China imechukua hatua kuonyesha hasira yake kwa Marekani

Serikali ya China imetangaza kuwa imesitisha mazungumzo muhimu ya hali ya hewa na Marekani, pamoja na ushirikiano katika maeneo mengine mengi.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo.

  2. Raila na Ruto wafanya kampeni zao za mwisho mwisho pwani ya Kenya,

    Azimio la Umoja wakifanya mkutano wao wa kampeni pwani ya Kenya
    Maelezo ya picha, Azimio la Umoja wakifanya mkutano wao wa kampeni pwani ya Kenya

    Raila Odinga, mgombea urais kutoka Azimio la Umoja yuko eneo la Pwani ya Kenya katika kampeni zake za lala salama.

    Mapema leo hii, Raila alianzia katika eneo la Lamu, Malindi, Kilifi na hatimae kumalizia mjini Mombasa katika uwanja wa Tononoka. Hii ni katika jitihada zake za kujaribu kujipatia kura za mwisho mwisho kuelekea uchaguzi mkuu.

    Hata hivyo, yeye na hasimu wake wa kisiasa katika kinyang’anyiro hicho cha urais, William Ruto kutoka chama cha UDA, wamekuwa wakipishana katika eneo hilo la pwani, ambapo Ruto yeye alikuwa mjini Mombasa hapo jana.

    Haya yanajiri zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, wagombea wawili wakuu wa urais nchini humo wapo katika hatua za mwisho za kampeni. Kuna jumla ya wagombea wanne wanaowania nafasi hiyo ya kuwa rais wa tano wa taifa la Kenya.

    Kila mmoja yuko mbioni kunadi sera zake, katika eneo ambalo linaonekana kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa ajira, migogoro ya ardhi, pamoja na malalamiko ya kuhamishwa kwa shughuli za bandari.

    Wakijaribu kupita mule mule kwenye matatizo ya wananchi, sera ya Azimio la Umoja imekuwa ni ukuaji wa uchumi, elimu bora kwa wote pamoja na huduma bora ya afya.

    Naibu wa rais William Ruto akifanya kampeni Nairobi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Naibu wa rais William Ruto akifanya kampeni Nairobi

    William Ruto ambae pia ni naibu rais katika serikali inayoondoka madarakani, amekuwa akisisitiza kwamba, iwapo serikali yake itapata ridhaa ya wananchi, basi kipaombele chake itakuwa ni kutenga kiasi cha bilioni 50 kwa mwaka kwa ajili ya kutoa mikopo midogo midogo.

    Kilele cha kampeni hizi, kinatarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi.

    Soma zaidi:

  3. Habari za hivi punde, China imechukua hatua kuonyesha hasira yake kwa Marekani

    Balozi wa China nchini Marekani, Qin Gang

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Balozi wa China nchini Marekani, Qin Gang

    China imechukua hatua kuonyesha hasira zake kwa Marekani

    Serikali ya China imetangaza kuwa imesitisha mazungumzo muhimu ya hali ya hewa na Marekani, pamoja na ushirikiano katika maeneo mengine mengi.

    China na Marekani zilizindua makubaliano ya hali ya hewa mwaka jana katika mkutano wa hali ya hewa wa COP26 huko Glasgow.

    Wizara ya mambo ya nje ya China imesema nchi hiyo pia inasitisha mazungumzo kati ya makamanda wakuu wa kijeshi, mazungumzo ya kuzuia uhalifu wa kuvuka mipaka na kuwarejesha makwao wahamiaji haramu.

    Hatua hizi zote zinafuatia ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi nchini Taiwan, jambo ambalo liliikasirisha China.

    Soma zaidi:

  4. Marekani yatoa taarifa kuhusu operesheni ya kijeshi ya China nchini Taiwan

    Serikali ya Marekani imezungumza kuhusu mazoezi ya kijeshi ya China

    Chanzo cha picha, REUTERS/Soe Zeya Tun

    Maelezo ya picha, Serikali ya Marekani imezungumza kuhusu mazoezi ya kijeshi ya China

    Serikali ya Marekani imezungumza kuhusu mazoezi ya kijeshi ya China kwa siku ya pili karibu na kisiwa cha Taiwan.

    ‘’Hatua ya kijeshi ya China ni kubwa, ina athari, na bila uhalali wowote inasababisha mgogoro,’’ Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema.

