Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waasi wa M23 waingia katika mji wa Uvira, DR Congo

Milio ya risasi na milipuko ya hapa na pale imeripotiwa wakati waasi hao wakiingia katika mji huo muhimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,

Muhtasari

  • Jaji aamuru rekodi za jopo la majaji katika kesi ya Epstein ya 2019 ziachiliwe
  • Ghana yalaani ‘unyanyasaji’ wa wasafiri waliokuwa wakienda Israel
  • Taliban yawaonya Waafghanistan waliovalia mavazi ya Peaky Blinders
  • Waasi wa M23 waingia katika mji wa Uvira, DR Congo
  • Kiongozi wa mapinduzi yaliyoshindwa Benin akimbilia Togo
  • Utawala wa kijeshi Guinea-Bissau wapitisha sheria kumzuia rais na waziri mkuu kushiriki uchaguzi mkuu
  • Mwalimu afukuzwa kazi kwa kuwadanganya wanafunzi kuwa ameua watu 250
  • Marekani yaiunga mkono Japan katika mzozo na China kuhusu tukio la rada
  • Watu 22 wamefariki baada ya majengo mawili kuporomoka Morocco
  • Zelensky: Ukraine 'iko tayari kwa uchaguzi' ikiwa washirika wataihakikishia usalama
  • Marekani yazitaka Thailand na Cambodia kukomesha mapigano
  • Vurugu zashuhudiwa bungeni Brazil kufuatia shinikizo la kupunguza kifungo cha Bolsonaro
  • Australia yaanza kutekeleza marufuku ya mitandao ya kijamii kwa vijana chini ya miaka 16
  • ICG yaonya kuongezeka kwa vurugu Mashariki mwa DRC
  • Viongozi wa Ulaya ni dhaifu - Trump

Moja kwa moja

Martha Saranga & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

  2. Jaji aamuru rekodi za jopo la majaji katika kesi ya Epstein ya 2019 ziachiliwe

    Jaji wa mahaka ya shirikisho huko New York, Marekani ameiamua Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Marekani kutoa hadharani rekodi za jopo la majaji katika kesi ya Jeffrey Epstein ya 2019 inayohusu biashara ya ngono.

    Uamuzi wa Jaji Richard Berman unatokana na sheria mpya iliyopitishwa na Congress inayoihitaji Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kutoa faili kuhusu Epstein kufikia mwishoni mwa wiki ijayo.

    Esptein alishtakiwa kwa biashara haramua ya kingono Julai 2019. Alikufa katika gereza la New York mwezi mmoja baadaye alipokuwa akingoja kesi yake.

    Uamuzi huu unakuja siku moja baada ya jaji mwingine kutoa uamuzi sawa na huo katika kesi ya Ghislaine Maxwell, mshirika wa Epstein ambaye alipatikana na hatia 2021 kwa jukumu lake la kuwezesha unyanyasaji wa kingono uliokuwa ukifanywa wa Epstein.

    Sheria iliyopitishwa na Bunge na kutiwa saina na Rais Donald Trump inaitaka ofisi ya mwendesha mashtaka kuachilia taarifa za uchunguzi zinazohusiana na Epstein ifikapo tarehe 19 Disemba.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Ghana yalaani ‘unyanyasaji’ wa wasafiri waliokuwa wakienda Israel

    Ghana imelaani kile ilichokiita unyanyasaji kwa raia wake katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion nchini Israel baada ya wasafiri kadhaa kuzuiliwa na kufukuzwa, na kusema itachukua hatua.

    Wasafiri wa Ghana "walilengwa kimakusudi na kuteswa kikatili" Jumapili, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ilisema siku ya Jumatano, ikibainisha kuwa raia saba, wakiwemo wajumbe wanne wa bunge, walizuiliwa bila sababu "zinazokubalika" na kuachiliwa baada ya saa za uingiliaji kati wa kidiplomasia, na wengine watatu walifukuzwa.

