Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ligi Kuu England: Teknolojia ya VAR kufanyiwa majaribio mechi tano za EPL Jumamosi
Teknolojia ya kutumia video kuwasaidia waamuzi, maarufu kama VAR, itafanyiwa majaribio katika mechi kadha kwa pamoja Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza Jumamosi.
Teknolojia hiyo itajaribiwa katika mechi tano ambazo zitakuwa zinachezwa kuanzia saa kumi na moja saa za Afrika Mashariki.
Baada ya kujaribiwa katika mechi moja moja msimu uliopita, wasimamizi wa Ligi ya Premia sasa wanataka kuona iwapo teknolojia hiyo inaweza kufanikiwa ikitumiwa katika mechi kadha kwa wakati mmoja.
Majaribio hayo yatakuwa yanadhibitiwa kutoka kituo kimoja kikuu cha VAR.
Hakutakuwa na mawasiliano ya aina yoyote na waamuzi uwanjani mechi zitakapokuwa zikiendelea.
Kwa sasa wakati wa majaribio, teknolojia hiyo ya VAR itatumiwa katika uamuzi wa kuthibitisha magoli yanapofungwa, kuamua mikwaju ya penalti, kadi nyekundu za moja kwa moja na kuwatambua wachezaji wakati wa kutoa adhabu, hasa wanapokuwa wengi kwa pamoja kiasi cha kumkanganya mwamuzi.
Mechi ambazo VAR itafanyiwa majaribio
- AFC Bournemouth v Leicester City
- Chelsea v Cardiff City
- Huddersfield Town v Crystal Palace
- Manchester City v Fulham
- Newcastle United v Arsenal
Aprili, klabu za Ligi ya Premia zilipiga kura dhidi ya kutumiwa kwa teknolojia hiyo msimu wa 2018-19.
Sawa na msimu uliopita, VAR itatumiwa tu katika Kombe la EFL na Kombe la FA lakini katika viwanja vya klabu zinazocheza ligi kuu.
Ilitumiwa katika mechi 19 msimu uliopita, na msimu huu inatarajiwa kutumiwa katika mechi takriban 60.