa mujibu wa meneja wa klabu hiyo Maurizio Sarri.
Hazard alifunga mabao matatu dhidi ya Cardiff Jumamosi na kuwawezesha The Blues kupata ushindi wa 4-1.
Kufikia sasa amefunga mabao matano katika mechi tano zilizochezwa, moja kushinda mchezaji anayemfuata.
Baada ya mechi hiyo ya Jumamosi, Sarri alisema Mbelgiji huyo huenda akawa ndiye mchezaji bora zaidi Ulaya.
Alisema zamani alikuwa anaamini alikuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi Ulaya lakini kwa sasa anaamini huenda ndiye bora zaidi.
"Tumezungumza naye na kumwambia anaweza kufunga mabao 40," alisema Sarri.
"Kuna baadhi ya mambo anayoweza kuboresha, lakini anaweza."
Miongoni mwa anayotaka Hazard aboreshe, ni kutumia nguvu zake nyingi katika maeneo ya wapinzani uwanjani badala ya eneo la timu yake.
Kimsingi anamtaka ashambulie zaidi.
Hazard alijiunga na Chelsea mwaka 2012 na amewafungia jumla ya mabao 94 lakini hajawahi kufunga mabao 20 akichezea klabu mechi za ushindani msimu mmoja.
Mabao ya juu zaidi aliyofunga ilikuwa ni msimu wa 2014-15 alipofunga mabao 19, na misimu miwili iliyopita alifunga amabo 17 kila msimu.
Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah alishinda tuzo ya mfungaji mabao bora msimu uliopita baada ya kufunga mabao 32 Ligi ya Premia, na jumla ya mabao 44 mashindano yote.
Chelsea wanaongoza kwenye jedwali kwa wingi wa mabao, wakiwa wameshinda mechi zao zote msimu huu.
Klabu hiyo ya London magharibi imo alama mbili mbele ya mabingwa watetezi Manchester City lakini Sarri anaamini City na Liverpool walio wa pili wako bora zaidi kwa sasa kuliko Chelsea.
"Ni lazima tujiboreshe, hatua kwa hatua," alisema Mwitaliano huyo aliyechukua nafasi ya Mwitaliano mwingine Antonio Conte kabla ya mwanzo wa msimiu.
"Lengo langu ni tuwe klabu bora zaidi Ulaya katika kipindi cha mwaka mmoja, au mwaka mmoja unusu hivi. Hilo ndilo lengo.
"Nafikiri kwa maoni yangu kwa sasa, timu mbili, Liverpool na Manchester City wako vyema zaidi kutushinda."