‘Tuko tayari kuzungumza na Rwanda kidiplomasia,kisiasa na ikibidi hata kijeshi'-Msemaji wa rais Tshisekedi
DRC na Rwanda zimekuwa zikirushiana cheche za maneno na lawama kuhusu kiini cha machafuko mashariki mwa Congo
Moja kwa moja
‘Tuko tayari kuzungumza na Rwanda kidiplomasia,kisiasa na ikibidi hata kijeshi-Msemaji wa rais Tshisekedi
Maelezo ya sauti, Rwanda na DRC zajibizana kuhusu mzozo unaoendelea mashariki kwa Congo Huku mazungumzo ya kuleta amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yakiendelea jijini Nairobi,viongozi wa DRC na Rwanda wamekuwa wakirushiana cheche kali za maneno kuhusu kiini cha mgogoro na machafuko mashariki mwa Congo.
Siku moja tu baada ya rais wa Rwanda Paul Kagame kudai kwambamwenzake wa DR Congo Felix Tshisekedi anatumia mzozo huo kwa sababu za kisiasa,upande wa DR Congo umetoa majibu kwa kauli zake.
Mwandishi wa BBC Caro Robi amezungumza na msemaji wa rais Tshisekedi Tina Salama ambaye amesema nchi yake inaunga mkono juhudi za kuleta amani katika eneo hilo lakini amezidi kuionyooshea Rwanda kidole cha lawama kwa kuliunga mkono kundi la M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Rwanda na nchi jirani ya Uganda zimekana vikali kuyaunga mkono makundi yenye silaha na kuhusika na wizi wa madini nchini DR Congo .

Unaweza pia kusoma
Kombe la Dunia 2022: Luis Suarez akataa kuomba msamaha kwa kuushika mpira wa Ghana 2010

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambulizi wa Uruguay Luis Suarez amekataa kuomba radhi kwa mpira wake wa mkono dhidi ya Ghana katika Kombe la Dunia 2010.
Suarez alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza katika robo fainali kwa kuwanyima Black Stars bao kwa kuupiga mpira wa mikono wavuni kwa makusudi.
Asamoah Gyan alikosa penalti iliyofuata na Uruguay wakapiga hatua inayofuata kwenye mechi hizo.
"Mchezaji wa Ghana alikosa penalti, sio mimi," alisema Suarez kabla ya timu hizo kukutana katika mechi ya Kundi G siku ya Ijumaa katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Ghana inacheza na Uruguay ikijua ushindi utawapeleka katika hatua ya mtoano - lakini kushindwa kutaifanya timu hiyo ya Amerika Kusini kusonga mbele ikiwa Korea Kusini itaskosa kuishinda Ureno.
Iwapo Uruguay na Korea Kusini zote zitashinda, tofauti ya mabao - na ikiwezekana mabao - yataamua hatima yao, huku timu hiyo ya Asia ikiwa na faida ya bao moja.
Ni mara ya kwanza kwa mataifa hayo kukutana tangu mchezo huo miaka 12 iliyopita, na mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Suarez hakuomba msamaha licha ya kuambiwa na mwandishi wa habari wa Ghana kwamba baadhi ya nchi za Afrika wanamwona kuwa ni “shetani wa kweli”.
Wakimbizi wapenzi wa jinsia moja Kenya wahofia usalama wao kambini,

