Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Real Madrid wanapanga kumuuza Cristiano Ronaldo, atakwenda Juventus?
Klabu ya Uhispania ya Real Madrid inajiandaa kukubali kitita cha Euro milioni 100 (£88m) kutoka Juventus ili kumuachia Cristiano Ronaldo.
Mshambulizi huyo miaka 33 ndiye mfungaji bora katika historia ya Madrid akiwa na mabao 451.
Hata hivyo, Umri wake, na mipango ya klabu yake kuandaa kikosi kipya kutokana na kile kilichosajili alama 17 nyuma ya mabingwa wa La Liga, Barcelona, imeipa matumaini mabingwa wa Italia kukamilisha uhamisho.
Ronaldo alipokea medali yake ya tano ya Champions League kwa kutwaa kombe hilo na Madrid mwezi Mei.
Aidha, baada ya ubingwa dhidi ya Liverpool mjini Kiev, mkufunzi wa Real Zinedine Zidane pia ameagana na klabu hiyo huku akimpisha kocha wa zamani wa uhispania Julen Lopetegui.
Mustakabali wa Ronaldo, Mshindi mara tano wa Ballon d'Or umekuwa gumzo kwa kipindi kirefu miaka ya awali na uhusiano wake na rais wa klabu hiyo Florentino Perez umeaza kutiliwa shaka.
Uhamisho wowote utapiku rekodi ya usajili katika klabu ya Juventus iliyowekwa kufuatia kuwasili kwa mfungaji wa Argentina Gonzalo Higuain kwa euro milioni 90m walizotoa kwa real mwaka wa 2016.
Pesa za usajili wa Ronaldo kutoka Real Madrid zitazidi bei yake ya pauni milioni £80 alipojiunga nao kutoka Manchester United mnamo 2009.
Muda wa mabadiliko Bernabeu?
Ripoti za Cristiano Ronaldo kupoteza furaha Real Madrid zimekuwa zikitabirika kila mwaka, na yamekuwa yakitatuliwa kwa nyongeza ya mshahara kwa mreno huyo na mahitaji yake mengine kutimizwa.
Lakini awamu hii, Ronaldo alipofunguka kuhusu hali yake katika klabu hiyo, punde tu baada ya ushindi kwenye fainali ya Kombe la Champions League dhidi ya Liverpool, hakuna aliyempa sikio hapo mwanzoni.
Hili linaonekana kuchukua mkondo tofauti wakati huu na dalili zote nchini Uhispania zinaashiria kuwa huu ndio msimu wa Ronaldo kuondoka Real Madrid.
Uwezekano wa kuondoka kwake umeongezeka kwani Real Madrid imejiepusha na kujitetea kwa vyombo au kutoa taarifa kupinga madai kuhusu fununu za uhamisho wa Ronaldo au hata kujitokeza kufafanua kuwa atasalia kwenye klabu.
Haya yanamaanisha kuwa rais Florentino Perez anaamini huu ndio msimu wa kumhamisha nyota huyu.
Ikiwa Real itaweza kuitoza Juventus euro milioni 100m, Perez ataridhika kuwa ni dili nzuri kwa mchezaji atakayeingia miaka 34 mwisho wa msimu ujao.
Ronaldo kumpisha Neymar?
Kwa muda mrefu ilionekana kuwa ni muda tu kabla ya nyota huyo wa Brazil kuondoka Paris kuelekea Madrid, ambapo usakataji wake bora wa soka na fursa za mauzo na mikataba ya kibiashara yatamfanya msajiliwa wa maana.
Ikiwa Neymar atafika msimu huu, itakuwa vigumu kujua jinsi kiburi chake kitaoana na cha Ronaldo au kuelewana vizuri uwanjani na chumba cha wachezaji, na Ronaldo atalazimika kumpa Neymar nafasi.
Hata kama Neymar atatua Real, Rais Perez pia ni shabiki mkubwa wa star mwingine wa PSG, Kylian Mbappe, ambaye maonyesho yake yamekuwa ya kufana Kombe la Dunia Urusi na kumfanya mchezaji wa kuvutia Zaidi.
Licha ya yote, ni msimu wa mabadiliko Bernabeu.
'Tatizo ni Mshahara wa Ronaldo'
Mwandishi James Horncastle ameiambia BBC kuwa malipo ya Ronaldo yamekuwa changamoto kwa sababu ni mara nne anayopokea Higuain, mchezaji anayelipwa zaidi Juventus.
Juventus wanavutiwa sana na Ronaldo, na wamekuwa wakifanya mazungumzo na ajenti wake.
Hata hivyo, inaonekana kuwa itakuwa uhamisho mgumu kukamilika.