Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ujumbe wa Marekani wakutana na Rais mteule wa Kenya William Ruto
Walijadili ‘’ushirikiano wa kimkakati wa Marekani na Kenya, kukuza amani na usalama katika kanda, na njia za kuimarisha uchumi wa [nchi hizo mbili]’’.
Moja kwa moja
Watu wauawa Kharkiv baada ya mashambulizi ya makombora usiku kucha - maafisa
Vikosi vya Urusi vimekuwa vikiendelea kushambulia maeneo ya makazi katika mji wa pili wa Ukraine Kharkiv, huku takriban watu kumi wakiripotiwa kuuawa usiku kucha.
Maafisa wa eneo hilo wanasema watu saba wameuawa katika mashambulizi ya Jumatano jioni.
Watu wengine watatu walikufa katika shambulio la roketi kabla ya alfajiri katika jiji hilo la leo asubuhi, kulingana na huduma za dharura za eneo hilo zilizotajwa na Reuters.
Aliyenusurika Bohdan Oliinyk aliambia shirika la habari kuwa waokoaji walimuokoa mke wake na watoto wawili waliokuwa ndani ya jingo la orofa nne ambalo lilishambuliwa.
‘’Nilikuwa kwenye kochi wakati huo, lakini niliamka dakika tatu kabla ya mlipuko huu na kwenda nje. Labda Mungu aliniokoa kwa namna fulani,’’ Oliinyk alisema.
Soma zaidi:
Uhuru aahidi makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani
Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi alikutana na kufanya mazungumzo na Seneta wa Marekani Chris Coons ambaye alimtembelea katika Ikulu ya Nairobi.
Seneta Coons, ambaye anaongoza ujumbe wa bunge la Seneti na Wawakilishi wa Bunge la Marekani, alimpongeza Rais Kenyatta kwa kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo wakati wa uchaguzi.
“Tunatiwa moyo na amani ambayo Kenya imeendelea kuwa nayo katika kipindi hiki,’’ alisema Seneta Coons.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alisema Kenya itasalia imara katika kusisitizia kanuni za utawala bora ili kuhakikisha nchi inashikilia msimamo wake wa mfano bora wa demokrasia barani kwa kudumisha amani katika kipindi hiki cha mpito’’.
Hamu yangu kuu ni kwamba amani itakuwepo na kuweza kuwa mfano katika bara na ulimwengu,” Rais Kenyatta alisema.
Pia waliokuwepo wakati wa mazungumzo hayo ni pamoja na Waziri mambo ya nje Raychelle Omamo, Waziri wa biashara Betty Maina na Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman miongoni mwa wengine.
Awali, Seneta Coons alifanya mazungumzo na rais mteule William Ruto kuzungumzia uhusiano kati ya Marekani na Kenya.
Mwingine aliyekutana naye ni kinara na Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga kujadili ‘’maadili ya kidemokrasia yanayoshirikishana Kenya na Marekani, kulingana na akaunti ya Twitter ya ubalozi wa Marekani.
Soma zaidi:
India: Mahakama yahalalisha unyanyasaji dhidi ya wanawake kisa 'mavazi yasiyo na maadili'
Na sasa tuelekee nchini India ambapo kulingana na vyombo vya habari vya ndani,
“Mnamo Februari 8 mwaka huu, kulikuwa na malalamiko ya unyanyasaji wa kijinsia katika mkusanyiko uliokuwa umeandaliwa na Chandran na wengine karibu na eneo la Koilandi Kozhikode.
"Mwanamke huyo katika malalamiko yake aliyowasilisha Julai 29 alisema kuwa washiriki walipokuwa wakirejea baada ya mkusanyiko huo, Chandran alimshika na kumgusa isivyofaa,’’ wakili wa mashtaka alisema.
Akitoa dhamana mbele ya Chandran, Jaji alisema, ‘’Picha zilizowasilishwa pamoja na ombi la dhamana la mshtakiwa zinadhihirisha kuwa mlalamikaji mwenyewe alikuwa amevalia mavazi ya kushawishi kingono. Katika kesi hii, kifungu cha 354A hakikubaliani na kesi hiyo dhidi ya mtuhumiwa.’’
