Kombe la Dunia Urusi 2018: Mo Salah ajipata kwenye mzozo kuhusu picha

Kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov amemtumia Mohamed Salah kujinufaisha kisiasa baada ya kupigwa picha na nyota huyo raia wa Misri, kwa mujibu wa mkuu wa shirika linalopambana na ubaguzi duniani.

Kikosi cha Misri kitakachoshiriki Kombe la Dunia kiko jamhuri hiyo ya zamani iliyokuwa chini ya Urusi zamani na ambayo imeathiriwa sana na vita.

Utawala wa kiongozi wa jamhuri hiyo Kasyrov umelaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu.

Piara Power kutoka Fare Network alisema Fifa ilifanya makosa makubwa kuruhusu Chechnya kuwa kambi ya kufanyia mazoezi.

Kadyrov alitetea rekodi yake ya haki za binadamu alipofanya mahojiano na BBC mapema mwaka huu.

Akizungumza mwezi Januari alisisitiza kuwa ripoti kuhusu mauaji ya kiholela na mateso dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Chechnya ilibuniwa.

Shirikisho la kandanda duniani Fifa limejitetea kila wakati kuwa linalinda haki za binadamu.

Lakini mkurugenzi mkuu wa Fare Network aliiambia BBC kuwa wameelezea wasiwasi kuhusu Chechnya kuwa kambi ya kufanyia mazoezi kwa muda mrefu.

"Kama unamjua Kadyrov na unafuatilia vile anaongoza eneo hilo, basi wakati fulani unaweza kujua kuwa anajaribu kujinufaisha kisiasa, na ninafikiri amefanya hivyo (kwa picha yake na Mo Salah)."

Amnesty International ilisema picha hiyo na Salah ilikuwa na manufaa ya kisiasa.

Wasi wasi wa Salah kucheza mechi ya ufunguzi

Huijulikani ikiwa Salah atakuwa kwenye kikosi kitakachokutana na Uruguay wakati wa mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia siku ya Ijumaa.

Mshambuliaji huyo wa Liverpool mwenye miaka 25 alipata jeraha la bega walipokabiliana na Sergio Ramos wakati Liverpool ilishindwa na Real Madrid kwenye fainali ya ligi ya mabingwa.

"Anaendelea kupata nafuu lakini siwezi kuthibitisha ikiwa atacheza mechi ya kwanza," alisema meneja wa shirikisho la kandanda la Misri, Ehab Lehita.