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Kumeripotiwa visa vya unyanyasaji wa wakimbizi wanaoshiriki mapenzi ya jinsia katika kambi hiyo katika miaka michache iliyopita. Wakimbizi wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (LGBT) katika kambi moja kubwa nchini Kenya wanaomba kuhamishwa kwa kile walichokitaja kuwa ni ongezeko la ubaguzi na unyanyasaji unaofanywa na wakimbizi wengine dhidi yao katika kambi hiyo kwa sababu ya mwelekeo wao wa kijinsia.
Mmoja wa wakimbizi hao, ambaye aliomba jina lake lisitajwe kutokana na hofu ya kutokea mzozo zaidi, aliambia BBC "hatujisikii salama tena kambini".
Kakuma inaendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na ni mojawapo ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi nchini Kenya, inayohifadhi maelfu ya wakimbizi wa ndani, pamoja na wale kutoka nchi jirani.
Wiki iliyopita kulikuwa na maandamano ya makundi ya LGBT katika kambi hiyo, ambayo yalilalamikia unyanyasaji na unyanyasaji dhidi yao, ambayo ilisababisha kukamatwa kwa muda kwa watu 18, ugomvi, na matumizi ya gesi ya machozi.
Wote waliozuiliwa waliachiliwa siku iliyofuata baada ya maafisa wa UNHCR kujadiliana kuachiliwa kwao.
"Tumechoshwa, Kakuma si salama tena kwetu sisi wanachama wa jumuiya ya LGBTQI. Tunatishiwa. Tumetoa malalamiko kwa UNHCR na hakuna hatua iliyochukuliwa," alisema mkimbizi huyo.
Wanadai kuwa ubaguzi na unyanyasaji huo umewafanya kushindwa kupata huduma za kijamii kama vile elimu na matukio yanayofanyika katika kambi hiyo kwa sababu hawaruhusiwi kujumuika jamii nyingine.
Msemaji wa UNHCR aliiambia BBC kwamba shirika hilo limekuwa likifanya kazi na jumuiya ya LGBT katika kambi hiyo ili kuwahakikishia usalama wao kwa kuongeza doria ya polisi wanakoishi na kufanya kazi, pamoja na watu wa kujitolea kusaidia na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya usawa na ulinzi wa haki za watu hao.
Papa kuzuru DR Congo na Sudan Kusini mwaka ujao

Chanzo cha picha, Getty Images
Safari ya Papa Francis katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini imeratibiwa tena mapema mwaka ujao, Vatican imetangaza.
Papa atazuru nchi hizo mbili kati ya Januari 31 na 5 Februari, kulingana na taarifa kutoka Vatican.
Ataambatana na Askofu Mkuu wa Canterbury na Msimamizi wa Mkutano Mkuu wa Kanisa la Scotland nchini Sudan Kusini ambako atatumia siku mbili za mwisho za safari yake, ilisema.
Safari ya Papa katika nchi hizo mbili ilikuwa imepangwa kufanyika Julai mwaka huu lakini ilikatishwa kwa sababu ya matatizo yake ya kiafya.
Atakuwa mwenyeji wa marais wa mataifa hayo mawili na pia atakutana na maaskofu, makasisi wengine na wanachama wa mashirika ya kiraia katika nchi zote mbili. Nchini Sudan Kusini, anatarajiwa pia kukutana na wakimbizi wa ndani.
Hawick High: Shule iliyosomesha washindi wawili wa Tuzo ya Nobel

Maelezo ya picha, Sir Angus Deaton na Richard Henderson walirejea katika shule yao ya zamani baada ya zaidi ya miaka 50 r Wawili hai kati ya watano wa Uskochi wa Tuzo ya Nobeli wamerejea katika Shule ya malazi kwa mara ya kwanza baada ya miaka zaidi ya 50.
Sir Angus Deaton kutoka Chuo kikuu cha Princeton na Richard Henderson kutoka Chuo kikuu cha Cambridge walitembelea madarasa yao katika shule ya sekondari ya Hawick waliposomea.
Walikutana na wanafunzi na waalimu na kujadili kuhusu safari yao ya kielimu.
Mwalimu mkuu Vicky Porteous alisema: "Kwangu mimi, kukutana na wanasayansi niwapendao imenifurahisha sana."