    ‘’Hakuna uhalali kwa matendo yao’’, aliendelea Blinken, akizungumza katika mkutano wa Asia.

    China ilijibu ziara ya hivi majuzi nchini Taiwan na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi.

    Ziara hiyo ambayo serikali ya Beijing ilikuwa imeonya kwa muda, na kufuatiwa na operesheni za kijeshi ambazo zimetatiza pakubwa Taiwan.

    Marekani ilichukua hatua gani dhidi ya China?

    Balozi wa China nchini Marekani, Qin Gang, aliitwa Ikulu ya Marekani jana kuhusu suala la nchi hiyo, kwa mujibu wa gazeti la Washington Post.

    ‘’Kufuatia hatua za Uchina, tumemwita Balozi Qin Gang kwenye Ikulu ya White House kuelezea vitendo vya uchochezi vya PRC [Jamhuri ya Watu wa Uchina],’’ msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby aliambia gazeti hilo.

    Hatua hiyo, inachukuliwa kuwa maandamano ya kidiplomasia.

    Kirby aliongeza kuwa utawala wa Biden umekosoa hatua za kijeshi za China, ‘’ambazo ni kutowajibika dhidi ya lengo letu la muda mrefu la kudumisha amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan’’.

  5. Ukraine: Watoto 359 wamefariki kutokana na mashambulizi ya Urusi - Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu

    Liza Dmitrieva mwenye umri wa miaka 4 alikua mwathirika wa shambulio la Urusi huko Vinnytsia mnamo Julai 14.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Liza Dmitrieva mwenye umri wa miaka 4 alikua mwathirika wa shambulio la Urusi huko Vinnytsia mnamo Julai 14.

    Watoto 359 walifariki dunia kutokana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine.

    Zaidi ya wengine 700 walipata majeraha ya viwango tofauti, ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu inaripoti.

    ‘’Idadi hizi sio za mwisho, kwani kazi inaendelea na kutafuta miili katika maeneo yenye uhasama mkali, yale yaliyokaliwa kwa muda na yaliyokombolewa,’’ idara hiyo inabainisha.

    Watoto walioathiriwa zaidi walikuwa katika mkoa wa Donetsk - 371, mkoa wa Kharkiv - 195, mkoa wa Kyiv - 116, mkoa wa Chernihiv - 68, mkoa wa Luhansk - 61, mkoa wa Mykolaiv - 57, mkoa wa Kherson - 54, mkoa wa Zaporizhia - 40.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu pia iliripoti kwamba taasisi za elimu 2,211 ziliharibiwa kwa sababu ya mabomu na makombora na jeshi la Urusi tangu Februari 24.

    Kati yao, 230 waliharibiwa kabisa.

    Soma zaidi:

  6. DR Congo kufanya mazishi ya wahanga wa maandamano dhidi ya Umoja wa Mataifa

    Takriban watu 19 wakiwemo walinda amani wa Umoja wa Mataifa walifariki katika mapigano hayo

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Takriban watu 19 wakiwemo walinda amani wa Umoja wa Mataifa walifariki katika mapigano hayo

    Takriban watu 19 wakiwemo walinda amani wa Umoja wa Mataifa walifariki katika mapigano hayo

    Mazishi ya waandamanaji waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa.

    Haya yanajiri siku nne baada ya hafla ya kuwaenzi wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao pia walifariki wakati wa maandamano hayo.

    Maandamano yalizuka katika mji wa Goma wiki iliyopita huku raia wakishutumu tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani, Monusco, kwa kushindwa katika misheni yao ya kupambana na makundi yenye silaha.

    Vipeperushi vyenye maneno Bye bye Monusco vimesambazwa kote Goma huku wanaharakati wakitoa wito kwa watu kufunga biashara zao na kuadhimisha siku hiyo kuwakumbuka waliofariki hivi majuzi.

    Wengi wa waliouawa walikuwa chini ya umri wa miaka 30 - mdogo alikuwa mtoto wa miaka 11.

    Vipeperushi pia vinaeleza kuwa maandamano yataendelea hadi Monusco iondoke katika eneo hili.

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani umekuwa ukifanya kazi katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa zaidi ya muongo mmoja na ni ujumbe wa pili kwa ukubwa duniani wa kulinda amani.

    Hata hivyo, wananchi wamesema uwepo wake haujaleta amani, na wangependa kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya nchi peke yao.