    Ujumbe wa bunge ulikuwa unahudhuria mkutano wa kimataifa wa usalama wa mtandaoni huko Tel Aviv, huku wasafiri watatu waliofukuzwa walirejea Ghana, kulingana na wizara hiyo.

    "Tabia hii ya kulaaniwa ya Israel ni ya uchokozi, haikubaliki," ilisema taarifa hiyo.

    Wizara ya Mambo ya Nje itawaita maafisa kutoka Ubalozi wa Israel jijini Accra mapema Jumatano ili kueleza kutofurahishwa kwake.

    Wizara hiyo imesema madai ya serikali ya Israel kwamba ubalozi wa Ghana ulishindwa kutoa ushirikiano katika kuwarudisha raia wake "hayakubaliki kabisa," na kuongeza kuwa ujumbe huo umekuwa msikivu na umezingatia sheria za kimataifa.

    Ghana na Israel zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia baada ya uhuru mwaka 1957. Kufuatia Vita vya Waarabu na Israeli vya 1973, Ghana, pamoja na nchi nyingine za Kiafrika, zilikata uhusiano na Tel Aviv. Mahusiano, hata hivyo, yamerejeshwa 1994 na tangu wakati huo yamejumuisha safari na ushirikiano wa kawaida.

  4. Taliban yawaonya Waafghanistan waliovalia mavazi ya Peaky Blinders

    Wanaume wanne wa Afghanistan waliamriwa kuripoti katika wizara ya tabia na wema ya serikali ya Taliban kwa kuvaa mavazi yanayofanana na waigizaji wa tamthilia ya runinga ya Peaky Blinders.

    Marafiki hao waliambiwa mavazi yao "yanakinzana na maadili ya Afghanistan na Kiislamu," msemaji wa Taliban aliiambia BBC, akiongeza kuwa maadili ya Peaky Blinders yanakwenda kinyume na utamaduni wa Afghanistan.

    Katika video zilizochapishwa mtandaoni, wanaume hao ambao wameachiliwa wanaonekana wakiwa wamevalia kofia na suti sawa na zile zinazovaliwa katika tamthilia ya Uingereza ya baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.

    Tangu kutwaa madaraka mwaka 2021, serikali ya Taliban imeweka vikwazo katika maisha ya kila siku kwa mujibu wa tafsiri yao ya sheria za Kiislamu.

    "Hata dangaziri zingekubalika, lakini maadili katika tamthilia ya Peaky Blinders yako kinyume na utamaduni wa Afghanistan," Saiful Islam Khyber, msemaji wa Wizara hiyo aliiambia BBC.

    Wanaume hao, wote wakiwa na umri wa miaka ishirini, waliamriwa kuripoti serikalini huko Jibrail.

    Hawakukamatwa rasmi, "waliitwa tu na kushauriwa na kuachiliwa," Khyber aliiambia CBS News.

    "Tuna maadili yetu ya kidini na kitamaduni, na haswa kwa mavazi tuna mitindo maalum ya kitamaduni," Khyber alisema.

    Wanaume hao walionekana wakiwashukuru maafisa kwa ushauri wao katika video iliyotolewa na wizara baada ya kuhojiwa - ingawa haijulikani ni chini ya hali gani mahojiano hayo yalirekodiwa.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Waasi wa M23 waingia katika mji wa Uvira, DR Congo

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameingia katika mji wa mashariki mwa Congo wa Uvira, kituo muhimu cha jeshi la Congo karibu na mpaka na Burundi, vyanzo vinne wakiwemo wakaazi wawili wameiambia Reuters siku ya Jumatano.

    Milio ya risasi na milipuko ya hapa na pale imeripotiwa wakati waasi hao wakiingia katika mji huo muhimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, katika mashambulizi ambayo yamewalazimu maelfu ya watu kutoroka na kuvuka mpaka na kuingia Burundi.

    Wakaazi na vyanzo vya kijeshi vimesema wanajeshi walikuwa wakikimbia shambulio la Uvira, mji wa mwisho unaoshikiliwa na serikali katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.