Wanaume hawa wote walizaliwa Edinburgh lakini wakahamia katika shule hiyo ya malazi wakati wa utoto wao.
Sir Angus alitunukiwa Tuzo ya Nobel mwaka 2015 kwa kazi yake ya sayansi ya uchumi Bw Henderson, alitunukiwa Tuzo ya Nobel mwaka 2017 ya kemia.
Kabila la watu wa asili ya Afrika washiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza India

Chanzo cha picha, @ECISVEEP/BBC Gujarat
Kwa mara ya kwanza katika jimbo la Gujarat, nchini India kituo cha kupigia kura cha kikabila kimewekwa katika jamii ya Siddi , ambao walihamia India wakitoka Afrika.
Watu wa jamii ya Siddi waliokuwa wamevaa mavazi yao ya kitamaduni waliwasili katika kituo hiki cha kupigia kura kilichojengwa katika kijiji cha Jambur katika manispaa ya Talala iliyopo katika wilaya ya Gir Somnath.

Chanzo cha picha, @ECISVEEP
Wakizungumzia kuhusu kituo cha kupigia kura, wakazi hao wenye asili ya Afrika walilismbia shirika la habari ANI, “Ni suala la kujivunia kwetu sisi kwamba Tume ya Uchaguzi imeandaa kituo maalum kwa ajili yetu cha kupiga kura. Tumekuwa tukiishi hapa kwa miaka mingi, lakini hii ni mara ya kwanza kupewa kituo cha aina hii .”
Wanashiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa bunge la mji wa Talala wa wilaya ya Gir Somnath, ambako shughuli ya uchaguzi zinaendelea.
Elon Musk kufanya majaribio ya kifaa cha kuwezesha ubongo wa binadamu kuwasiliana na kompyuta

Chanzo cha picha, Getty Images
Bilionea wa teknolojia Elon Musk amesemaleo kwamba moja ya kampuni zake itaweza katika miezi sita kuwa na uwezo wa kupandikiza kifaa kwenye ubongo wa mwanadamu kitakachoruhusu mawasiliano na kompyuta.
Kifaa hicho kilichotolewa na kampuni ya Neuralink ya Musk, kitaruhusu mtumiaji kuwasiliana moja kwa moja na kompyuta kupitia mawazo yao, alisema.
"Tumewasilisha nadhani karatasi zetu nyingi kwa FDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani) na tunafikiri pengine katika muda wa miezi sita tunapaswa kuwa na Neuralink yetu ya kwanza katika binadamu," alisema katika wasilisho la kampuni.
"Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii ili kuwa tayari kwa mwanadamu wetu wa kwanza mwenye kipandikizi hiki (implant), na ni wazi tunataka kuwa waangalifu sana na hakika kwamba itafanya kazi vizuri kabla ya kuweka kifaa ndani ya mwanadamu," alisema.
Musk -ambaye alinunua Twitter mwezi uliopita na pia anamiliki SpaceX, Tesla na makampuni mengine kadhaa - amejulikana kutoa utabiri mkubwa kuhusu kampuni zake na nyingine hazikuwa za kwelis.
Mnamo Julai 2019, aliapa kwamba Neuralink itaweza kufanya majaribio yake ya kwanza kwa wanadamu mnamo 2020.
Mifano hiyo, ambayo ni saizi ya sarafu, imepandikizwa kwenye mafuvu ya kichwa cha nyani.
Katika wasilisho la Neuralink, kampuni hiyo ilionyesha nyani kadhaa "wanacheza" michezo ya msingi ya video au kusongesha mshale kwenye skrini kupitia kipandikizi chao cha Neuralink.
Musk alisema kampuni hiyo itajaribu kutumia vipandikizi hivyo kurejesha uwezo wa kuona na kusonga kwa binadamu.
"Hapo awali tungemwezesha mtu ambaye karibu hana uwezo wa kusongesha misuli yake ... na kuwawezesha kutumia simu zao haraka kuliko mtu ambaye ana mikono ya kufanya kazi," alisema.
"Japo inaweza kusikika kama miujiza, tuna imani kuwa inawezekana kurejesha utendakazi kamili wa mwili kwa mtu ambaye amekatwa uti wa mgongo," alisema.
TPLF kusalimisha silaha nzito - Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images
Balozi wa Ethiopia nchini Kenya amesema kuwa kundi la waasi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) litasalimisha silaha zake nzito siku ya Jumamosi kufuatia mazungumzo kati ya makamanda wakuu wa jeshi na TPLF.
Balozi Bacha Debele alitoa tangazo hilo katika video iliyowekwa kwenye YouTube.
“Kuhusu kusalimisha silaha nzito walitakiwa kuzisalimisha tarehe 17 Novemba, lakini hilo halikutekelezwa lakini sasa imeamuliwa wazisalimishe tarehe 3 Desemba,” alisema.
Bw Bacha alisema makamanda wa uwanja wa vita "wanakutana kila siku" kujadili mchakato wa kupokonya silaha na wapiganaji wa TPLF wanakusanywa katika maeneo maalum.
"Taarifa nilizozipata leo zinaonyesha kuwa shughuli zimeanza kuwakusanya [wapiganaji wa TPLF] katika maeneo yaliyotengwa. Wanatekeleza [mchakato huu wa kupokonya silaha]," aliongeza.
Balozi huyo pia alisema itakuwa jambo la aibu kuzungumzia hadharani kuhusu gharama ya binadamu ya vita hivyo.
Serikali ya Ethiopia na TPLF zilitia saini makubaliano ya amani nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu ili kumaliza kwa amani vita hivyo vya miaka miwili.
Unaweza pia kusoma
Ngozi Fulani: Tukio la ubaguzi wa rangi Buckingham lilikuwa unyanyasaji, asema bosi wa shirika la uhisani