Mahakama iliendelea kusema, ‘’Mzee wa miaka 74, mlemavu hawezi kufanya vitendo kwa nguvu. Kwa hiyo, hii ni kesi ya dhamana kwa mshtakiwa,’’ mahakama ilisema.
Mahakama ilisema kuwa ni wazi kutokana na maneno ya kifungu cha 354 kwamba mshtakiwa lazima awe na nia ya kumdhalilisha mwanamke, na ili kesi iwe chini ya kifungu hiki, lazima kuwe na mawasiliano ya kimwili ambayo sio mazuri kimaadili, yenye uashiria ngono ya wazi na maoni ya kingono kama inavyotajwa katika sehemu hiyo.
Chandran alidai kuwa mwanamke huyo alitoa malalamiko ya uwongo dhidi yake.
Zaidi ya hayo, ikibaini kuwa mlalamikaji alikuwa mwanamke msomi ambaye alikuwa anajua vyema madhara ya unyanyasaji wa kijinsia, mahakama ilisema, ‘’Yeye mwenyewe anapaswa kueleza kwa nini alisita kuripoti. Lakini hakuna maelezo yaliyotoka kwake,’’ mahakama ilisema.
Chandran ameshirikisha picha za mlalamishi katika mahakama kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo kuna viongozi wanawake walioonyesha wasiwasi kuhusu agizo la mahakama huku mmoja wao akisema ‘’Mahakama zimehalalisha unyanyasaji dhidi ya wanawake kwa kunyooshea lawama nguo wanazovaa. Hii inasikitisha sana. Hukumu hii itaweka mfano mbaya katika kesi za unyanyasaji wa kijinsia,’’ gazeti la Indian Express limeripoti.
Seneta wa Marekani akutana na Ruto kuzungumzia uhusiano kati ya Marekani na Kenya
Tuliripoti awali kwamba Seneta wa Marekani Chris Coons yuko Kenya kwa ajili ya mikutano na Naibu Rais William Ruto - ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa wiki jana - pamoja na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, anayepinga matokeo.
Mkutano na Rais Uhuru Kenyatta pia uliandaliwa.
Ujumbe wa Marekani jijini Nairobi sasa umeweka kwenye Twitter ujumbe kuwa seneta huyo na Bw Ruto wamekutana.
Walijadili ‘’ushirikiano wa kimkakati wa Marekani na Kenya, kukuza amani na usalama katika kanda, na njia za kuimarisha uchumi wa [nchi hizo mbili]’’.
Akiwa naibu wa rais, Bw Ruto angali na majukumu rasmi ya kutekeleza, lakini kwenye mtandao wa Twitter, hakukutajwa ushindi wa Bw Ruto wala mzozo unaozunguka ushindi wake.
Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi bado haujampongeza naibu rais kwa ushindi wake.
Mapema wiki hii, ilibaini kuwa alitangazwa mshindi na kuipongeza tume ya uchaguzi na Wakenya kwa shughuli ya upigaji kura kwa amani na utulivu.
Odinga akutana na Seneta wa Marekani
Seneta Coons pia amekutana na Bw Odinga kujadili ‘’maadili ya kidemokrasia yanayoshirikishana, kulingana na akaunti ya Twitter ya ubalozi wa Marekani.
Tena, hakukutajwa iwapo uchaguzi huo ulijadiliwa.
Soma zaidi:
Funza tatizo linaloathiri wengi nchini Rwanda,
Ugonjwa wa funza unazidi kusambaa katika Kijiji cha Kabazungu wilaya ya Musanze kaskazini mwa Rwanda.
Wakaazi wanasema ugonjwa huo unasababishwa na uchafu unaotokana naumasikini.
Kuna familia nyingi ambazowatu wake wameathiriwa na ugonjwa wa funza - baadhi hawezi hata kutembea.
Katika miaka ya hivi karibuni, Rais Paul Kagame alisema kuwa tatizo la ugonjwa wa funza linapaswa kutokomezwa kabisa miongoni mwa wananchi.
Katika kijiji hiki, kuna familia ambazo zinaonekana kuathiriwa pakubwa na funza, baadhi wanaona aibu hata kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na hali zao.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 76 ambaye anatembea kwa taabu kutokana na funza aliambia BBC kuwa anashindwa kuwaondoa funzakutokana na ulemavu wake na kwamba hana watoto wala wajukuu wa kumsaidia kuwaondoa kwenye miguu yake.