    Rais wa Marekani Donald Trump aliafiki makubaliano ya amani wiki iliyopita kati ya Rais wa DR Congo Félix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda ili kumaliza mzozo huo uliodumu kwa muda mrefu lakini mapigano yameendelea.

    Maduka na shule zimefungwa, huku wakazi waliojawa na hofu wakisalia majumbani huku kukiwa na hofu kwamba waasi wamechukua udhibiti wa baadhi ya majengo ya serikali.

    Wakazi wameiambia BBC kuna milio ya risasi katika mji huo ulio kilomita 27 tu kutoka mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.

    Duru za kijeshi na usalama zilisema wapiganaji hao waasi walisonga mbele kutoka kaskazini, karibu na mpaka wa Burundi.

  6. Kiongozi wa mapinduzi yaliyoshindwa Benin akimbilia Togo

    Kiongozi wa mapinduzi yaliyoshindwa nchini Benin ametafuta hifadhi katika nchi jirani ya Togo, afisa mkuu wa serikali ya Benin ameiambia Reuters siku ya Jumatano, akitaka arejeshwe mara moja.

    Wanajeshi walichukua udhibiti wa kituo cha televisheni cha serikali ya Benin kwa muda mfupi Jumapili asubuhi na kudai kuwa wamemuondoa madarakani Rais Patrice Talon, ingawa wanajeshi wa Benin, wakisaidiwa na vikosi vya anga vya Nigeria, ujasusi wa Ufaransa na usaidizi wa vifaa, walizuia jaribio hilo.

    Wanajeshi hao walimtaja Kanali Tigri Pascal kuwa kiongozi wa mapinduzi. Awali alikuwa hajulikani aliko.

    Wizara ya mambo ya nje ya Togo haijasema chochote.

    Wapangaji wa mapinduzi walijaribu kumteka Talon, na walikaribia vya kutosha hadi Talon akashuhudia mapigano makali, taarifa ya serikali ya Benin ilisema Jumatatu.

    Pia walifanikiwa kuwateka nyara maafisa wawili wakuu wa kijeshi ambao waliachiliwa Jumatatu asubuhi, taarifa hiyo ilisema.

    Msemaji wa serikali ya Benin, Wilfried Leandre Houngbedji, alisema Jumapili kwamba watu 14 wamekamatwa kuhusiana na jaribio la mapinduzi.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Utawala wa kijeshi Guinea-Bissau wapitisha sheria kumzuia rais na waziri mkuu kushiriki uchaguzi mkuu

    Utawala wa kijeshi wa Guinea-Bissau umepitisha katiba ya mpito ya miezi 12 ambayo inawazuia rais wa mpito na waziri mkuu kugombea katika uchaguzi ujao, wiki mbili baada ya maafisa wa jeshi kufanya mapinduzi ambayo yaliisimamisha katiba.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, hati hiyo yenye vifungu 29, iliyochapishwa Jumanne, inataka uchaguzi wa rais na wabunge ufanyike mwishoni mwa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja, na tarehe ya kupiga kura itawekwa na rais wa mpito.

    Maafisa wa jeshi nchini Guinea-Bissau, walimpindua Rais Umaro Sissoco Embalo Novemba 26 na kumteua Meja-Jenerali Horta Inta-a kama rais wa mpito siku iliyofuata.

    Ilidio Vieira Te, mtumishi wa umma na waziri wa zamani wa fedha, aliteuliwa kuwa waziri mkuu siku moja baadaye.

    Mapinduzi hayo yalifanyika siku moja kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais na wabunge.

    Uongozi wa kijeshi utadhibiti mageuzi ya kisheria na kitaasisi wakati wa mpito, ikiwa ni pamoja na kuandaa marekebisho ya katiba iliyosimamishwa, kuunda Mahakama Mpya, kubadilisha kanuni za vyama vya siasa na kusimamia uteuzi wa wasimamizi wapya wa uchaguzi, kwa mujibu wa hati hiyo.

    Baraza la Kitaifa la Mpito lenye watu 65, wakiwemo maafisa 10 wakuu wa jeshi wanaowakilisha Kamandi Kuu ya Kijeshi, watafanya kazi kama chombo cha kutunga sheria cha mpito, hati hiyo inasema.

