Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uingereza yafuzu nusu fainali kwa kuilaza Sweden 2-0
Baada ya kujaribu kwa mara ya tisa, hatimaye timu ya taifa ya Uingereza imefuzu kwa nusu-fainali Kombe la Dunia.
Ni hatua kubwa kwa timu hiyo kwani mwisho walishiriki nusu-fainali mnamo 1990 - baada ya miaka 28.
Hii ni baada ya kuitwanga Sweden 2-0 ugani Samara kwenye ngoma ya robo-fainali.
Beki Harry Maguire aliiweka three lions kifua mbele dakika ya (30) kupitia kona kipindi cha kwanza kabla ya kiungo Dele Alli kuzidisha la pili dakika ya (58).
Goli hilo la Dele Alli limemfanya kuwa Muingereza mwenye umri mdogo zaidi kuipa bao Kombe la Dunia tangu Michael Owen alipofunga akiwa na umri wa miaka (18 na siku 190) wakichuana na Romania,1998).
Alli ana umri wa miaka 22 na siku 87.
Ingawa Harry Kane, anayeongoza orodha ya wafungaji Urusi akiwa na mabao 6, hakupata bao, halijamzuia kuisaidia Uingereza kwa kuwashughulisha mabeki wa Sweden, Victor Lindelöf na Andreas Granqvist.
Kikosi cha Gareth Southgate kiliwanyamazisha wengi kufuatia uhodari dhidi ya Sweden ambao walikuwa wanakutana na Uingereza kwenye mechi ya tatu Kombe la Dunia.
Michuano ya awali kati ya wawili hao iliishia sare ya 1-1 na 2-2 wa mwisho ukiwa 2006, nchini Ujerumani.
Kipa wa Uingereza ambaye pia ndiye mchezaji bora wa mechi, Jordan Pickford, alikuwa tegemeo la timu kwa mara nyengine baada ya kupangua mipira iliyoelekea langoni na kudumisha uongozi hadi dakika ya mwisho.
"Ni matokeo mazuri, tulitarajia mechi kali dhidi ya Sweden, tulijua walivyojihami, tulikabiliana nao vyema, na kwa makini. Tumejitahidi na kudhihirisha uwezo wetu na juhudi zetu mechini.'' Alisema Pickford.
Imekuwa ni siku ya uchungu kwa Sweden kwani safari yao hadi robo fainali haikuwa rahisi.
Ilifuzu kutoka kundi hatari lililowajumuisha Ufaransa na Uholanzi kabla kuinyima Italia katika mechi ya kumsaka mshindi.
Hata baada ya kuwekwa kwenye kundi moja na Ujerumani, Mexico na Korea, katika Kundi F, Sweden ilimaliza wa kwanza.
Kwa sasa Uingereza inamsubiri mshindi kati ya Croatia na Urusi kabla ya kurudisha tabasamu kwa nyuso za mashabiki wake tangu 1966 walipolitwaa Kombe la Dunia.