Katika baadhi ya nyumba, idadi ya watoto walio na funza inaonekana kuwa ni kubwa swala linalowahangaisha majirani zao.
Mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema:
‘’Shida tuliyo nayo ni kwamba watoto wengi hapa ndio walioshambuliwa na funza. Mimi binafsi nilijaribu kuwaondoa funza hao bila mafanikio. Sasa hofu yetu ni kwamba wanaweza kuambukiza hata watoto wetu na pengine sisi wenyewe kutokana na kwamba mayai ya funza yakitapakaa sehemu yote hii hata sisi tutaambukizwa’’
Wakazi hawa wanasema kwamba wanajaribu kutatua tatizo hilo kwa njia ya ushirikiano, lakini hakuna matokeo mazuri.
Mkazi mwingine alisema:
“Hawa watoto hapa nilijaribu kuwaondoa funza mimi mwenyewe na kuwaasa wazazi wao kununua dawa ya kuweka katika vidonda vilivyoachwa na funza kwani na mimi nilihofia kuambukizwa’’.
Meya wa wilaya ya Musanze, Ramuli Janvier hakujibu BBC kuhusu suala hili, siku chache tu zilizopita alisikika akisemakuwa katika eneo hilo zaidi ya watu 50 wameathirika na funza na kwamba mkakati wao ni pamoja na kampeni ya kuwaondoa na kuhusisha kila mtukutoka nyumba moja hadi nyingine.
Umaskini na uchafu?
Wanaougua au kuuguza funza wanasema chanzo ni mazingira ya uchafu na umasikini wa kupindukia katika maeneo wanamoishi baadhi wakiwa bado wanaishi pamoja na mifugo yao.
Mama huyu naye hakutaka jina lake litajwe:
“Kwa hiyo funza wakirudi tutawadhibiti vipi tukiwa tunaishi katika nyumba za aina hii? Nyumba zenyewe hazina kichwa wala miguu, ni vumbi tupu lililojaa hapa na pale, hatuna maji, hatuna pesa za kununua hata sabuni, hivyo uchafu ukiwa mwingi funza pia wanakuja kwa wingi’’
Kwanyakati tofauti rais Paul Kagame alizungumzia swala la ugonjwa wa funza miongoni mwa wananchi huku akiwakemea viongozi wa serikali za mitaa kwa kulifumbia macho na kuonya kwamba litafutiwe ufumbuzi ama viongozi watimuliwa.
Soma zaidi:
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Rais mteule wa Kenya na mpinzani wake kukutana na seneta wa Marekani
Rais mteule wa Kenya William Ruto na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa hivi majuzi Raila Odinga wameratibiwa kukutana na Seneta wa Marekani Chris Coon ambaye yuko katika ziara ya nchi tano za Afrika.
Marekani bado haijampongeza Bw Ruto kufuatia tangazo rasmi kwamba alishinda uchaguzi wa wiki jana.
Bw Odinga amesema hatambui matokeo hayo.
Seneta Coon na ujumbe wake pia watakutana na Rais Uhuru Kenyatta.
Seneta huyo aliwasili katika mji mkuu, Nairobi, Jumatano usiku na atafanya mazungumzo na viongozi hao watatu kuhusu ‘’afya, usalama, na ustawi wa kiuchumi’’, ubalozi wa Marekani ulisema.
Ujumbe huo pia utakutana na wahifadhi, watoa huduma za afya na mashirika yanayofanya kazi kuwawezesha wasichana.
Soma zaidi:
Afghanistan: Mlipuko mbaya zaidi umetokea katika msikiti wa Kabul uliojaa watu
Mlipuko mkubwa umetokea katika msikiti uliokuwa na watu wengi katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul na kuua watu 21, polisi wamesema.
Watu wengine 33 walijeruhiwa, msemaji wa polisi wa Kabul Khalid Zadran alisema.
Mlipuko wa Jumatano ulitokea wakati wa maombi ya jioni.
Imamu wa msikiti huo anaripotiwa kuwa miongoni mwa waliofariki.
Haijulikani ni nani aliyehusika na shambulio hilo, wiki moja baada ya wanamgambo wa Islamic State (IS) kumuua kiongozi wa kidini anayeunga mkono Taliban katika mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga, pia huko Kabul.