    Mapema wiki hii, mwakilishi maalum wa Monusco wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliambia BBC kwamba ujumbe wa kulinda amani utafanyiwa tathmini.

    Mjumbe huyo alisema mpango wa mpito wa taratibu na unaowajibika utawekwa.

    Soma zaidi:

  7. Museveni akanusha kwamba anamtayarisha mwanawe kuchukua wadhifa wa urais

    Museveni asema siku zote Urusi na china zimeingia barani kama marafiki.

    Chanzo cha picha, Presidential Press Unit, Uganda

    Maelezo ya picha, Museveni asema siku zote Urusi na china zimeingia barani kama marafiki.

    Mwanahabari wa BBC Alan Kasujja amepata fursa ya kuzungumza na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

    Kabla ya kuanza mazungumzo yao, walikuwa na muda mfupi wa kutaniana.

    Akizungumza naye kwa kipindi cha BBC cha Africa Daily, alimuuliza kama Uganda inakaribia Urusi na Uchina, na akasema kuwa nchi hizi hazikuwa wakoloni au wafanyabiashara wa utumwa zamani.

    Anasema siku zote wameingia barani kama marafiki.

    Kasujja alipohoji jukumu la upinzani nchini Uganda, alimrudisha nyuma hadi mwaka 1789 - mapinduzi ya Ufaransa na mageuzi ya demokrasia huko Uropa.

    Uganda iko kwenye njia tofauti, Rais Museveni anasema.

    Anapoelezea msimamo wake kuhusu vita vya Ukraine, analinganisha uwepo wa Nato katika Ulaya ya Mashariki na mzozo wa makombora wa Cuba mwaka 1962.

    Alan akaanza kushangaa jinsi majibu hayo yanahusiana na idadi ya vijana ya Uganda inayozidi kuongezeka.

    Zaidi ya 77% ya watu hapa wako chini ya umri wa miaka 30.

    Alan: Kutokana na mazungumzo ambayo nimekuwa nayo wiki iliyopita, yanalenga mahitaji yao ya haraka - iwe wanaweza kumudu kupanda kwa gharama ya maziwa ya watoto, gharama za matibabu na kama kutafuta kazi hapa au kusafiri ng’ambo.

    Rais haoni tofauti hii.

    Ananiambia: “Unachoita historia Bw Kasujja, mimi naita mambo ya sasa.”

    Lakini akiangalia siku zijazo, inaonekana yuko tayari kujihusisha na wazo la mabadiliko.

    Nilimuuliza swali lililoulizwa wakati wa mjadala niliofanya na vijana wasomi katika mji mkuu - ikiwa wanaulizwa kukaza mikanda yao, kwa nini wanasiasa hawawezi kuzuia matumizi yao ya magari makubwa, madereva na safari za watendaji?

    Bw Museveni anasema hilo swali ni sahihi na haki kuulizwa.

    Ninapouliza kwa nini hajatoa mwongozo wa athari hiyo, anasema lingekuwa wazo zuri.

    Katika mada ya kupanda kwa bei ya mafuta, anasema nchi inapaswa kuwa katika mpito kwa magari ya umeme na treni.

    Ingepunguza bei ya bidhaa kwa kila mtu, anaamini.

    Lakini vipi kuhusu hatma yake ya baadaye?

    Alan: Ninashirikishana naye angalizo kwamba viongozi wengi mashuhuri wa Uganda - Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Spika wa Bunge - wanatoka kizazi kipya katika miaka yao ya 40 na ya awali ya 50.

    Ninauliza kama tunashuhudia mwanzo wa mpito wa madaraka.

    “Ndio,” ananiambia, “watu wanakuja. .”

    Anakanusha kuwa anamtayarisha mwanawe - Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kamanda wa vikosi vya ardhini vya Uganda - kuchukua wadhifa wa urais.

    Lakini anasisitiza kwamba kizazi kijacho cha viongozi kinapaswa kutoka katika chama chake, National Resistance Movement.

    Kwa hiyo, baada ya miaka 35 kuongoza nchi, yuko tayari kutumia muda zaidi shambani na ng’ombe wake – pengine kustaafu?

    “Kuna raha sana huko.

    Ningeweza kwenda wakati wowote” anasema “sihitaji kazi”.