    Guinea-Bissau, taifa dogo la pwani ya Afrika Magharibi kati ya Senegal na Guinea, limekumbwa na ukosefu wa utulivu tangu kupata uhuru kutoka Ureno mwaka 1974, huku rais mmoja pekee ndiye amewahi kumaliza muhula kamili wa uongozi.

    Kufuatia mapinduzi nchini Guinea mwaka 2021, katiba ya mpito ilieleza kuwa kiongozi wa mapinduzi Mamady Doumbouya hatoweza kugombea katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo.

    Hata hivyo nchi hiyo ilipitisha katiba mpya mwezi Septemba ambayo ilitupilia mbali kipengele hicho, na Doumbouya atagombea katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 28, 2026.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mwalimu afukuzwa kazi kwa kuwadanganya wanafunzi kuwa ameua watu 250

    Mchezaji wa raga wa Wales na mwalimu wa shule amepigwa marufuku kufundisha kwa miaka miwili baada ya kuwaambia wanafunzi kuwa ameua zaidi ya watu 250 akiwa mdunguaji katika kijeshi.

    Scott John Trigg-Turner, 44, alitoa madai ya uwongo kwa wanafunzi wa mwaka wa 8 huko Newport kwamba alikuwa katika jeshi la majini la Marekani, akiitwa 'Kill Switch' na bado anamiliki bunduki.

    Trigg-Turner amekanusha kuwa amekosa maadili na aliwaambia wachunguzi kwamba maneno yake "yalitafsiriwa vibaya."

    Mwalimi mwenzake Sharon Davies alisema alikuwa na mashaka na Trigg-Turner baada ya kusikia hadithi alizowaambia wanafunzi wa Shule ya Bassaleg mwaka 2023, ikiwa ni pamoja na kujisifu kuhusu kuua "zaidi ya watu 250."

    Katika barua pepe kwa Baraza la Wafanyakazi wa Elimu Wales (EWC) lililochunguza madai yake, Trigg-Turner alisema "Sijawahi kuvuka mipaka ya kitaaluma na siwezi kufanya hivyo."

    Jopo la EWC pia liliambiwa alifika kwa kuchelewa na alitoka darasani mapema bila makubaliano mara kadhaa na alitoa maelezo yasiyolingana kwa wenzake kuhusu jinsi alivyoanza kutumia viti vya magurudumu.

    Ni Mchezaji mashuhuri wa kimataifa wa Wales wa raga ya kiti cha magurudumu, pia amechezea timu ya magurudumu ya Wigan Warriors na Torfaen Tigers.

    Hakuwepo kwenye kikao hicho, hakuwakilishwa na hajatoa jibu rasmi.

    Kikao cha EWC kiliambiwa wakati wa uchunguzi Trigg-Turner alikanusha kuwa na bunduki nyumbani kwake na wala hakuwahi kusema ana bunduki.

    Aliongeza kuwa kuhusu kutaja jeshi alikuwa anamzungumzia mwanafamilia na kusema maoni yake kwa darasa yamechukuliwa vibaya.

    Trigg-Turner, ambaye baadaye alikwenda kufanya kazi katika Chuo cha Cardiff na Vale baada ya kuondoka Bassaleg, ameondolewa kwenye rejista ya EWC katika kategoria zote mbili za mfanyakazi katika shule na vyuo vya elimu ya juu.

    Mwenyekiti wa jopo Helen Beard-Robbins amesema: "Kuna ushahidi juu ya uongo aliowaambia wanafunzi, wafanyakazi wenzake na meneja wake."

    Jopo hilo liliamua Trigg-Turner hatorejeshwa kazini kwa miaka miwili.

    Ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi huo ndani ya siku 28.

