Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Serikali Benin yazima jaribio la mapinduzi

Milio ya risasi ilisikika asubuhi ya leo katika mji wa Cotonou, na wanajeshi walitangaza kupindua serikali kupitia televisheni lakini sasa Waziri wa mambo ya ndani anasema mapinduzi yameshindwa na wanajeshi 13 waliofanya jaribio hilo wamekamatwa.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Serikali Benin yazima jaribio la mapinduzi

    Serikali ya Benin imetangaza kuwa imefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi lililofanywa na baadhi ya wanajeshi wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

    “Jeshi la Benin na viongozi wake, wakiwa waaminifu kwa kiapo chao, wamesalia kuwa waaminifu kwa jamhuri,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Alassane Seidou, katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni.

    Mapema Jumapili, kundi la wanajeshi lilitoa matangazo kwenye runinga yakidai kwamba yamepindua na kumvua madaraka Rais Patrice Talon. Mashuhuda waliiambia BBC kwamba walisikia milio ya risasi na baadhi ya wanahabari wa televisheni ya taifa kushikiliwa mateka.

    Mshauri wa rais ameieleza BBC kuwa kiongozi huyo yuko salama na yuko katika ubalozi wa Ufaransa. “Asubuhi ya Jumapili, tarehe 7 Desemba 2025, kundi dogo la wanajeshi lilianzisha uasi uliolenga kuyumbisha nchi na taasisi zake,” Seidou alisema.

    Hata hivyo, wanajeshi watiifu serikalini waliweza “kurejesha udhibiti wa hali hiyo na kuzuia jaribio hilo,” aliongeza.

    Helikopta zimeonekana zikizunguka juu ya mji mkuu wa Cotonou makao ya serikali na barabara zimefungwa huku kukiwa na ulinzi mzito wa jeshi katika mitaa kadhaa.

    Benin, koloni la zamani la Ufaransa, kwa muda mrefu imejulikana kama moja yanchi zenye demokrasia thabiti barani Afrika.

    Ni moja ya nchi wazalishaji wakubwa wa pamba barani, ingawa inasalia miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani.

  2. Wanajeshi Benin watangaza kupindua Serikali

    Jaribio la mapinduzi linaendelea nchini Benin, baada ya kundi la wanajeshi kudai kwamba wamemwondoa Rais Patrice Talon madarakani na sasa wanachukua usimamizi wa nchi.

    Wanajeshi hao, waliounda kile walichokiita “Kamati ya kijeshi”, walionekana kwenye runinga ya taifa Jumapili asubuhi wakitangaza kwamba wamesitisha katiba, kuvunja serikali na kufuta shughuli za vyama vya siasa.

    Walijitetea kwa kusema kuwa hatua hiyo imetokana na kutoridhishwa na namna Rais Talon alivyokuwa akiiongoza nchi. Inadaiwa kuwa kundi hilo linaongozwa na Luteni Kanali Pascal Tigri.

    Hadi sasa haijafahamika Rais Talon alipo, kwani wanajeshi wameripotiwa kufika katika makazi yake mjini Cotonou. Hata hivyo, shirika la habari la AFP limemnukuu msemaji wa Ikulu likisema kuwa rais yuko salama na jeshi linaanza kurejesha udhibiti.

    Milio ya risasi ilisikiwa asubuhi katika mji huo, huku taarifa zikisema helikopta za kijeshi zilikuwa zikizunguka angani juu ya Cotonou.

    Ubalozi wa Ufaransa umewataka raia wake kubaki majumbani kwa ajili ya usalama wao.

    Benin inatarajiwa kufanya uchaguzi wa urais Aprili 2026, ambao ndiyo mwisho wa muhula wa Rais Talon. Ameshathibitisha kutogombea muhula wa tatu na tayari amemtaja mrithi anayemtaka.

    Jaribio hili la mapinduzi nchini Benin limekuja siku chache tu baada ya Rais Umaro Sissoco Embaló kupinduliwa katika nchi jirani ya Guinea-Bissau.

    Katika miaka ya karibuni, Afrika Magharibi imekumbwa na misururu ya mapinduzi, hali inayoongeza hofu ya kuzorota kwa usalama wa eneo hilo.

  3. Moto waua 25 katika klabu ya usiku Goa, wakiwemo wafanyakazi na watalii

    Moto mkubwa uliotokea katika klabu maarufu ya usiku katika eneo la pwani la Goa, India, umeua watu 25, kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo.