Mkuu mmoja mweusi wa shirika la uhisani la Uingereza ambaye aliulizwa mara kadhaa alikotoka "hakika" mmoja wa waliokuwa watumishi wa muda mrefu wa Malkia, Lady Susan Hussey, ameiambia BBC kuwa tukio hilo lilikuwa "unyanyasaji".
Ngozi Fulani aliulizwa kuhusu historia yake katika hafla ya Jumba la Buckingham mnamo Jumanne. Tayari mhudumu huyo wa zamani wa Malkia amejiuzulu.
Bi Fulani alilinganisha mazungumzo na Lady Hussey, 83, na "mahojiano".
Buckingham ilielezea matamshi hayo kuwa "hayakubaliki na ya kusikitisha sana".
Na msemaji wa Prince William alisema "ubaguzi wa rangi hauna nafasi katika jamii yetu". Tukio hilo limeghubika ziara ya Mwanamfalme huyo na mkewe nchini Marekani ili kutoa tuzo kwa ajili ya Tuzo yake ya Earthshot.
Lady Hussey, ambaye alikuwa msiri wa karibu wa marehemu Malkia na aliandamana naye kwenye mazishi ya Duke wa Edinburgh, ameomba msamaha.
Bi Fulani, ambaye alianzisha shirika la kuzuia unyanyasaji wa kinyumbani la Sistah Space, alikanusha madai kwamba matamshi ya Lady Hussey yana uhusiano wowote na umri wake.
"Hebu tufafanue wazi hii ni nini. Nimesikia mapendekezo mengi sana kuhusu umri wake na mambo kama hayo, na nadhani hiyo ni aina ya dharau - aina ya suala la umri," aliambia kipindi cha Today cha BBC Radio 4.
"Ilikuwa kama kuhojiwa. Hiyo ndiyo njia pekee ninayoweza kuielezea."
Wakenya wakimbilia mikopo ya serikali saa chache baada ya kuzinduliwa