  9. Marekani yaiunga mkono Japan katika mzozo na China kuhusu tukio la rada

    Marekani kwa mara ya kwanza imeikosoa China kwa kuvuruga rada za ndege za kijeshi za Japan wakati wa mazoezi ya wiki jana, tukio ambalo majirani hao wa Asia wamelitolea maelezo tofauti huku kukiwa na mvutano unaozidi kuongezeka.

    Mazoezi hayo karibu na visiwa vya Okinawa vya Japan yanakuja baada ya Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi kuanzisha mzozo na Beijing mwezi uliopita kwa matamshi yake juu ya jinsi Tokyo inavyoweza kujibu shambulio la China dhidi ya Taiwan.

    China inadai Taiwan ni eneo lake na haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu kuchukua udhibiti wa kisiwa hicho, ambacho kiko zaidi ya kilomita 100 kutoka eneo la Japani na kimezungukwa na njia za bahari ambazo Tokyo inazitegemea.

    "Hatua za China hazileti amani na utulivu wa kikanda," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani alisema Jumanne, akizungumzia tukio hilo.

    "Ushirikiano wa Marekani na Japan una nguvu kuliko hapo awali. Ahadi yetu kwa mshirika wetu Japani haiyumbi, na tunawasiliana kwa karibu kuhusu hili na masuala mengine."

    Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japan Minoru Kihara alikaribisha matamshi hayo, akisema "yanaonyesha muungano wenye nguvu wa Marekani na Japan".

    Akizungumza jijini Beijing, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun aliepuka kukosoa moja kwa moja matamshi ya Marekani, akisisitiza kwamba shughuli za mafunzo na mazoezi ya China zinafuata sheria za kimataifa na zinaendeshwa kwa usalama.

    Siku ya Jumanne Japan ilipaisha ndege za kivita ili kufuatilia vikosi vya anga vya Urusi na China vilivyokuwa vikifanya mazoezi ya pamoja.

    Siku ya Jumatano, walinzi wa pwani wa Japan walisema meli zake ziliona meli nne za walinzi wa pwani ya China ndani ya kile inachosema ni eneo lake karibu na visiwa vya Senkaku vinavyozozaniwa.

    Kikosi cha ulinzi wa pwani cha China kimesema kinatekeleza operesheni "kisheria" ili kulinda haki na maslahi ya nchi. China inaviita visiwa hivyo kuwa ni Diaoyu.

    Ndege za kivita za China zilielekeza rada zao kwenye ndege za Japan siku ya Jumamosi. Hatua kama hizo ni za kutisha kwa sababu zinaashiria shambulio na zinaweza kuilazimisha ndege inayolengwa kuchukua hatua ya kukwepa.

    Beijing, hata hivyo, ilisema ndege ya Japan ilikaribia mara kwa mara na kuvuruga shughuli za jeshi la wanamaji la China lilipokuwa likifanya mafunzo yaliyotangazwa hapo awali mashariki mwa Miyako.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Watu 22 wamefariki baada ya majengo mawili kuporomoka Morocco

    Takribani watu 22 wamefariki na makumi kujeruhiwa siku ya Jumatano baada ya majengo mawili kuporomoka huko Fez, mojawapo ya miji mikongwe zaidi Morocco, vimeripoti vyombo vya habari vya serikali.

    Mamlaka za mkoa wa Fez ziliripoti majengo mawili ya karibu ya ghorofa nne yameporomoka usiku, limesema shirika la habari la serikali.

    Majengo hayo yalikaliwa na familia nane na yalikuwa katika kitongoji cha Al-Mustaqbal.

    Mara tu walipoarifiwa kuhusu tukio hilo, mamlaka za mitaa, idara za usalama na vitengo vya ulinzi wa raia walikwenda eneo la tukio na kuanza mara moja shughuli za utafutaji na uokoaji.

    Fez, mji mkuu wa zamani katika karne ya nane na mji wa tatu wenye wakazi wengi nchini humo, ulikumbwa na wimbi la maandamano miezi miwili iliyopita dhidi ya serikali kutokana na kuzorota kwa hali ya maisha na huduma duni za umma.