Vikosi vya usalama sasa vimefunga eneo la mlipuko huko Kabul.
Mashahidi walielezea kusikia mlipuko mkubwa ambao ulivunja madirisha katika majengo ya karibu.
‘’Niliona watu wengi wameuawa, hata watu walitupwa nje ya madirisha ya msikiti,’’ mtu mmoja aliyeshuhudia aliambia shirika la habari la Reuters.
Stefano Sozza, mkuu wa shirika la matibabu la dharura, linalosimamia hospitali kuu ya jiji hilo, aliiambia BBC kwamba kundi lake tayari limewatibu watu 35, wakiwemo watoto.
‘’Madaktari wetu... waliwapasua [wagonjwa] waliokuwa wakihitaji msaada wa upasuaji usiku kucha. Majeraha yalihusiana zaidi na mlipuko huo kwa hiyo kulikuwa na makombora ndani ya miili na majeraha ya moto katika miili yote ya wahasiriwa’’.
Alisema anaamini mlipuko huo ulitokea ndani ya msikiti huo.
Labda kulikuwa na mtu aliyeingia wakati wa maombi, kwa hivyo kulikuwa na watu wengi wakati huo na kisha [mshambulizi] akatumia kilipuzi. Watu wote waliokuwa karibu na mshambuliaji walifariki na pande zote zimepata majeruhi,’’ Bw Sozza aliongeza.
Waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watuhumiwa kuharibu mtambo muhimu wa kuzalisha umeme
Umoja wa Ulaya na Taasisi ya Uhifadhi wa Mazingira katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamewashutumu waasi wa M23 kwa kupiga makombora na kuharibu kwa kiasi ‘’kikubwa’’ mtambo wa kuzalisha umeme katika mbuga ya wanyama.
Waasi hao wanasemekana kutumia silaha nzito kushambulia Mbuga ya Kitaifa ya Virunga wakati wa mapigano makali na jeshi siku ya Jumanne katika eneo la Rutshuru mashariki mwa DR Congo.
Katika taarifa kwenye Twitter, EU nchini DR Congo ilisema inalaani M23 kwa ‘’hujuma kwenye kituo cha umma kinachotoa umeme kwa wakazi wa Kivu Kaskazini’’.
EU - ambayo inafadhili ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa ajili ya maji kuzunguka mbuga ya Virunga - ilitoa wito kwa M23 ‘’kuweka silaha chini mara moja na kuondoka katika eneo wanalokalia’’.
Tangu Juni, waasi wa M23 wamekuwa wakimiliki maeneo yanayopakana na mbuga hiyo, ambayo ni makazi ya sokwe wa milimani walio hatarini kutoweka.
Taasisi ya Uhifadhi ya Congo iliwataja watu wa eneo hilo wakisema kwamba silaha mbili nzito zilitoka eneo la M23 umbali wa kilomita 5 ili kugonga mtambo huo na kusababisha ‘’uharibifu mkubwa wa nyenzo’’.
Taasisi hiyo ilisema hakuna mfanyakazi wao aliyedhurika kwani walihamishwa wakati mapigano hayo yalipotokea, lakini inaongeza kuwa ‘’kulikuwa na waathiriwa wengi katika vijiji vinavyozunguka’’.
Waasi wamekanusha kushambulia kituo hicho, wakisema kuwa vituo vya uhifadhi wa mazingira ‘’sio malengo ya kijeshi’’ ya mashambulizi yao.
Mkuu wa mrengo wa kisiasa wa kundi hilo, Bertrand Bisimwa, alitoa taarifa akisema madai ya taasisi hiyo ‘’yamebiniwa tu’’ ili kuliondoa jeshi na washirika wake kutokana na ‘’kitendo chao cha kutisha’’.
Vyombo vya habari vya ndani vinasema watu sita waliuawa wakati wa mapigano hayo ya Jumanne.
Marekani na Taiwan kuanza mazungumzo rasmi ya biashara
Marekani imetangaza kuwa itaanza mazungumzo rasmi ya kibiashara na Taiwan, wiki kadhaa baada ya ziara yenye utata ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi.
