Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wenger apatwa na mtego wa habari za uzushi
Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger ameangukia mtego wa habari za uzushi mtandaoni kwamba mchezaji nyota wa zamani George Weah ameshinda urais nchini Liberia.
Ukweli ni kwamba matokeo ya uchaguzi huo wa Jumanne bado hayajatangazwa.
Wenger alikuwa akihutubia wanahabari katika kikao cha kutoa maelezo kuhusu hali ya kikosi chake kabla ya mechi za wikendi.
Wenger, kwa mujibu wa tovuti ya Arsenal, amesema: Ningependa kumpongeza mmoja wa wachezaji wangu wa zamani, ambaye amekuwa rais wa Liberia, George Weah.
"Si kila siku ambapo mchezaji wa zamani huwa rais wa taifa na kwa hivyo hongera Georgie na ninachoweza kumwambia tu ni kwamba aendeleze moyo na hamu yake ya kujifunza na kushinda."
Arsene Wenger alikuwa meneja wa Weah katika klabu ya Monaco miaka ya 1990.
Weah, mshindi wa zamani wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani ya Fifa, alikuwa anawania urais kwa mara ya tatu baada ya kushindwa na Ellen Johnson Sirleaf mara mbili awali.
Sirleaf anastaafu.