    Idadi kubwa ya waathiriwa wanadaiwa kuwa ni wafanyakazi wa klabu hiyo inayoitwa Birch by Romeo Lane, iliyoko karibu na ufukwe maarufu, ingawa watalii pia wanahofiwa kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

    Polisi wanaamini kuwa mlipuko wa mtungi wa gesi katika jiko la klabu hiyo ndiyo uliosababisha moto mkubwa ulioteketeza jengo hilo Jumamosi usiku wa manane kwa saa za eneo hilo.

    Asubuhi ya leo Jumapili, maafisa walithibitisha kuwa idadi ya vifo imeongezeka kutoka 23 hadi 25. Mashuhuda waliozungumza na BBC walisimulia hali ya taharuki katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za burudani za usiku.

    Mkuu wa Polisi Goa, Alok Kumar, alisema: "Moto ulikuwa umekolea zaidi katika eneo la jikoni lililopo ghorofa ya chini."

    Miili mingi ilipatikana karibu na eneo la jikoni, jambo linaloashiria kuwa waathiriwa wengi walikuwa wafanyakazi wa klabu, amesema Alok Kumar.

    Klabu hiyo ilikuwa imejaa kutokana na kuwa na onyesho la DJ maarufu wa muziki wa Bollywood. Eneo hilo linajulikana kwa kuwa na klabu nyingi za usiku zinazojaza watu wengi wakati wa usiku.

  4. Waliokufa kwa mafuriko Indonesia wafikia 900

    Idadi ya vifo nchini Indonesia kutokana na mafuriko ya hivi karibuni imeongezeka na kufikia 900, huku mamia wakiwa bado hawajapatikana.

    Zaidi ya nyumba 100,000 zimeharibiwa baada ya kimbunga chenye nguvu kugonga Ghuba ya Malaka wiki iliyopita, kikiambatana na mvua kubwa na mmomonyoko wa ardhi katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Asia ya Kusini-Mashariki.

    Juhudi za kuwafikia watu walioko kwenye maeneo ambayo bado mawasiliano yamekatika zinaendelea, huku misaada ikihitajika pamoja.

    Mafuriko haya ni mojawapo ya matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyoikumba Asia katika wiki za hivi karibuni, huku jumla ya vifo katika nchi za Sri Lanka, Thailand, Malaysia na Vietnam ikikaribia 2,000.

    Huko Aceh Tamiang, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi Indonesia, waliokolewa wamesema kwamba vijiji vilimezwa kabisa na maji yanayotiririka kwa kasi.

    Mmoja waliokolewa katika Kijiji cha Lintang Bawah aliiambia BBC kwamba watu waliparamia na kuishi juu ya paa za nyumba zao.

    Fitriana alisema: "Kulikuwa pia na wale waliokaa juu ya paa za nyumba zao pamoja na watoto wao wa miaka minne, kwa siku tatu bila kula au kunywa."

    Aliongeza kuwa karibu nyumba 90% za kijiji chake zimeharibiwa, zikiacha familia 300 bila mahali pa kwenda.

  5. "Natupiwa zigo la lawama Liverpool" – Mo Salah

    Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, ameeleza kuwa anahisi anashushiwa heshima yake na kuwekwa njia panda na klabu hiyo, huku uhusiano wake na kocha mkuu Arne Slot ukiwa vipande vipande.

    Salah, ambaye amefunga magoli 250 katika mechi 420 alizochezea Liverpool, alikuwa benchi katika mchezo wa usiku wa Jumamosi waliokwenda sare ya 3-3 dhidi ya Leeds United, ukiwa ni mchezo wa tatu mfululizo kuanzia benchi.

    Baada ya mchezo huo, katika mahojiano ya kipekee na waandishi wa habari, Salah alisema: "Inaonekana wazi kwamba kuna mtu aliyetamani nishutumiwe kwa kila kitu. Nilikuwa na uhusiano mzuri na kocha, lakini ghafla hatuna uhusiano wowote. Sijui ni kwa nini, lakini inaonekana kuna mtu asiyetaka nikae klabuni. Nahisi kama klabu imenitupia mzigo wa lawama. Hivyo ndivyo ninavyojisikia."

    Licha ya hali hiyo, Salah aliweka wazi mapenzi yake kwa klabu: "Nitakuwa daima na kikosi hiki. Watoto wangu pia wataiunga mkono. Ninapenda klabu hii sana na daima nitapenda."

