Tetesi za Soka Ulaya Ijumaa 14.09.2018: Real Madrid, Neymar, Mbappe, Jurgen Klopp, Sir Alex Ferguson, Ethan Ampadu

Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa zinasema Real Madrid wana kitita cha £330m wanazotaka kutumia, huku rais wao Florentino Perez akipanga kuwanunua wachezaji nyota kuimarisha kikosi hicho. Miongoni mwa wachezaji anaowataka ni nyota wawili wa Paris St-Germain Neymar, 26 na Kylian Mbappe, 19. (AS, via Sun)
Meneja wa Arsenal Unai Emery amejitolea kuhakikisha mkabaji kamili Nacho Monreal anasalia katika klabu hiyo. Mchezaji huyo wa miaka 32 kutoka Uhispania amekuwa akitafutwa na Barcelona. (Daily Mirror)
Meneja wa Tottenham Mauricio Pochettino bado hajafutilia mbali uwezekano wa Toby Alderweireld, 29, kuafikiana kuhusu mkataba mpya na klabu hiyo. (Daily Express)
Liverpool wanatarajiwa kuwa imara zaidi watakapokutana na Tottenham mechi ya mapema Ligi ya Premia Jumamosi. Hii ni baada ya ndege ya kukodishwa kuwasafirisha wachezaji watatu wa Anfield kutoka Brazil Roberto Firmino, Alisson na Fabinho kutoka Marekani ambapo walikuwa wanachezea timu ya taifa. Walifika kwa wakati na kushiriki mazoezi na wachezaji wengine Alhamisi. (Daily Mirror)

Chanzo cha picha, Getty Images
Roma wanajizatiti kuondoa vifungu vya kuondoka kwa beki wao Mgiriki Kostas Manolas, 27, kutoka kwenye mkataba wake. Beki huyo amehusishwa nakuhamia Chelsea na Manchester United, pamoja na kiungo wa kati Lorenzo Pellegrini, 22, ambaye anaaminika kunyatiwa na Manchester City. (Calciomercato)
Barcelona walivunja rekodi ya dunia walipolipwa euro 222m kumuuza Neymar kwa Paris St-Germain Agosti 2017, lakini klabu hiyo ya Catalonia imelazimika kulipa asilimia tatu ya fedha hizo ambazo ni euro 6.6m kwa mtaalamu kutoka Brazil Andre Cury kwa mchango wake katika kufanikisha uhamisho huo. (Marca)
West Brom bado hawajaamua kuhuus wachezaji wasio na mikataba Wes Hoolahan, 36, na Russell Martin, 32, ambao walikaribishwa kushiriki mazoezi na klabu hiyo wakati wa mapumziko ya kimataifa. (Birmingham Mail)
Meneja wa Tottenham Mauricio Pochettino amesisitiza kwamba hana wasiwasi kuhusu uchezaji wa Harry Kane msimu huu. Mchezaji huyo wa Englandmwenye miaka 25 amefunga mabao mawili katika mechi nne alizowachezea Spur msimu huu. (Talksport)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkufunzi mkuu wa Cardiff Neil Warnock, 69, bado hajaamua ni wakati gani atastaafu. (London Evening Standard)
Jurgen Klopp anatarajiwa kuimarisha zaidi benchi lake la wakufunzi Liverpool kwa kumuongeza kocha wa makipa wa timu ya taifa ya wachezaji chipukizi England Jack Robinson, ambaye alifanya kazi Manchester United kwa miaka saba. (Liverpool Echo)
Sir Alex Ferguson alitaka kumnunua mchezaji wa kimataifa wa Wales Ethan Ampadu, 17, akiwa Manchester United pale kiungo huyo wa kati mkabaji wa Chelsea alipocheza michuano ya watoto akiwa na miaka 12. (Manchester Evening News)

Chanzo cha picha, Getty Images
Kevin Keegan atafichua ukweli wa kutamausha kuhusu kipindi chake cha pili alichokaa kama mkufunzi Newcastle katika hafla itakayowashirikisha mashabiki huku akiendelea kutangaza kitabu chake kipya mweiz ujao. (Newcastle Chronicle)
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya England Stuart Pearce anaamini mtazamo wa Gary Neville kwamba Liverpool wanafaa kuhakikisha wanaondoka Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mapema ili kujiimarishia nafasi ya kushinda ligi kuu England ni "sahihi asilimia 95 pekee" (Talksport)
Meneja wa Blackburn Tony Mowbray anasema klabu hiyo itamuunga mkono kikamilifu mchezaji wao Bradley Dack mwenye miaka 24, lakini anasema alihisi mchezaji huyo alionekana kutomakinika baada ya kukiri kukaidi masharti ya kifungo cha nje. (Lancashire Telegraph)
Gareth Evans, afahamikaye kama Harry the Hornet, kibonzo wa Watford aliye maarufu kutokana na miondoko yake na uchezaji ngoma, ameng'atuka kutoka kwenye wadhifa huo. (Watford Observer)
Bora kutoka Alhamisi

Chanzo cha picha, Getty Images
Beki Jerome Boateng, 30, amemwambia Jose Mourinho kuwa amekataa ofa ya kujiunga na Mashetani Wekundu kwa sababu haoni kuwa kuhamia Manchester United akitokea Bayern Munich kama kupiga hatua ya maendeleo. (Mirror)
Mshambuliaji Marcus Rashford anataka kusalia Manchester United na kupambana kupata nafasi katika kikosi cha kwanza. Hatahivyo kama atashindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza basi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 atalazimika kufanya maamuzi magumu mwishoni mwa msimu. (Sun)
Kocha wa Manchester United Mourinho "ameshindwa kumvumilia" winga wa klabu hiyo Anthony Martial mwenye umri wa miaka 22. Martial anatarajiwa kuondoka United na kujiunga na timu nyengine ya ligi kuu ya England. Klabu za Arsenal na Tottenham zimeonesha nia ya kumsajili raia huyo wa Ufaransa. (Express)
Paul Pogba "aliahidiwa" na wakala wake wakati anarejea Manchester United akitoka Juventus kuwa angejiunga na Barcelona au Real Madrid mara baada ya kumalizika kwa msimu.(Manchester Evening News)

Chanzo cha picha, Rex Features
Rais wa Real Madrid Florentino Perez ameghadhabika baada ya kusikia mipango ya kocha wa zamani wa klabu hiyo Zinedine Zidane kuwa anataka kuinoa Manchester United.(Express)
Kiungo mchezeshaji wa Lyon Nabil Fekir, 25, ameachana na fikra za kukwama kwa uhamisho wake - lakini hilo halijamkatisha tamaa ya kufikiria kuchezea Ligi ya England katika siku za usoni. (Mirror)
Winga Willian amesema hakutaka kabisa kuhama Chelsea katika kipindi hiki licha ya kutakiwa na Manchester United na kupokea ofa mara tatu kutoka Barcelona. Raia huyo wa Brazil mwenye miaka 30 anatumai kusalia Chelsea kwa miaka mitano zaidi. (Sky Sports)