Chanzo cha picha, William Ruto / Twitter
Zaidi ya Wakenya milioni moja wamejiandikisha kwa mpango wa mikopo ya serikali inayolenga vijana na wafanyabiashara wasio rasmi siku moja tu baada ya kuzinduliwa.
Mpango huo, unaojulikana kama Hustler Fund, ulizinduliwa na Rais William Ruto Jumatano na tayari ametoa zaidi ya shilingi 400m ($3.3m; £2.7m) kwa wakopaji.
Vyombo vya habari vya ndani vilimnukuu waziri wa vyama vya ushirika akitoa mfano wa kuchukuliwa kwa mikopo hiyo, na hadi miamala 600 kwa sekunde, saa baada ya uzinduzi - ambao ulipungua baadaye.
Wakopaji wanaweza kupata pesa kwa kupiga nambari ya USSD au kutumia programu kwenye simu zao za rununu.
Mikopo hiyo inaanzia kati ya $4 (£3) na $408 kwa wakopaji binafsi. Mikopo kwa vikundi na biashara ndogo itazinduliwa baadaye.
Wakopaji wanatarajiwa kurejesha mkopo ndani ya siku 14, na riba ya kila mwaka ya 8% iliyohesabiwa kwa siku itatozwa.
Hazina hiyo ilikuwa ahadi kuu ya kampeni na rais aliyeingia madarakani mwezi Septemba.
Ameupigia debe mfuko huo unaolenga zaidi ya watu milioni nane kuwa ndio utakaotoa maisha kwa vijana, wanawake na makundi ya watu wa kipato cha chini ambao hawawezi kupata mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa kibiashara.
Mwanajeshi wa Tanzania afariki dunia katika mashambulizi Msumbiji

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wawili wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wameaga dunia nchini Msumbiji.
Wanajeshi hao wamethibitishwa kufariki Novemba 29, 2022 katika kijiji cha Nkonga, Nangade wakati wa mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Ahlu-Sunnah Wa-Jamaa.
Wawili hao wametambuliwa kuwa Sajenti Musa Mpondo wa Tanzania na Koplo Zikamee Kamai kutoka Botswana.
Mwanajeshi mmoja mwingine kutoka Tanzania alipata majeraha kidogo na anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Level ll huko Pemba.
Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SAMIM) umetuma risala za rambi rambi kwa jamaa na familia za wenzao waliopoteza maisha yao.
Aidha, ujumbe huo pia umehakikisha kujitolea kwake kwa ajili ya kurejesha amani na uthabiti katika eneo la Cabo Delgado nchini Msumbiji kwa kukabiliana na aina yoyote ya vurugu mbaya na ugaidi.
Ujumbe huo umethibitisha kwamba idadi kadhaa ya magaidi pia wamepoteza maisha na silaha kadhaa kunaswa.
Pele: Gwiji wa Brazil yuko hospitalini lakini bintiye athibitisha kwamba 'hakuna dharura'

Chanzo cha picha, Getty Images
Gwiji wa Brazil Pele amelazwa hospitalini lakini bintiye amethibitisha kuwa "hakuna dharura" iliyotokea.
Mapema Jumatano, ESPN Brasil iliripoti Pele alikuwa amepelekwa katika Hospitali ya Sao Paulo Albert Einstein akiwa na "uvimbe".
Lakini bintiye Pele Kely Nascimento aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Instagram na kusema kwamba "hakuna chochote kibaya".
Pele aliondolewa uvimbe kwenye utumbo wake mnamo Septemba 2021 na tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu mara kwa mara hospitalini.
"Kuna mengi yazua wasiwasi kwenye vyombo vya habari leo kuhusu afya ya baba yangu, Nascimento alisema.
"Yuko hospitalini akipata matibabu. Hakuna dharura au utabiri mpya mbaya".
Nitakuwa huko kwa sherehe za Mwaka Mpya na ninaahidi kutuma picha kadhaa. ESPN Brasil pia iliripoti kwamba mzee huyo wa miaka 82 alikuwa na matatizo ya moyo na kuna wasiwasi kwamba matibabu yake ya chemotherapy hayana matokeo kama ilivyotarajiwa.
Soma zaidi:
IS yatangaza kifo cha kiongozi wake na kumtaja mtu atakayechukua nafasi yake