    Lakini lazima nimkumbushe…aliniambia vivyo hivyo tulipozungumza mnamo mwaka 2013.

    Soma zaidi:

  8. Moto katika ukumbi wa burudani waua 13 na kuwajeruhi makumi wengineThailand

    moto

    Chanzo cha picha, SAWANG ROJANATHAMMASATHAN RESCUE FOUNDATION

    Watu 13 waliuawa na wengine 41 kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika ukumbi wa burudani mkoa wa Chonburi uliopo kusini -mashariki mwa Thailand.

    Moto ulizuka mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Ijumaa katika klabu ya B nightspot katika wilaya ya Sattahip, polisi walisema.

    Kanda za video zinayosambazwa mitandaoni zinaonyesha watu wanaokimbia klabu wakipiga mayowe, wengine nguo zao zikiwaka..

    Waokoaji wanasema nyenzo zinazoweza kuwaka kwenye kuta huenda kuwa zimezidisha moto.

    Ukumbi huko Chonburi, jimbo lililoko kilomita 150 (maili 90) kusini mwa Bangkok, lilikuwa jengo la ghorofa moja lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800 (futi za mraba 51,660).

    Wazima moto walipambana kwa zaidi ya saa mbili ili kudhibiti moto huo, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Miili ya wahasiriwa - wanawake wanne na wanaume tisa - ilipatikana karibu na lango na bafu.

    Wengine walipatikana karibu na kibanda cha DJ. Kufikia sasa, wote waliofariki wanaaminika kuwa raia wa Thailand.

  9. Ndege 20 za China zenye makombora zilivuka mstari wa mpakani na Taiwan: Ripoti

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndege za kivita za China zilikuwa zikiruka juu ya kisiwa cha Pingtan cha bara - ambacho kiko katika Mlango-Bahari wa Taiwan kutoka kaskazini mwa Taiwan na ni mojawapo ya maeneo ya karibu zaidi katika bara na kisiwa hicho.

    Picha zinaonyesha ndege hizo zikiwa na makombora.

    Watalii katika kisiwa hicho walikuwa wakiziona ndege hizo kwa kutumia darubini.

    China pia ilirusha makombora juu ya Taiwan kutoka Kisiwa cha Pingtan siku ya Alhamisi.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kama tulivyoripoti hapo awali, wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema leo kwamba meli na ndege "nyingi" za China zimevuka mstari wa kati wa Taiwan Strait kwa siku ya pili mfululizo.

    Chanzo cha Taiwan kilichofahamishwa kuhusu suala hilo sasa kimeiambia Reuters kwamba takriban meli 10 za jeshi la wanamaji la China zilivuka mstari wa mpaka na kubaki katika eneo hilo siku ya Ijumaa asubuhi, na takriban ndege 20 za kijeshi za China pia zilivuka eneo hilo kwa muda mfupi.

    Meli za jeshi la majini za Taiwan ziko karibu kufuatilia shughuli za jeshi la wanamaji la China, chanzo kiliongeza.

    Mstari wa ‘kati’ni mstari usio rasmi wa kugawanya mpaka kati ya China bara na Taiwan.

    China yamuwekea vikwazo PelosI

    TH

    Chanzo cha picha, EPA

    China imetangaza kumuwekea vikwazo Spika wa Marekani Nancy Pelosi na familia yake ya karibu katika ziara yake nchini Taiwan.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alisema kuwa Pelosi "ameingilia sana mambo ya ndani ya China, ameharibu vibaya mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya China, akapuuza pakubwa kanuni ya kuwa na China moja, na kutishia pakubwa amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan", kulingana na taarifa.

    China inaiona Taiwan kama jimbo lililojitenga ambalo lazima liunganishwe na bara, kwa nguvu ikiwa italazimu

    Unaweza pia kusoma

  10. Michael E. Langley athibitishwa kuwa jenerali wa kwanza mweusi wa nyota nne wa kikosi cha Marine

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Luteni Jenerali Michael E. Langley atakuwa jenerali wa kwanza wa nyota nne Mweusi katika historia ya miaka 246 ya Wanamaji, baada ya Seneti kuthibitisha kupandishwa cheo kwake wiki hii, Jeshi la Wanamaji lilisema Jumanne.