Duru ya kwanza ya mazungumzo inatarajiwa kuanza "mapema msimu wa joto", alisema Mwakilishi katika Ofisi ya Biashara Marekani Majadiliano yao yatajumuisha mazungumzo kuhusu kuwezesha biashara, biashara ya kidijitali na viwango vya kupambana na ufisadi.
Uhusiano kati ya Marekani na China umezidi kuwa mbaya kufuatia ziara ya Pelosi ya Taiwan. Mpango wa Marekani na Taiwan kuhusu Biashara (The US-Taiwan Initiative on 21st Century Trade) ulizinduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Juni, na pande zote mbili sasa zimesema zimefikia makubaliano.
"Tunapanga kufuata ratiba kabambe.... ambayo itasaidia kujenga uchumi wa karne ya 21 ulio bora zaidi, wenye ustawi zaidi na thabiti," alisema Naibu Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Sarah Bianchi katika taarifa yake.
Biashara kati ya Marekani na Taiwan ilikuwa na thamani ya karibu $106bn (£88bn) mwaka 2020. Tangazo hilo linakuja wakati China ikizindua mazoezi yake makubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kutokea karibu na Taiwan baada ya ziara ya Pelosi mapema mwezi Agosti.
Chini ya "sera ya China Moja", Marekani inatambua na ina uhusiano rasmi na China badala ya kisiwa cha Taiwan lakini inadumisha uhusiano "usio rasmi" na Taiwan, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuuza silaha kwa kisiwa hicho ili iweze kujilinda.
Soma:
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Ujumbe wa Marekani kukutana na Uhuru, Ruto na Raila jijini Nairobi
Ujumbe kutoka nchini Marekani unatarajiwa kukutana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto (Rais mteule) na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
Ujumbe huo unaongozwa na Seneta wa Delaware Chris Coons uliwasili nchini usiku wa Jumatano ulipokelewa na Balozi wa Marekani Meg Whitman.
Ujumbe huo uko katika ziara rasmi katika nchi tano za Afrika.
"Ni jambo la kustaajabisha kukaribisha ujumbe unaoongozwa na Seneta Chris Coons, ni kituo cha tatu katika ziara ya nchi tano barani Afrika!
Ujumbe huo utakutana na wahifadhi wa mazingira, watoa huduma za afya na mashirika yanayofanya kazi kuwawezesha wasichana," Whitman aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Haya yanajiri siku chache baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) Wafula Chebukati, kumtangaza William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022.
Ujumbe huo pamoja na mambo mengine utajadili masuala ya malengo ya pamoja, ikiwa ni pamoja na afya, usalama na ustawi wa kiuchumi.
Unaweza pia kusoma
Msanii wa Nigeria 'kujibu mashtaka' ya kumtemea mate polisi
Msanii wa Nigeria Buju BNXN atakuwa na maswali ya kujibu baada ya kujigamba kwenye mtandao wa Twitter jinsi alivyomtemea afisa wa polisi mate usoni, polisi wamesema.
Mwanamziki huyo, ambaye jina lake halisi ni Daniel Benson, amefuta ujumbe huo mtandaoni.
Msemaji wa polisi wa jimbo la Lagos alisema nyota huyo " bila shaka atajibu shambulio lake dhidi ya afisa wa polisi".
"Maafisa wa polisi watawajibishwa kwa tabia zao mbaya ikiwa itathibitishwa," Benjamin Hundeyin alisema kwenye ujumbe wa Twitter.
Vyombo habari nchini humo vinaripoti kwamba mwanamuziki huyo alihusika katika mabishano na maafisa wa polisi siku ya Jumatano alasiri - jambo ambalo huenda lilimfanyaa ashirikishe ujumbe huo mtandaoni.
Video ya makabiliano hayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Rais mteule wa Kenya William Ruto ana mamlaka gani?
Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais nchini Kenya mchakato wa makabidhiano wa madaraka ulianza .Hata hivyo ,hatua ya muungano wa Azimio kupinga matokeo inapunguza kasi ya kuapishwa kwa rais mteule WilliamRuto na kuongeza muda wa kuhudumu kwa rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta.
Lakini je,wawili hao wana mamlaka yapi?
- Rais siku hiyo aliingia kwenye awamu ya "Uongozi wa muda" maana yake atakuwa ameshikilia kiti kama kiongozi wa muda akijiandaa kumkabidhi Mkuu wa nchi ajaye.