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, IS bado inafanya mashambulizi ya hapa na pale huko Iraq na Syria (Picha kutoka maktaba ikionesha mji wa Mosul) Kundi la wanajihadi la Islamic State (IS) limetangaza kifo cha kiongozi wake, Abu al-Hassan al-Hashemi al-Qurayshi.
Ujumbe wa sauti kutoka kwa msemaji wa kundi hilo ulisema aliuawa wakati akipigana na wale aliowaita"maadui wa Mungu", lakini hakutoa maelezo zaidi.
Marekani ilisema aliuawa katika operesheni iliyofanywa na waasi wa Jeshi Huru la Syria kusini-magharibi mwa Syria katikati ya Oktoba.
Alikua kiongozi mwezi Machi, baada ya mtangulizi wake kujilipua wakati wa uvamizi wa majeshi ya Marekani kaskazini-magharibi mwa Syria.
Msemaji huyo alimtaja mbadala wake kuwa ni Abu al-Hussein al-Husseini al-Qurayshi.
Kama ilivyokuwa kwenye tangazo la awali, msemaji huyo alijiepusha kufichua jina lake halisi, utaifa au asili yake.
Alimtaja Abu al-Hussein kama “mmoja wa mujahidin mkongwe” na akawataka wafuasi wa kundi hilo waweke kiapo cha utii kwake.
Kidogo sana kilijulikana kuhusu Abu al-Hassan, ambaye hakuwahi kutoa kauli yoyote kwa jina lake kama kiongozi.
Lakini siku ya Jumatatu, kituo cha Telegram cha kupambana na IS kinachounga mkono kundi hasimu la wanajihadi al-Qaeda kilisema aliuawa "muda fulani uliopita".
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani ilisema katika taarifa yake kwamba Abu al-Hassan aliuawa katika jimbo la kusini-magharibi mwa Syria la Deraa na Jeshi Huru la Syria, kundi mwavuli la makundi ya waasi wanaotaka kumpindua Rais Bashar al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Hakuna jeshi la Marekani lililohusika katika operesheni hiyo, msemaji wa jeshi aliongeza.
IS wakati fulani ilishikilia kilomita za mraba 88,000 (maili za mraba 34,000) kutoka mashariki mwa Iraq hadi magharibi mwa Syria na kuweka utawala wake wa kikatili kwa karibu watu milioni nane.
Kundi hilo lilifukuzwa kutoka eneo lake la mwisho mnamo 2019, lakini UN ilionya mnamo Julai kwamba bado ni tishio la kudumu.
Soma zaidi:
San Francisco yaruhusu utumiaji wa polisi roboti yenye uwezo wa kuua

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Roboti ya kutegua bomu inanyoosha mkono wake Baraza tawala la Wasimamizi wa San Francisco limepiga kura kuruhusu polisi wa jiji hilo kutumia roboti zinazoweza kuua.
Hatua hiyo inawaruhusu polisi kupeleka roboti zilizo na vilipuzi katika hali mbaya zaidi.
Dk. Catherine Connolly, kutoka kundi la Stop Killer Robots, alisema hatua hiyo ni "mwanzo wa kitu kibaya" ambayo inaweza kuwatenga wanadamu na kuuawa.
Polisi wa jiji hilo - SFPD - waliiambia BBC kwa sasa hawatumii roboti zozote zenye nguvu hatari.
Walisema ingawa kunaweza kuwa na hali za siku zijazo ambapo nguvu mbaya inaweza kutumiwa na roboti.
Msemaji wa polisi alisema "roboti zinaweza kuwa na vilipuzi ili kuvunja miundo iliyoimarishwa iliyo na vurugu, silaha, au hatari".
Pia walisema roboti zinaweza kutumika "kulemaza, au kuwakosesha mwelekeo washukiwa wa vurugu, wenye silaha, au hatari ambao wana hatari ya kupoteza maisha".
Mawakili wa hatua hiyo walisema itatumika tu katika hali mbaya zaidi.
Wapinzani, hata hivyo, wanasema mamlaka hiyo inaweza kusababisha jeshi la polisi kuendelea kijeshi.
Hatua hiyo ilipitishwa, na marekebisho siku ya Jumanne yakabainisha kuwa maafisa wanaweza tu kutumia roboti zinazotumia nguvu mbaya baada ya kutumia mbinu mbadala za kupunguza kasi.
Bodi hiyo pia ilieleza kuwa ni idadi ndogo tu ya maafisa wa ngazi za juu wanaoweza kuidhinisha matumizi yake.
Aina hii ya roboti hatari tayari inatumika katika maeneo mengine ya Marekani.
Soma zaidi:
Mwimbaji wa Marekani Jake Flint afariki saa chache baada ya harusi