    Langley atafikia rasmi cheo chake kipya katika sherehe huko D.C. wikendi hii, Wanamaji walisema. Kisha atakuwa mkuu mpya wa Kamandi ya U.S. Africa katika makao makuu yake huko Stuttgart, Ujerumani. Huko, atasimamia askari wapatao 6,000. Rais Biden alimteua mwezi Juni.

    Katika kesi yake ya uthibitisho mwezi uliopita, Langley alimshukuru baba yake - ambaye alihudumu katika Jeshi la Wanahewa kwa miaka 25 - pamoja na mama yake wa kambo na dada zake wawili. "Kama wateule wengi wamesema katika ushuhuda mbele yangu, familia za kijeshi zinaunda msingi wa utayari wetu wa Pamoja," alisema. "Bila msaada wao, nisingekuwa hapa leo."

    Marine Corps imekuwa na majenerali wachache wa nyota tatu Weusi, akiwemo Langley, ambaye alipandishwa cheo hicho mwaka jana. Wamarekani wengine wenye asili ya Kiafrika pia wamepata vyeo vya nyota nne katika matawi mengine, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin, jenerali mstaafu wa Jeshi.

  11. Wahamiaji walengwa nchini Afrika Kusini baada ya ghadhabu ya ubakaji wa genge

    TH

    Chanzo cha picha, AFP

    Wakaazi wa kitongoji cha Afrika Kusini karibu na Johannesburg wamechoma moto nyumba za wahamiaji wanaoamini kuwa wanafanya kazi kinyume cha sheria katika migodi ya ndani ambayo haijatumika.

    Kumekuwa na hasira nyingi baada ya kundi kubwa la wachimba migodi kutuhumiwa kwa ubakaji wa wanawake wanane wiki iliyopita.

    Makumi ya watu wanashikiliwa na polisi kuhusiana na shambulio hilo lakini hakuna aliyefunguliwa mashtaka ya ubakaji.

    Katika miaka ya hivi karibuni, umaskini umekuwa mojawapo ya vichochezi vya mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni.

    Wengine wanaamini - iwe sawa au vibaya - kwamba wageni ndio sababu ya shida zao nyingi.

    Watu wa Kagiso wanasema wachimba migodi wa kigeni - wanaojulikana kama Zama Zamas - wanahusika na uhalifu katika eneo hilo. Unyanyasaji wa kijinsia wiki iliyopita katika eneo la karibu la Krugersdorp ulizua hali ya wasiwasi na wakaazi wakaitisha maandamano.

    Akielezea msukumo wa maandamano hayo, mkazi mmoja aliambia BBC: "Ninaogopa kwenda kwenye maduka. Polisi wetu hawafanyi lolote."

    "Waache kufanya kile wanachofanya," mwanamke mwingine alisema, akiwalaumu wahamiaji kwa mashambulizi ya kikatili.

    Siku ya Alhamisi asubuhi, polisi, wakiwa chini na kwenye helikopta, walifyatua maguruneti na risasi za mpira ili kuwatawanya umati wenye hasira waliokuwa wakiwafukuza wachimba migodi.

    Watu waliojihami kwa zana za bustani waliwalazimisha kutafuta usalama katika mashimo ya kupitisha hewa ya migodi ya chini ya ardhi.

  12. Taiwan yatayarisha mifumo ya makombora kukabiliana na ‘hatari’ kutoka Uchina

    th

    Chanzo cha picha, EASTERN THEATRE COMMAND via Reuters

    Jeshi la Taiwan limetuma mifumo ya makombora ya ardhini na kutuma ndege na meli kufuatilia hali ilivyo katika pwani yake wizara yake ya ulinzi inasema.

    Inakuja wakati meli nyingi za China na ndege zilivuka mstari wa kati wa Taiwan Strait mapema leo asubuhi.

    Wizara ya ulinzi ya Taiwan ilikariri kauli yake kwamba itaongeza utayari wake wa mapigano lakini haitaomba kutaka vita.

    Uchina yaanzisha tena mazoezi huku Pelosi akiapa kuwa Taiwan haitatengwa

    Siku ya pili ya hali ya hofu kati huko Taiwan na China inatazamiwa kuanza siku yake ya pili ya mazoezi ya kijeshi kuzunguka kisiwa hicho. Mazoezi hayo yanafuatia ziara yenye utata ya mwanasiasa wa chama cha Democratic wa Marekani Nancy Pelosi nchini Taiwan.