    Tovuti ya habari ya serikali ya SNRT imeripoti "kuwa majengo yaliyoporomoka yalikuwa na dalili za kupasuka kwa muda mrefu, bila hatua madhubuti kuchukuliwa."

    Pia unaweza kusoma:

  11. Zelensky: Ukraine 'iko tayari kwa uchaguzi' ikiwa washirika wataihakikishia usalama

    Ukraine iko "tayari kwa uchaguzi", Rais Volodymyr Zelensky amesema, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kurejelea madai kwamba Kyiv ilikuwa "ikitumia vita" kama mbinu ya kuepuka kufanya uchaguzi.

    Muhula wa miaka mitano wa Zelensky kama rais ulipaswa kumalizika Mei 2024, lakini uchaguzi umesitishwa nchini Ukraine tangu sheria ya kijeshi ilipotangazwa baada ya uvamizi wa Urusi.

    Akizungumza na waandishi wa habari kufuatia maoni ya Trump katika mahojiano ya kina na Politico, Zelensky alisema ataomba mapendekezo yaandaliwe ambayo yanaweza kubadilisha sheria.

    Uchaguzi unaweza kufanyika katika siku 60 hadi 90 zijazo ikiwa usalama wa kura utahakikishwa kwa msaada wa Marekani na washirika wengine, alisema.

    "Ninaomba sasa, na ninasema hili waziwazi, Marekani inisaidie, labda pamoja na wenzetu wa Ulaya, kuhakikisha usalama wa uchaguzi wenyewe," aliwaambia waandishi wa habari.

    "Ninaamini suala la uchaguzi nchini Ukraine linategemea kwanza kabisa watu wetu, na hili ni swala la watu wa Ukraine, si watu wa nchi nyingine. Kwa heshima yote kwa washirika wetu," alisema.

    Soma zaidi:

  12. Marekani yazitaka Thailand na Cambodia kukomesha mapigano

    Marekani imeziambia Thailand na Cambodia "kukomesha uhasama mara moja" huku mapigano ya mpaka yakiendelea kwa siku ya tatu, na kuua watu wasiopungua 10 na mamia kwa maelfu ya watu wakihama makazi yao.

    Mataifa hayo mawili lazima yafuate hatua za kumaliza mvutano zilizoainishwa katika makubaliano ya amani yaliyoratibiwa na Rais wa Marekani Donald Trump mnamo Oktoba, Waziri wa Mambo ya kigeni Marco Rubio alisema.

    Trump pia amesema kwamba "angewapigia simu" ili kusimamisha mapigano hayo, ambayo yameongezeka zaidi tangu yale yaliyozuka Julai na kuua watu kadhaa.

    Nchi zote mbili zimetupiana lawama kwa kuchochea upya mapigano hayo, ambayo yameshuhudia mashambulizi ya angani na ufyatuaji risasi.

    Jumla ya idadi ya vifo katika siku tatu za uhasama ni 10 - saba kwa upande wa Cambodia na watatu kutoka Thailand.

    Maafisa wa Thailand waliwahamisha zaidi ya watu 400,000, huku upande wa Phnom Penh ukisema watu 100,000 upande wa Cambodia wamehamishiwa kwenye makazi.

    Soma zaidi:

  13. Vurugu zashuhudiwa bungeni Brazil kufuatia shinikizo la kupunguza kifungo cha Bolsonaro

    Bunge la Brazil lilikumbwa na vurugu Jumanne huku wabunge wa kihafidhina wakiendelea kushinikiza sheria ambayo ingepunguza adhabu ya kifungo cha rais wa zamani wanchi hiyo Jair Bolsonaro.

    Mbunge mmoja wa mrengo wa kushoto aliondolewa kwa nguvu na polisi baada ya kujaribu kuvuruga shughuli, huku video zikionesha hali ya taharuki ikizuka wakati maafisa usalama wakijaribu kurejesha utulivu.

    Bolsonaro alianza kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 27 jela mwezi Novemba kwa kujaribu kupanga mapinduzi kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2022.

