Julen Lopetegui asema Gareth Bale 'atajaza pengo' la Ronaldo Real Madrid

Chanzo cha picha, Reuters
Gareth Bale anaweza kusaidia kujaza pengo lililowachwa na kuondoka kwa Cristiano Ronaldo katika klabu ya Real Madrid, kulingana na mkufunzi huo wa Uhispania Julen Lopetegui.
Mshambuliaji wa Wales Bale alikuwa amehusishwa na uhamisho kutoka klabu hiyo baada ya kushindwa kushiriki katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo chini ya ukufunzi wa Zinedine Zidane msimu uliopita.
Lakini uhamisho wa Ronaldo kuelekea Juventus uliogharimu £99m unamaanisha kwamba Bale sasa ni kiungo muhimu katika timu hiyo.
Gareth Bale anafurahi kusalia Real Madrid, alisema Lopetegui.
"Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika historia ya hivi karibuni ya Real Madrid. Alitaka kuondoka na tukamwachilia kuondoka. Gareth Bale ni mchezaji mzuri sana anaweza kujaza pengo hilo''.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 aliyejiunga na Real Madrid kwa dau la £87m mwaka 2013 na ameshinda kombe la vilabu bingwa mara nne , akifunga mara mbili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Liverpool mnamo mwezi Mei.
Lopetagui alisema alicheza vyema na mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzima.
''Iwapo kikosi hiki ndicho nitakachokuwa nacho wakati wa kuanza kwa msimu nitafurahi sana''.
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari kabla ya Real kucheza dhidi ya United katika mechi ya kimataifa mjini Miami siku ya Jumanne, alipinga mazungumzo ya Bale kujiunga na ligi ya Uingereza.
''Sitaki kuzungumza kuhusu mambo ambayo hayawezi kuwa'', alisema mkufunzi huyo wa zamani wa Uhispania.
''Gareth Bale anafurahia kucheza Real Madrid. Hii ni fursa nzuri kwa yeye kuonyesha kipaji chake na kwa sasa anashirikiana na timu''.