    • Akizungumza nchini Japani, Pelosi amesisitiza ziara yake yenye utata mjini Taipei - licha ya onyo kutoka Beijing - haikuchochewa na maslahi binafsi.

    • Pia aliapa kwamba Marekani haitairuhusu China kuitenga Taiwan

    • Siku ya Alhamisi China ilirusha makombora ya balestiki kwenye maji karibu na pwani ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi ya Taiwan, Taiwan inasema.

    • Kisiwa hicho kinasema hatua hiyo, ambayo inazuia meli na ndege kutumia anga, inakiuka mamlaka yake na ni sawa na kuzuiwa.

    • Marekani na Taiwan zote zimeishutumu China kwa kujaribu kubadilisha hali ilivyo katika Mlango-Bahari wa Taiwan

    • Uchina inaiona Taiwan kama jimbo lililojitenga ambalo lazima liunganishwe na bara, kwa nguvu ikiwa ni lazima

    • Marekani haitambui Taiwan kidiplomasia, lakini ina uhusiano mkubwa nayo

    Je, China ilirusha makombora juu ya Taiwan?

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uvumi umekuwa ukiongezeka kwamba China inaweza kuwa imerusha makombora juu ya Taiwan kwa mara ya kwanza.

    Beijing ilirusha makombora 11 ya balestiki kwenye maji karibu na pwani ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa Taiwan siku ya Alhamisi, kama sehemu ya mazoezi yake makubwa zaidi ya kijeshi katika eneo hilo kufuatia ziara ya Bi Pelosi katika kisiwa hicho.

    Makombora ya balistiki hurushwa hadi mwinuko wa juu sana na kisha kufuata njia isiyo na nguvu na mvuto huwaleta kwenye shabaha yao.

    Hakuna makubaliano rasmi kuhusu urefu wa anga ya eneo, mapendekezo yanaanzia takriban kilomita 30 (maili 19) - urefu wa juu zaidi ambao ndege hupaa - hadi 160km (maili 100).

    Vyombo vya habari vya serikali ya China viliripoti siku ya Ijumaa kwamba baadhi ya makombora yalikuwa yameruka juu ya Taiwan. Kamandi ya maonyesho ya kijeshi ya Mashariki ilichapisha mahojiano ya runinga ambapo profesa katika Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Kitaifa alisema kuwa hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kombora kuvuka Taiwan.

    Walakini, hakujawa na taarifa rasmi juu ya hili hadi sasa kutoka kwa serikali ya Uchina au Taiwan.

    Wizara ya ulinzi ya Japan kwanza ilikisia kwamba takriban makombora manne yaliruka juu ya Taiwan. Watano kati yao pia walitua katika eneo la kipekee la kiuchumi la Japan, ubalozi wake nchini Marekani ulisema.

    Unaweza pia kusoma

  13. Brittney Griner: Marekani yaitaka Urusi ikubali dili ya kumuachilia mchezaji nyota wa mpira wa vikapu aliyefungwa jela

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imeitaka Moscow kukubali makubaliano ya kumwachilia mchezaji wa mpira wa vikapu Brittney Griner, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela nchini Urusi.

    Mshindi huyo mara mbili wa Olimpiki alipatikana na hatia ya kumiliki na kusafirisha dawa za kulevya baada ya kukiri kuwa na mafuta ya bangi.

    Msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby alisema pendekezo la Marekani ni "pendekezo zito", lakini hakutoa maelezo zaidi.

    Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kuwa Washington inapeana ubadilishaji wa wafungwa unaohusisha mlanguzi wa silaha wa Urusi.

    Viktor Bout - anayejulikana kama "mfanyabiashara wa kifo" - anatumikia kifungo cha miaka 25 jela nchini Marekani.

    Anaweza kuhamishwa na Washington kwa mamlaka ya Urusi badala ya Griner na mwanajeshi wa zamani wa Marekani Paul Whelan, ripoti zinasema.

    Whelan, ambaye ana hati za kusafiria za Marekani, Uingereza, Kanada na Ireland, alihukumiwa mwaka 2020 hadi miaka 16 jela nchini Urusi baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi.

    Bw Kirby aliwaambia wanahabari kwamba wawili hao walikuwa wakizuiliwa kimakosa na walihitaji kuachiliwa huru .

    Unaweza pia kusoma

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Ijumaa tarehe 5 Agosti 2022