Joachim Low: Ujerumani walistahili kuondolewa Kombe la Dunia 2018

Chanzo cha picha, Reuters
Kocha wa Ujerumani Joachim Low amesema walistahili kuondolewa michuao ya Kombe la Dunia.
Mabingwa hao watetezi walimaliza wakiwa wanashika mkia Kundi F baada ya kushindwa 2-0 na Korea Kusini.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ujerumani kuondolewa katika raundi ya kwanza katika michuano hiyo tangu 1938.
"Hili ni jambo la kutufanya tutafakari," Low asema.
"Hili ni jambo la kihistoria. Na nina uhakika kwamba litazua malalamiko kutoka kwa umma Ujerumani."
Sweden walimaliza kileleni katika kundi hilo baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Mexico mechi iliyokuwa inachezwa wakati mmoja na hiyo ya Ujerumani.
Hii ilikuwa na maana kwamba Ujerumani walihitaji kuwashinda Korea Kusini mjini Kazan ndipo wafuzu.
"Tuliona Sweden walikuwa wamechukua uongozi mechi yao hivyo tulihitaji kuendelea kushambulia lakini timu yetu ilikuwa inatatizwa na mtiririko wa mechi na hatukuwa na ustadi ambao huwa ni kawaida yetu kuwa nao. Kwa hivyo, ni kweli, tulistahili kutupwa nje, ndio," alisema Low ambaye hajawahi kushindwa kufika nusufainali katika miaka 12 ambayo amekuwa mkufunzi.
"Katika michuano hii hatukustahiki kushinda au kufika hatua ya 16 bora. Tuliondolewa sio kwa sababu etu hatukutaka kushinda lakini kwa sababu hatukuwa na nafasi yoyote ya kuchukua uongozi wakati wowote ule - tulikuwa kila wakati tuko nyuma, tukijaribu kuwafikia."

Chanzo cha picha, Siegel
Mabao yote mawili ya Korea Kusini yalifungwa muda wa ziada, dakika mbili na dakika tatu baada ya dakika 90 kuchezwa.
Bao la Kim Young-gwon lilikuwa awali limekataliwa lakini baadaye likakubaliwa baada ya kutumiwa kwa VAR.
Na baada ya kipa wa Ujerumani Manuel Neuer kugeuka mchezaji na akapokonywa mpira akiwa eneo la Korea Kusini, Ju Se-jong alipiga mpira wa mbali uliomfikia Son Heung-min na mshambuliaji huyo wa Tottenham akautumbukiza mpira kwenye lango lililokuwa wazi.
Historia
- Hii ndiyo mara ya pili katika historia kwa Ujerumani kuondolewa michuano katika raundi ya kwanza, mara ya mwisho ikiwa mwaka 1938 kabla ya hatua ya makundi kuanzishwa.
- Ujerumani walifika angalau nusufainali fainali nne zilizopita za Kombe la Dunia walizoshiriki - ambapo walifika nusufainali mara mbili.
- Hii ni mara ya tatu kwao kutofika robofainali tangu 1978, waliondolewa robofainali 1994 na 1998.
- Ujerumani ndio mabingwa watetezi wa nne kuondolewa hatua ya makundi Kombe la Dunia katika fainali tano za karibuni (pia Ufaransa 2002, Italia 2010, Uhispania 2014)
- Hii ni mara ya kwanza kwa Ujerumani kukosa kuishinda timu ya bara Asia Kombe la Dunia. Mechi za awali walishinda kwa jumla ya 19-3.
- Tangu makala ya 2010, Ujerumani wameshindwa mechi mbili za Kombe la Dunia ambazo Thomas Muller hakuwa kwenye kikosi cha kuanza mechi (walishindwa pia 0-1 na Uhispania nusufainali mwaka 2010) ukilinganisha na anapowachezea ambapo walishinda mechi 12 kati ya 15.
- Mabao mawili ambayo Ujerumani wamefunga Kombe la Dunia mwaka huu ndiyo idadi ya pili kwa uchache wa mabao kufungwa na bingwa mtetezi, ambapo wamewashinda Ufaransa mwaka 2002 walipokosa kufungwa bao lolote.

Chanzo cha picha, BBC Sport
Ujerumani walishindwa 1-0 mechi yao ya kwanza na kisha wakalaza Sweden 2-1 kupitia bao la dakika ya 95 la Toni Kroos na kufufua matumaini ya kusonga mbele.
Low aliamua kumuacha nje Thomas Muller - ambaye amefunga mabao 10 Kombe la Dunia - kwenye benchi kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo tangu 2010 nusufainlai dhidi ya Uhispania.
"Kwa mujibu wa niliyoyaona leo, tulikuwa na kikosi kizuri, Thomas Muller hakuniridhisha katika mechi za kwanza mbili hivyo nilifikiri nitatuma ujumbe. Ilikuwa ni lazima kubahatisha, hatuendea na kusubiri tu na ni kwa sabbau hivyo kwamba tulijipata tukifungua mianya safu ya nyuma.
"Tukiwa na kipindi kizuri cha maandalizi kambini, timu imefanya kazi vyema na tulihisi kwamba tungebadilisha gia lakini tulishindwa na Mexico wakati ambapo kupata alama moja kungetufaa sana na hatukuweza kubadilisha gia tena.
"Ulishawishika kwamba wakati michuano iikianza mambo yangeenda vyema lakini hiyo haikuwa.
"Tumekuwa tukiongeza presha kujaribu kufunga mabao, hasa vipindi vya pili, lakini hatukufanikiwa. Tulikuwa maiti, kimsingi, baada ya bao lao la kwanza. Tulifahamu kwamba hatukuwa na nafasi yoyote tena.
"Nimepigwa na butwaa kwamba hatukuweza kuwashinda Korea Kusini. Nilipozungumza na timu nilielewa kwamba walijihisi wakiwa na presha. Walikuwa tayari kusonga mbele, kucheza na kufuzu. Tunahitaji kuzungumzia hili kwa utulivu na nafikiri itatuchukua saa kadha kukubali ukweli huu."
Drogba hakushangaa
Mchezaji wa zamani wa Chelsea na Ivory Coast Didier Drogba ameambia BBC One kwamba mwenyewe hakushangaa.
"Hii haikushangaza, ikizingatiwa uchezaji wao mechi ya kwanza, na pia walisumbuka dhidi ya Sweden."

Chanzo cha picha, Getty Images
"Baada ya bao hilo la dakika za mwisho (dhidi ya Sweden), tulifikiria wangerejea lakini walicheza vibaya tena leo. Hawakustahili kusonga.
"Nafikiri hali si shwari kwenye kikosi. Tunafahamu kuhusu mkutano wa Mesut Ozil na Ilkay Gundogan na rais wa Uturuki, na Ujerumani kutokuwa na umoja tangu wakati huo. Kisha unatazama matokeo, yale yanayotokea. Siku moja haya yatakuja kukuuma."