    Washirika wake wa kihafidhina bungeni wamependekeza sheria ambayo ingepunguza adhabu kwa makosa yanayohusiana na mapinduzi, na pia kuwaachilia huru wafuasi kadhaa wa Bolsonaro waliovamia majengo ya serikali muda mfupi baada ya kuondoka madarakani.

    Wakati huo huo, hati za mahakama zilionesha kuwa timu ya wanasheria wa Bolsonaro iliwasilisha ombi rasmi kwa mahakama imruhusu kuondoka gerezani kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

    Rufaa hiyo inarejelea ombi la rais huyo wa zamani kuruhusiwa kutumikia kifungo chake chini ya kifungo cha nyumbani kwa sababu za kiafya.

    Bolsonaro alitumia muda wake katika chumba cha wagonjwa mahututi mapema mwaka huu kufuatia upasuaji wa utumbo, na alidungwa kisu tumboni mwaka wa 2018 wakati wa mkutano wa hadhara.

    Soma zaidi:

  14. Australia yaanza kutekeleza marufuku ya mitandao ya kijamii kwa vijana chini ya miaka 16

    Australia imekuwa nchi ya kwanza duniani kupiga marufuku ufikiaji wa mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16, hatua iliyopokelewa vyema na wazazi wengi na watetezi wa haki za watoto lakini ikikosolewa na makampuni ya teknolojia na watetezi wa uhuru wa kujieleza.

    "Ni siku ya kujivunia kuwa waziri mkuu wa Australia," anasema Anthony Albanese wakati marufuku ya akaunti za mitandao ya kijamii kwa walio chini ya miaka 16 inaanza kutekelezwa kwa mara ya kwanza duniani.

    Miongoni mwa majukwaa yanayohitajika kutekeleza sheria hii mpya ni Pamoja na Instagram, Facebook, Threads, X, Snapchat, Kick, Twitch, TikTok, Reddit na YouTube.

    Lulu mwenye umri wa miaka 15 ameionesha BBC jinsi akaunti zake zilivyogoma kufunguka muda mfupi baada ya kuanza kutekelezwa kwa hatua hiyo.

    “Nilikuwa na hasira sasa ninajitahidi kuzoea hali hii ninasikia huzuni”binti mwingine alieleza

    Serikali inasema marufuku hiyo inalenga kuwalinda vijana kutokana na maudhui hatarishi, lakini wakosoaji wanapendekeza kwamba inaweza kuwatenga vijana walio katika mazingira magumu na kuwasukuma watoto kwenye maeneo yasiyodhibitiwa za mtandao.

    Serikali inasema marufuku hiyo inalenga kuwalinda vijana kutokana na maudhui hatarishi, lakini wakosoaji wanapendekeza kwamba inaweza kuwatenga vijana walio katika mazingira magumu na kuwasukuma watoto kwenye maeneo yasiyodhibitiwa kwa njia za kimtandao.

    “Hii ni hatua ya kijasiri ambayo nchi zingine nyingi zinaiangalia kwa makini lakini bado haijafahamika kwa namna gani serikali itapima mafanikio yake”, anaandika mwandishi wa BBC Australia.

    Soma zaidi:

  15. M23 waripotiwa kuingia Uvira, maelfu ya raia wakimbilia Burundi

    Waasi wa M23 waliingia katika mji muhimu wa Uvira, mashariki mwa Jamhuri ya demokrasia ya Congo, Jumanne usiku na kusababisha maelfu ya wakazi wakimbilie nchi jirani ya Burundi.

    Mashuhuda na vyanzo vya usalama vinasema wapiganaji hao waliingia Uvira kutoka upande wa kaskazini, wakati huu Marekani na nchi za Ulaya zikitaka mara moja waasi hao kusitisha mashambulizi na Rwanda kuondoa vikosi vyake mashariki mwa DRC.

    Hata hivyo Rwanda kupitia Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa imekanusha kuhusika kokote katika ukiukaji wa makubaliano wa hivi karibuni wa usitishaji mapigano mashariki mwa DRC.