    Aliongeza kuwa hali hiyo haikubaliki kwake: "Sijui kwa nini inatokea hivi. Hii ni kama natupiwa zigo la lawama. Sidhani mimi ndiye tatizo; nimefanya mengi kwa klabu hii. Si lazima nishindane kila siku kupata nafasi yangu kwa sababu nimeipata kwa bidii. Miimi si mkubwa kuliko wengine, lakini nimeipata nafasi yangu. Ni mpira wa miguu, ndivyo ilivyo."

    Salah, ambaye atashiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kuanzia Desemba 15, alisema haajaamua hatma yake ya baadaye Liverpool, licha ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili mnamo Aprili.

  6. Watoto 33 wauawa shule ya Chekechea ikishambuliwa

    Shambulio la ndege isiyo na rubani katika mji wa Kalogi, eneo la Kordofan Kusini nchini Sudan, limeripotiwa kulenga chekechea na kuua watu zaidi ya 50, wakiwemo watoto 33.

    Mtandao wa Madaktari wa Sudan pamoja na jeshi wamelilaumu kundi la Rapid Support Forces (RSF) kwa shambulio hilo, ingawa RSF haijatoa tamko.

    RSF nayo imeilaumu jeshi kwa kushambulia soko na kituo cha mafuta katika mpaka wa Adre, Darfur, kwa kutumia ndege isiyo na rubani siku ya Ijumaa. Sudan imekuwa ikikumbwa na vita tangu Aprili 2023 baada ya mzozo wa madaraka kati ya jeshi na RSF, ambao hapo awali walikuwa washirika.

    Wizara ya mambo ya nje inayounga mkono jeshi imesema shule hiyo ya chekechea ilishambuliwa mara mbili kwa makombora huku raia pamoja na wahudumu wa afya waliokimbilia kuokoa watoto walishambuliwa tena.

    UNICEF imelaani tukio hilo, ikisema kuua watoto shuleni ni ukiukwaji mbaya wa haki za mtoto. Shirika hilo limezitaka pande zote kusitisha mashambulizi mara moja na kuruhusu misaada kufika kwa usalama.

  7. Mazungumzo ya mpango wa amani na Marekani yanasonga mbele - Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema amekuwa na mazungumzo ya simu “yenye kujenga” na Steve Witkoff, mjumbe wa amani wa Rais Donald Trump, pamoja na mkwe wa Trump, Jared Kushner.

    Zelensky alisema walijadili namna ya kuhakikisha Urusi inazingatia makubaliano yoyote ya kumaliza vita, na akaeleza kuwa Ukraine imejitolea kuendelea kufanya kazi na Marekani.

    Maafisa wa Ukraine waliojiunga pia kwenye mazungumzo hayo ya simu kutoka Miami wapo huko katika siku ya tatu ya mazungumzo na wajumbe wa Marekani kuhusu mpango wa kuikaribisha Ukraine kwenye makubaliano ya amani.

    Hata hivyo, Urusi haijaonyesha dalili za kutoa ustahimilivu wowote na inaendelea kushambulia Ukraine kwa makombora na ndege zisizo na rubani.

    Zelensky alisema kupitia X kwamba Ukraine itaendelea kushirikiana kwa nia njema na Marekani ili kufanikisha mpango huo wa amani. Wakati huohuo, washirika wa Umoja wa Ulaya waliilaani Urusi baada ya shambulio kubwa la anga usiku ambapo miundombinu ya reli na nishati iliharibiwa katika maeneo kadhaa ya Ukraine.

    Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema amezungumza na Zelensky na kuahidi “mshikamano,” akiongeza kuwa Ufaransa itafanya kazi na washirika kuhakikisha hatua za kupunguza mvutano na kusukuma mbele usitishaji mapigano. Macron pia alithibitisha kuwa atajiunga na Zelensky, Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kwa mazungumzo London Jumatatu kuhusu usalama wa Ukraine baada ya vita.

    Wakati huohuo, mazungumzo ya Florida kati ya maafisa wa Ukraine na Marekani kuhusu mpango wa amani unaoungwa mkono na Washington yanaendelea. Witkoff alisema mazungumzo yao na Rustem Umerov, waziri wa usalama la Ukraine, yamekuwa “yenye kujenga” na wamekubaliana juu ya mfumo wa mipango ya usalama. Hata hivyo, mustakabali wa kumaliza vita walisema unategemea utayari wa Urusi kuchukua hatua za kupunguza mvutano na kusitisha umwagikaji damu.