- Sura ya Tisa (9), Sehemu ya Pili (2), Ibara ya 134 ya Katiba ya Utekelezaji wa Madaraka ya Urais Wakati wa Uongozi wa Muda inasema Mkuu wa Nchi anayemaliza muda wake anapoteza mamlaka ya kuteua majaji wa Mahakama za Juu.
- Wakati huo huo, rais anapoteza mamlaka ya kuteua afisa yeyote wa umma; kuteua au kumfukuza kazi waziri (CS), Katibu wa kudumu (PS) na maafisa wengine wa Serikali.
- Pia anasalimisha mamlaka ya kuteua, kuchagua au kutengua kamishna mkuu, balozi, au mwakilishi wa kidiplomasia au ubalozi.
- Rais pia amenyimwa uwezo wa kutumia nguvu ya huruma, maana yake hawezi kuwasamehe wafungwa.
- Kenyatta pia ataacha mamlaka ya kutoa heshima kwa jina la wananchi na Jamhuri.
- Kipindi cha "uongozi wa muda" huanza siku ambayo Wakenya watapiga kura na kinaisha wakati rais mpya aliyechaguliwa anaanza kutekeleza majukumu yake.
Rais mteule ana mamlaka gani?
Kabla ya kuapishwa rasmi kuchukua hatamu za uongozi ,rais mtele hana mamlaka ya kuweza kuteua au kumfuta kazi afisa yeyote wa serikali .
Hata hivyo pindi anapothibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais,ulinzi wake huimarishwa pamoja na wa familia yake .
Pia huanza kupewa taarifa za kiusalama na vyombo husika .Teuzi anazoweza kufanya ni katika kundi lake la maafisa wanaojitayarisha kuingia katika utawala wake ambao hushirikiana na kamati ya makabidhiano .
Hata hivyo mamlaka hayo ni ndani ya kundi lake na sio ya kikatiba .
Pindi anapokula kiapo na kuwa rais,yeye hupata mamlaka kamili ya mkuu wa nchi na mkuu wa majeshi ya ulinzi wa taifa .
Unaweza pia kusoma
Mauaji ya kimbari Rwanda: Tarehe ya kuanza kwa kesi ya Félicien Kabuga yawekwa
Kesi ya mfanyabiashara wa zamani anayeshukiwa kuwa mmoja wa wahusika wakuu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda itaanza tarehe 29 Septemba, mahakama imeamua.
Félicien Kabuga mwenye umri wa miaka 87 alifikishwa katika mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) mjini Hague kwa ajili ya kusikilizwa kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Alizuiliwa nchini Ufaransa miaka miwili iliyopita baada ya kuwa mafichoni kwa zaidi ya miongo miwili.
Katika miaka ya 1990, Bw Kabuga alikuwa rais wa kituo cha redio cha Radio Television Libre des Mille Collines, ambacho kilitangaza wito wa kuuawa kwa Watutsi.
Anatuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Atashtakiwa katika mahakama ambayo ni mrithi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda, iliyomaliza kazi yake nchini Tanzania mwaka 2015.
Mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda yalisababisha mauaji ya Watutsi 800,000 na maelfu ya Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Soma:
Mali yaishtumu Ufaransa kwa kutuma silaha kwa wanamgambo
Uhusiano kati ya Ufaransa na Mali umeendelea kuzorota, huku nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikishutumu mamlaka yake ya zamani ya kikoloni kwa kusambaza silaha na taarifa za kijasusi kwa wanamgambo wanaoipinga serikali.
Katika barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop anasema Ufaransa imekiuka anga yake mara kadhaa na kuwasilisha silaha kwa wapiganaji wa Kiislamu katika jaribio la kuiyumbisha nchi yake.
Ufaransa imepinga tuhuma hizo.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umevunjika kufuatia mapinduzi mawili na uamuzi wa watawala wa kijeshi wa Mali kufanya kazi kwa karibu na mamluki kutoka Urusi.
Siku ya Jumapili, Ufaransa ilisema wanajeshi wake wote sasa wameondoka Mali, ambako wamekuwa wakipambana na wanamgambo wa Kiislamu kwa takriban miaka 10.
Mgombea ugavana wa ODM apinga kuahirishwa kwa uchaguzi Mombasa
Mmoja wa wagombea wa kiti cha ugavana katika kaunti ya Mombasa pwani ya Kenya amepinga hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika Agosti 23.