    Awali Shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo (ICG) limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuzuka upya kwa mapigano katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya demokrasia ya Congo, kufuatia shambulio jipya linalodaiwa kutekelezwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda karibu na eneo la Uvira, Kivu Kusini.

    Limesema hatua hii inaweza kutatiza zaidi utulivu wa kanda yote, ikizingatiwa ukaribu wa eneo hilo na mipaka ya Burundi.

    ICG imesisitiza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matumizi ya ndege zisizo na rubani huku ikionya kuwa teknolojia hii imeongeza kiwango cha mapigano na kuhatarisha zaidi usalama wa raia.

    “Matumizi hayo ni ishara ya hatua mpya ya hatari katika mzozo ambao tayari umesababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao” Ilieleza taarifa ya ICG

    Aidha, imelitaka jeshi la RDF kujiondoa kikamilifu kutoka ardhi ya DRC, huku M23 ikihimizwa kurudi kwenye maeneo yake ya awali na kuheshimu azimio la kikanuni lililosainiwa Doha 19 Julai 2025.

    “Pande zote zikumbuke wajibu wao wa kulinda raia na kuzingatia kikamilifu Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2773, hasa kipengele cha kuheshimu mipaka na uadilifu wa eneo la DRC” ilieleza taarifa ya ICG

    Limezitaka serikali na makundi husika kutekeleza kikamilifu ahadi za Makubaliano ya Washington ya 4 Desemba 2025 na kuchukua hatua za haraka za kupunguza mvutano.

    Raia wa Congo na watafiti wanashuku kuwa Rwanda inahimiza ukosefu wa utulivu katika eneo hilo ili kudhoofisha uwezo wa serikali ya Congo wa kudhibiti usafirishaji haramu wa maliasili (madini, wanyama na mimea).

    Hata hivyo Rwanda imekuwa ikikanusha madai haya mara kwa mara na kuthibitisha tena kujitolea kwake kwa mifumo ya kikanda ya kupambana na unyonyaji haramu wa maliasili.

    Soma zaidi:

  16. Trump: Ulaya inaporomoka na viongozi wake ni dhaifu

    Rais wa Marekani Donald Trump amewakosoa viongozi wa Ulaya kwa kuwaita "dhaifu" na kusema Marekani inaweza kupunguza msaada kwa Ukraine.

    Katika mahojiano ya kina na mtandao wa habari Politico, Trump alisema nchi za Ulaya "dhaifu" zimeshindwa kudhibiti uhamiaji au kuchukua hatua madhubuti kukomesha vita vya Ukraine na Urusi, akiwashutumu kwa kuiacha Kyiv ipigane "hadi ianguke".

    Viongozi wa Ulaya wamefanya majaribio ya kuonyesha jukumu katika juhudi zinazoongozwa na Marekani za kukomesha vita hivyo, ambavyo wanahofia vitaathiri maslahi ya muda mrefu ya bara hilo kwa ajili ya suluhisho la haraka.

    Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Uingereza Yvette Cooper alisema alichokiona barani Ulaya ni "uimara", akitoa mfano wa uwekezaji katika ulinzi pamoja na ufadhili kwa Kyiv.

    Aliongeza kuwa marais wawili walikuwa "wakishughulikia mchakato wa amani" akimrejelea Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky huku "rais mmoja Putin hadi sasa akiendelea tu kuzidisha mgogoro huo kwa kutekeleza mashambulizi zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora".

    Trump aliendelea kuongeza shinikizo kwa Zelensky kuunga mkono makubaliano ya amani, na akamhimiza "kuwa tayari kutoa ushirikiano" kwa kukabidhi eneo kwa Moscow.

    Urusi ilizindua uvamizi wake kamili nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

    Zelensky, akiandika kwenye mtandao wa X baadaye Jumanne, alisema Ukraine na Ulaya zilikuwa zikifanyia kazi kikamilifu "vipengele vyote vya hatua zinazowezekana ili kukomesha vita", kwamba vipengele vya Ukraine na Ulaya vya mpango huo sasa vilikuwa vimeendelezwa zaidi.

  17. Hujambo karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo