Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afcon U-17: Simba watoto wa Uganda na Serengeti Boys wa Tanzania kuwakilisha ukanda wa Cecafa Mei 2019
Timu ya Uganda ya vijana wa chini ya miaka 17 imeungana na wenyeji Tanzania katika kufuzu kwa michuano ya vijana yatakayotimua vumbi mwezi Mei 2019.
Uganda, maarufu kama Simba Watoto, walijikatia tiketi hiyo Jumapili baada ya kuiadhibu Ethiopia katika mchezo wa fainali wa mashindano ya kufuzu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa magoli 3-1.
Iliwachukua dakika 15 tu Simba watoto hao kuandika bao la uongozi kupitia Samson Kasozi katika uga wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Abdul Wahad Iddi alikuwa mwiba mkali kwa Waethopia baada ya kuiandikishia Uganda magoli mawili katika kipindi cha pili.
Ethiopia walifanikiwa kupata goli la kufutia machozi katika dakika za 'lala salama' kupitia Wondimagegn Bunaro.
Tanzania yatuzwa kwa nidhamu
Tanzania ilipata tuzo ya timu yenye nidhamu kwenye michuano hiyo. Kelvin John alichaguliwa kuwa mchezaji Bora wa michuano hiyo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (Caf) Ahmad Ahmad alikuwa ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwepo uwanjani kutazama mtanange huo.
Katika mchezo wao wa nusu fainali, Uganda waliwaacha midomo wazi timu ya Tanzania, maarufu kama Serengeti Boys kwa kuwachabanga magoli 3-1. Ethiopia wao waliwafunga Rwanda katika hatua hiyo.
Serengeti Boys, ambao walishafuzu kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo yatakayofanyika Mei 2019, wamemaliza michuano ya kufuzu katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Rwanda kwa mikwaju ya penati 4-3.
Dakika 90 zilimalizika kwa vijana hao kutoshana nguvu kwa goli 2-2.
Mafanikio ya Simba watoto yanakuja katika kipindi amabacho kaka zao, timu ya wakubwa ya Uganda, The Caranes, imekuwa na mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na walishiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 baada ya kusubiri kwa miaka 39.
"Tunafuraha kwa kuwa hii ndio mara ya kwanza kwa vijana wetu kufuzu kwa mashindano haya. Kufuzu huku ni ushuhuda kuwa tunafanya kazi nzuri katika eneo kuendeleza vijana," amesema Moses Magogo, Rais wa chama cha mpira wa miguu nchini Uganda.
Kabla ya kuanza kwa michuano ya kufuzu, Caf iliwazuia wachezaji 11 kushiriki kutokana na kuwa na umri mkubwa baada ya kufanyiwa vipimo ya mifupa (MRI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hii ni mara ya kwanza kwa Caf kufanya mashindano ya kufuzu kwa michuano ya vijana chini ya miaka 17 kutokana na kanda za kijiografia.
Michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya bara la Afrika yatafanyika kuanzia tarehe 12 mpaka 26 Mei 2019 nchini Tanzania, na timu zitakazomaliza katika nafasi nne za juu zitaiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa nchini Peru mnamo Oktoba 2019.