Abdulswamad Sharif Nassir Mgombea wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) amesema ataenda mahakamani kupinga uamuzi huo akidai kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC) Wafula Chebukati hakuwashauri wagombea kabla ya kufikia uamuzi huo.
''Kuna mambo matatu tu ambayo yanaweza kufanya uchaguzi kuahirishwa nayo ni ukosefu wa usalama wa hali ya juu, kuvunjwa kwa kanuni za uchaguzi na janga la kitaifa...mambo haya hayajashuhudiwa Mombasa,'' alisema.
Akizungumza na wandishi wa habari Bw Sharif alisema: ''Sheria iko wazi... hauwezi tu kuinuka na kusema leo kuwa hakuna uchaguzi ...kisha ni vipi wenzetu wanajua mapema zaidi kuwa kura zitabadilishwa''
Hapo jana ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kusema kwamba tarehe mpya ya chaguzi hizo zitachapishwa katika gazeti ramsi la serikali hivi karibuni.
Shambulio la msikiti Kabul : 'Inahofiwa kuna majeruhi wengi’
Mlipuko huo unaodhaniwa kuwa ulitokea wakati wa sala ya jioni (magharibi), uliwauwa watu wapatao watatu na kuwajeruhi wengine makumi kadhaa, kulingana na shirika lisilo la kiserikali la huduma za dharura.
Msemaji wa polisi katika mji mkuu Kabul, Khalid Zadran, alinukuliwa na mitandao ya kijamii akisema kuwa mlipuko huo ulitokea katika eneo la kaskazini- magharibi mwa mji.
Taarifa zinasema kuwa imamu wa msikiti wa Siddiqi alikuwa miongoni mwa wale waliofariki.
Haijawa wazi ni nani aliyepanga na kutekeleza shambulio hilo, ambalo linakuja wiki mmoja baada ya kiongozi wa kidini anayewaunga mkono -Taliban kuuawa katika mlipuko wa bomu la kujitolea muhanga, ambalo pia lilitokea mjini Kabul. Kikundi cha Islamic State (IS) kilidai kuwajibika na shambulio la awali.
Unaweza pia kusoma:
- Afghanistan: Nini kimebadilika mwaka mmoja baada ya Taliban kurudi
- Afghanistan: Mlenga shabaha wa Taliban ambaye sasa anafanya kazi ofisini
- Rubani wa Afghanstan aliyewapatia Taliban helikopta ya kivita
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Polisi wa wanachunguza vurugu zilizoshuhudiwa Bomas
Siku chache baada ya Tume ya Uchaguzi nchini Kenya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais, polisi nchini humo wanachunguza vurugu zilizoshuhudiwa katika ukumbi wa Bomas – kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura za wagombea urais kitaifa.
Katika taarifa ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wake rasmi wa Twitter u siku ya Jumatano Agosti 17, 2022, ilisema Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) inachukua fursa hii kuwafahamisha umma kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye uchunguzi wa matukio mawili yanayohusiana na Uchaguzi Mkuu.
"Kwa hivyo, Huduma ya Kitaifa ya Polisi inawaomba wananchi kujitolea kutoa taarifa za siri ambazo zitasaidia katika uchunguzi wa matukio hayo mawili," taarifa hiyo ilisomeka kwa sehemu.
Pia iliongeza kuwa faili za CCTV tayari zimekusanywa na kutumwa kwa Idara Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kisheria ili kusaidia katika uchunguzi huo.
Hatua hii inajiri saa chache baada ya mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati kukashifu kisa hicho akisema kuwa wafanyikazi wake walinyanyaswa kwa sababu waliamua kutopendelea wakati wakitekeleza majukumu yao katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura.
Chebukati pia aliyataja madai yaliotolewa na makamishna wanne wa tume hiyo kama ya uwongo akiongeza kwambamakamishena hao walijaribu kulazimisha kufanyika kwa kura ya marudio kinyume na kiapo cha utendakazi walichokula katika tume hiyo.
Aidha alisema kwamba uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na uwazi wa kiwango cha juu zaidi ya chaguzi zozote zile zilizoandaliwa na tume hiyo.
Maelezo zaidi:
Hujambo na karibu