Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uganda haikuweza kulipia leseni ya matangazo AFCON
Shirika la Utangazaji la Uganda (UBC) limesema halikufanikiwa kupata haki ya kupeperusha mechi za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) moja kwa moja kutokana na uhaba wa pesa.
Hii ni licha ya kwamba timu ya taifa ya Uganda, Cranes, inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.
UBC imesema haikuweza kupata $600,00 ( £485, 000) zinazohitajika kujipatia leseni ya kupeperusha mechi hizo.
Badala yake, shirika hilo litawatangazia raia wa Uganda matukio makuu pekee kwenye mechi.
"Ni kwa masikitiko makubwa ambapo tunawatangazia rasmi watazamaji wetu na taifa kwa jumla kwamba UBC itapeperusha tu matukio makuu ya mechi na kutoa matangazo ya redio pekee kupitia vituo vyetu vyote," taarifa ya UBC imesema.
Mwandishi wa BBC nchini Uganda Catherine Byaruhanga anasema kuna uwezekano kwamba serikali itaingilia kati kusaidia, kama ilivyofanya mara kadha awali.
Kiongozi wa upinzani Kizza Besiye amesema ni aibu kubwa kwamba UBC haiwezi kununua haki za kupeperusha mechi za michuano hiyo.