Chanzo cha picha, FACEBOOK.COM/JAKEFLINTMUSIC
Maelezo ya picha, Jake Flint alichukuliwa kuwa nyota anayechipukia katika muziki wa Oklahoma aina ya 'Red Dirt' Hali ya sintofahamu inaendelea kutanda kuhusu kifo cha mwanamuziki wa taarabu nchini Marekani, Jake Flint, saa chache baada ya harusi yake siku ya Jumapili.
Flint, 37, alifariki usingizini huko Oklahoma, meneja wa zamani Brenda Cline alisema katika chapisho la mtandao wa kijamii.
Heshima zimeanza kumiminika kwa mwimbaji huyo ambaye alichukuliwa kuwa nyota anayechipukia katika muziki aina ya "Red Dirt", aina ya muziki wa taarabu kutoka Oklahoma.
Mke mpya wa Flint, Brenda Wilson Flint, amechapisha video ya wawili hao wakicheza chini ya mti siku ya harusi yao.
"Tunapaswa kupitia picha za harusi lakini badala yake lazima nichague nguo za kumzika mume wangu," aliandika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook.
Wenzi hao walifunga ndoa katika sherehe huko Tulsa siku iliyotangulia.
"Kwa moyo uliovunjika na huzuni kubwa lazima nitangaze kwamba Jake Flint ameaga dunia," meneja wa zamani Brenda Cline aliandika.
"Nimejaribu mara kadhaa leo kuweka ujumbe, lakini huwezi kutoa maoni juu ya kile ambacho huwezi kushughulikia."
Mtangazaji wa muda mrefu Clif Doyal alithibitisha kifo hicho kwa gazeti la Oklahoman, akisema kwamba Flint alifariki usingizini.
"Sidhani kama nimewahi kukumbana na hali ya kushtua kama hii ya kupoteza mtu na jinsi hii ni ukatili kwa Brenda, mke
"Kuwa bibi na mjane katika masaa machache tu haiwezekani."
Red Dirt, aina ya muziki wa taarabu, imepewa jina la rangi tofauti ya udongo katika jimbo la Oklahoma, ambapo Flint alizaliwa katika mji wa Holdenville kabla ya kuhamia Tulsa.
Kagame amshutumu Tshisekedi kwa kutafuta sababu ya Rwanda kuahirisha uchaguzi nchini DR Congo

Chanzo cha picha, RWANDA PRESIDENCY
Maelezo ya picha, Rais Kagame alisema ni "aibu" kwamba vyama vingi na nchi "zinadai kutaka kutatua tatizo hilo", lakini "hazijapata suluhu kwa miongo kadhaa sasa". Rais wa Rwanda Paul Kagame amemshutumu mwenzake wa DR Congo kwa "kujaribu kutafuta njia ya kuahirisha uchaguzi ujao"kwa kuihusisha Rwanda katika mgogoro wa mashariki mwa Congo.
Kinshasa haijajibu mara moja matamshi ya Bw Kagame ambaye bila kuwasilisha ukweli alisema rais wa Congo hakushinda "uchaguzi wa kwanza".
Katika hotuba ndefu nadra siku ya Alhamisi katika Bunge la Rwanda, Rais Kagame alisema ni "aibu" kwamba vyama vingi na nchi "zinadai kutaka kutatua tatizo hilo", lakini "hazijapata suluhu kwa miongo kadhaa sasa".
Bw Kagame alizionya nchi zenye nguvu, akitaja Marekani, Uingereza, Ufaransa, na Umoja wa Mataifa kwa kushutumu au kuamini kwamba Rwanda ndiyo inayohusika na machafuko mashariki mwa Congo, huku akishutumu vikosi vya Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kulitokomeza kundi la waasi la Rwanda la FDLR na wengine.
Pia alikanusha madai kwamba Rwanda ilikuwa ikiiba madini kutoka Congo, "kitu kimoja ambacho sisi sio, sisi sio wezi" alisema.
Alisema madini mengi ya Congo "yalisafirishwa kwa magendo au kupitia njia sahihi" kupitia Rwanda hadi Dubai, Brussels, au Tel Aviv, na Urusi.
"Wanatutuhumu kwa kuiba madini ya Congo vipi kuhusu sehemu yalikowasilishwa? " alihoji.
Bw Kagame alisema Rwanda haiko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba waasi wa M23 sio Wanyarwanda bali ni wa Congo, akilaumu uasi wao kwa serikali ya Kinshasa kwa kutoheshimu makubaliano ya awali na kundi hilo.
Kwa kuihusisha Rwanda, Kagame alimshutumu Bw Tshisekedi, kwamba alikuwa akitengeneza "visingizio vya dharura ili uchaguzi [mwaka ujao] usifanyike".
"Sawa, si kwamba alishinda uchaguzi wa kwanza kama tunavyojua, kama anajaribu kutafuta njia nyingine ya kuahirisha uchaguzi ujao basi ni afadhali atumie visingizio vingine sio sisi", aliongeza bila kuwasilisha ukweli wa madai yake.
Bw Kagame alisema Rwanda inaweza kusaidia katika kushughulikia tatizo la M23 na makundi mengine ya waasi mashariki mwa Congo "kwa sababu tuna nia ya kuwa na ujirani mwema", alisema.
Soma zaidi:
Cyril Ramaphosa: Rais anakabiliwa na tishio la kushtakiwa kwa kashfa ya kuwahonga wezi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anakabiliwa na tishio la kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na Imani naye kutokana na kashfa ya kuwahonga wezi.
Rais ameshutumiwa kwa kuficha wizi wa $4m (£3.3m) kutoka kwa shamba lake mnamo 2020, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara na kuwahonga wezi hao kimya.
Ripoti iliyofichuliwa kutoka kwa jopo huru imegundua kuwa Bw Ramaphosa alitumia vibaya nafasi yake na huenda alivunja sheria ya kupambana na ufisadi.
Hata hivyo, rais huyo amekana kufanya makosa, na kusema pesa hizo zilitokana na kuuza nyati.
Matokeo ya jopo hilo yamekabidhiwa bunge ambalo linatazamiwa kuyachunguza na kuamua iwapo litaanzisha mchakato wa kujadiliwa kwa hoja hiyo au la wiki ijayo.
Bw Ramaphosa amesalia chini ya mwezi mmoja kabla ya kongamano litakaloamua iwapo anaweza kuwania muhula wa pili na chama chake, African National Congress (ANC), mwaka wa 2024.
Tukio hilo linaweza kuwa mbaya zaidi huku Bw Ramaphosa akiwania wadhifa huo.
ANC itafanya mkutano na watendaji wake siku ya Alhamisi, ambapo inatarajiwa kuwa suala hilo litajadiliwa.
Kashfa ya Farmgate ilizuka mwezi Juni, wakati mkuu wa zamani wa jasusi wa Afrika Kusini, Arthur Fraser, alipowasilisha malalamiko kwa polisi akimshtumu rais kwa kuficha wizi wa $4m kutoka kwa shamba lake la Phala Phala kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo mnamo 2020.
Bw. Fraser, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa zamani Jacob Zuma, alidai kuwa pesa hizo zingeweza kuwa mapato ya utakatishaji fedha na ufisadi, na kumshutumu rais kwa kuwateka nyara na kuwahonga wezi hao.
Kushikilia kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa dola kunaweza kukiuka sheria za udhibiti wa fedha za kigeni.
Bw Ramaphosa amethibitisha kuwepo kwa wizi, lakini akasema kiasi kilichoibiwa kilikuwa kidogo kuliko kile kinachodaiwa, na akakana kujaribu kuficha.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja
